Mzozo wa Ukraine: Putin aamuru kikosi cha nyuklia cha Urusi kuwa tayari

Chanzo cha picha, AFP
- Author, Gordon Corera
- Nafasi, BBC
Rais wa Urusi Vladimir Putin ameamuru jeshi la Urusi kuweka vikosi vyake vya nyuklia katika "tahadhari maalum" - kiwango cha juu cha tahadhari kwa Vikosi vya Kimkakati vya Kombora vya Urusi.
Akizungumza na maafisa wakuu wa kijeshi, akiwemo Waziri wa Ulinzi Sergei Shoigu, alisema mataifa ya Magharibi yamechukua "hatua zisizo za kirafiki" kwa Urusi na kuweka "vikwazo visivyo halali".
Rais wa Urusi Vladmir Putin ameamuru usimamizi wa jeshi kuweka kikosi maalum cha nyuklia katika hali "maalum" ya tahadhari.
Hii ni baada ya kile ambacho Moscow inakiita "taarifa za uchokozi" za nchi za muungano wa Nato.
Kiongozi huyo wa Urusi tayari alikuwa ametoa onyo fiche kwamba yuko tayari kutumia silaha za nyuklia anapoanza uvamizi wake nchini Ukraine.

Chanzo cha picha, Getty Images
Wiki iliyopita, alionya kwamba "yeyote anayejaribu kutuzuia" ataona matokeo "hujawahi kuona katika historia yako".
Maneno haya yalitafsiriwa kama kuashiria tishio la kutumia silaha za nyuklia ikiwa mataifa ya Magharibi yataweka nia ya kuzuia nia yake.
Mabadiliko haya yaliyotangazwa hadharani ni njia ya Moscow kutuma onyo. Kuweka kikosi hicho kwenye hali ya juu ya tahadhari kunarahisisha kurusha silaha kwa haraka zaidi.
Lakini haimaanishi kuwa kuna nia ya sasa ya kuzitumia silaha hizo za maangamizi.
Urusi ndio taifa lenye akiba kubwa zaidi ya silaha za nyuklia ulimwenguni lakini pia inajua kuwa Nato pia inaakiba inayotosha kuiangamiza Urusi ikiwa zingetumiwa.
Lakini lengo ni uwezekano wa kujaribu kuzuia uungwaji mkono wa Nato kwa Ukraine kwa kuzua hofu juu ya ni kwa kiasi gani yuko tayari kwenda na kuleta sintofahamu juu ya aina gani ya uungwaji mkono kwa Ukraine atauchukulia kuwa mwingi.
Ukraine imesema nini?
Waziri wa mambo ya nje wa Ukraine Dmytro Kuleba amesema iwapo Urusi itatumia silaha za nyuklia dhidi ya Ukraine itakuwa "janga kwa dunia".
"Lakini haitatuvunja," alidai.
Kauli yake ilikuja baada ya Rais wa Urusi Vladimir Putin kuamuru jeshi la Urusi kuweka vikosi vyake vya nyuklia katika "tahadhari maalum" - kiwango cha juu zaidi cha tahadhari.
Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari, Kuleba alisema: "Agizo hili la Rais Putin lilikuja muda mfupi baada ya tangazo kutolewa kuhusu wajumbe wawili tayari kukutana [kwa mazungumzo].
"Tunaona tangazo hili au agizo hili kama jaribio la kuongeza vigingi na kuweka shinikizo la ziada kwa ujumbe wa Ukraine.
"Lakini hatutakubali shinikizo hili. Tutashughulikia mazungumzo haya kwa njia rahisi sana. Tunaenda huko kusikiliza [nini] Urusi inachosema na tutawaambia tunachofikiria juu ya haya yote."
Aliongeza: "Ukraine haianguki. Tunavuja damu, lakini tunaendelea kujilinda kwa mafanikio."
Marekani yakemea hatua ya Putin
Hakuna wakati ambapo Urusi imekuwa chini imepata tishio kutoka kwa Nato, anasema Katibu wa Habari wa Ikulu ya White House Jen Psaki, akijibu hatua Rais Putin kuweka vikosi vya nyuklia vya Urusi kwenye "tahadhari maalum".
Putin aliwalaumu viongozi wa Nato kwa kuruhusu "kauli za uchokozi" kutolewa dhidi ya Urusi. Lakini Psaki alisema ni jibu lililozoeleka kutoka kwa rais wa Urusi.
"Tumemwona akifanya hivyo mara kwa mara. Hakuna wakati ambapo Urusi imekuwa kwenye tishio kutoka kwa Nato, wala tishio kutoka Ukraine," aliiambia ABC News.
"Tuna uwezo wa kujitetea, lakini pia tunahitaji kutangaza kile tunachokiona hapa kutoka kwa Rais Putin," aliongeza.












