Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Mzozo wa Ukraine : Ujerumani yasitisha bomba huku nchi nyingi zikiiwekea Urusi vikwazo
Ujerumani imesimamisha bomba kuu la gesi la Urusi kufuatia agizo la Vladimir Putin la kutuma wanajeshi nchini Ukraine.
Siku ya Jumatatu rais wa Urusi alitambua mikoa miwili iliyojitenga ya Ukraine kama nchi huru na kuamuru wanajeshi wa Urusi kutumwa kwa nchi zote mbili.
Mataifa ya Magharibi kwa kiasi kikubwa yanaona hatua hiyo kama kisingizio cha uvamizi mpana.
Kwa kujibu, Ujerumani ilisitisha uidhinishaji wa bomba la Nord Stream 2 na mataifa mengine ya Magharibi yakatoa vikwazo.
Vikwazo vinaweza kuchukua aina mbalimbali - neno hilo linaweza kurejelea vitendo vingi vinavyotumiwa na nchi moja kudhuru nchi nyingine, kwa kawaida kuzuia vitendo vikali au ukiukaji wa sheria za kimataifa.
Bomba la Nord Stream 2 limeungwa mkono na Ujerumani licha ya upinzani kutoka kwa nchi kama vile Marekani, Uingereza, Poland na Ukraine. Iligharimu €10bn (£8.4bn), huku ufadhili ukigawanyika kati ya makampuni ya nishati ya Urusi na nchi za Magharibi.
Lakini kufuatia agizo la Bw Putin la kutuma wanajeshi katika mikoa ya Ukraine inayoshikiliwa na waasi ya Donetsk na Luhansk, Ujerumani ilitangaza kuwa inasitisha mchakato wa kutoa leseni ya bomba kati yake na Urusi na uendeshaji - na hivyo kusimamisha mradi huo .
Hatua hiyo ni kubwa kwani Urusi inaipatia Ulaya karibu 40% ya gesi yake, inayopatikana kutoka kwa usambazaji mkubwa mashariki mwa Urusi.
"Hii ni hatua ya kimaadili, kisiasa na kivitendo sahihi katika hali ya sasa," Waziri wa Mambo ya Nje wa Ukraine Dmytro Kuleba aliandika, akiukaribisha uamuzi huo. "Uongozi wa kweli unamaanisha maamuzi magumu katika nyakati ngumu. Hatua ya Ujerumani inathibitisha hilo."
Uchambuzi wa Jessica Parker
Wakati mawaziri na maafisa wa Ulaya wakichanganua kuhusu mipango ya vikwazo leo, kulitokea tangazo la ghafla kutoka Berlin.
Utata wa kimakusudi wa Olaf Scholz kuhusu mustakabali wa Nord Stream 2 ulimaanisha kuwa tangazo lake leo asubuhi liliwashangaza wengi. Hata hivyo, kuna maoni kwamba hatua hiyo ilichelewa sana.
Nakumbuka nikiwa chumbani na Waziri Mkuu wa Poland Mateusz Morawiecki mwezi Desemba, ambapo alisisitiza tena mradi huo ulikuwa "kosa kubwa." Bomba la gesi lilikuwa bado halijafanya kazi, bila shaka, na EU imekuwa ikitafuta vifaa mahali pengine.
Walakini, inazua maswali makubwa juu ya usalama wa nishati ya Uropa.
Kuhusu mipango ya vikwazo vya Umoja wa Ulaya dhidi ya Urusi, inaahidi kuwalenga wabunge wa Urusi, benki zinazofadhili jeshi la Urusi pamoja na uwezo wa serikali ya Urusi kufikia masoko ya fedha ya jumuiya hiyo. "Hatua za ziada" pia, tunaambiwa, zipo tayari kutumiwa ikiwa inahitajika.
Lakini kadiri hatua zinavyozidi kuwa ngumu, ndivyo wanavyoweza kupata ugumu kukubaliana kuzihusu .
Awamu hii ya vikwazo... itaumiza Urusi, na itaumiza sana," mkuu wa Sera ya Mambo ya Nje wa Umoja wa Ulaya Josep Borrell alisema.
Vikwazo vya Magharibi vilivyotangazwa Jumanne havilingani na kile kilichotishiwa katika tukio la uvamizi. Kulikuwa na uvumi kwamba Urusi ingeweza kukabiliwa na kukatwa kutoka kwa mfumo wa benki wa kimataifa, kunyimwa ufikiaji wa dola, au hata kukabili vikwazo vya kuagiza au kuuza nje.
Ikulu ya White House ilisema wazi kwamba vikwazo vyake vya awali "ni tofauti na vitakuwa pamoja na hatua za haraka na kali za kiuchumi" ilizotayarisha "ikiwa Urusi itaivamia zaidi Ukraine". Naye Waziri wa Ulinzi wa Uingereza Ben Wallace alisema kuna vikwazo vingi zaidi "katika tanki" vya kutumika ikiwa inahitajika.
Waziri Mkuu wa Poland Mateusz Morawiecki alikaribisha kuzuiwa kwa Nord Stream 2 - ambayo nchi yake imekuwa ikiipinga kwa muda mrefu - lakini akasema anatarajia mengi zaidi. Hapo awali alisema kwamba vikwazo lazima "viwe vya uchungu vya kutosha na kumzuia Vladimir Putin kuchukua hatua za ziada".
Rais wa Poland Andrzej Duda pia alitoa wito wa "vikwazo vikali".
Nchini Uingereza, kufuatia tangazo la Waziri Mkuu Boris Johnson la vikwazo vya awali, Mbunge wa ngazi ya juu wa Conservative Iain Duncan Smith alisema Urusi inahitaji kupigwa vikwazo "vigumu na sasa" - na kuuliza ikiwa Uingereza iko tayari kuchukua hatua zaidi.
Kujibu, waziri mkuu alisema: "Tunaipiga [Urusi] vikali sasa na tutaipiga zaidi katika siku zijazo."
"Tutaendelea kuiadhibu Urusi," Waziri Mkuu aliongeza.
Bado hakuna ushahidi wa wanajeshi wa Urusi kuvuka mpaka na kuingia katika maeneo yanayoshikiliwa na waasi mashariki mwa Ukraine, licha ya agizo la Bw Putin kufanya kazi anazoziita za kulinda amani.
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi Andrei Rudenko ameliambia shirika la habari la AFP kwamba Urusi haipeleki wanajeshi "kwa sasa".
"Hakuna anayepanga kupeleka chochote popote, ikitokea tishio tutatoa msaada kwa mujibu wa mikataba iliyoidhinishwa," alisema.