Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Waasi watangaza uhamasishaji wa kuingia vitani huku mapigano yakichacha
Maeneo yaliyojitenga ya mashariki ya Ukraine yanayoungwa mkono na Urusi yameamuru kuhamasishwa kwa jeshi huku kukiwa na ongezeko la mapigano makali .
Wanaume wenye umri wa kupigana katika jamhuri zilizojitangaza Donetsk na Luhansk wanawekwa kando kwa matayarisho ya vita .
Rais wa Marekani Joe Biden anasema ana imani kuwa Urusi itaivamia Ukraine, madai ambayo Moscow inakanusha.
Mataifa ya Magharibi yameishutumu Urusi kwa kujaribu kuandaa mgogoro ghushi katika maeneo ya mashariki kama kisingizio cha kuvamia.
Wachunguzi wa kimataifa wanaripoti "ongezeko kubwa" la mashambulizi kwenye mstari unaogawanya waasi na vikosi vya serikali.
Wanajeshi wawili wa Ukraine waliuawa na wanne kujeruhiwa kwa makombora siku ya Jumamosi, vifo vya kwanza kuripotiwa katika wiki kadhaa.
Waziri wa Ulinzi wa Bw Biden, Lloyd Austin, alisema vikosi vya Urusi vinaanza " kusogea karibu" na mpaka na Ukraine.
Katika mji wa Munich wa Ujerumani, Makamu wa Rais wa Marekani Kamala Harris aliuambia mkutano wa usalama kwamba ikiwa Urusi itavamia, Marekani na washirika wake wataweka "gharama kubwa ya kiuchumi" inayolenga taasisi zake za kifedha na viwanda muhimu, pamoja na wale waliosaidia uvamizi huo.
Biden asema ana imani Urusi ilishaamua kufanya Uvamizi
Rais wa Marekani Joe Biden amesema ana uhakika Rais wa Urusi Vladimir Putin ameamua kuivamia Ukraine, na kwamba shambulio linaweza kutokea katika "siku zijazo".
Bw Biden alisema tathmini hiyo ilitokana na ujasusi wa Marekani, ambao ulipendekeza mji mkuu wa Kyiv ungelengwa.
Urusi inakanusha kuwa inapanga kuivamia Ukraine .
Mataifa ya Magharibi yanaishutumu Urusi kwa kujaribu kuanzisha mgogoro ghushi katika maeneo yaliyojitenga ya mashariki mwa Ukraine ili kuipa sababu ya kuanzisha mashambulizi.
Marekani inakadiria kuwa kuna wanajeshi 169,000-190,000 wa Urusi waliokusanyika ndani na karibu na Ukraine, idadi ambayo inajumuisha wapiganaji wanaoungwa mkono na Urusi katika jamhuri zinazojiita za Donetsk na Luhansk mashariki mwa Ukraine.
Katika hotuba ya televisheni kutoka Ikulu ya White House, Rais Biden alisema Marekani ina "sababu ya kuamini" kwamba majeshi ya Urusi "yanapanga na kukusudia kushambulia Ukraine katika wiki ijayo, katika siku zijazo".
"Kufikia wakati huu nina uhakika kwamba amefanya uamuzi," aliongeza, akimaanisha Rais Putin. Hapo awali, rais na maafisa wake wakuu walisema hawakujua ikiwa ndivyo ilivyokuwa.
Lakini, alisema, Urusi inaweza "bado kuchagua diplomasia" na kwamba "haijachelewa sana kujiondoa na kurudi kwenye meza ya mazungumzo".
Mapema siku ya Ijumaa, katika ishara nyingine ya kuongezeka kwa mvutano, viongozi wa maeneo mawili yanayotenganisha walitangaza kuwahamisha wakaazi, wakisema Ukraine imezidisha mashambulizi ya makombora na inapanga kufanya mashambulizi.
Ukraine imesema mara kwa mara kuwa haipangi kufanya mashambulizi yoyote, na Waziri wa Mambo ya Nje Dmytro Kuleba alipuuzilia mbali kile alichokiita "ripoti za upotoshaji za Urusi".
Denis Pushilin, mkuu wa Jamhuri ya Watu wa Donetsk (DNR), alitangaza kuhamishwa kwa watu hao katika video inayodaiwa kurekodiwa siku ya Ijumaa. Walakini, uchambuzi wa BBC wa metadata ulionyesha kuwa ilirekodiwa siku mbili zilizopita, kabla ya kupamba moto kwa uhasama.
Ikulu ya Kremlin ilisema Rais Putin aliamuru kuwa kambi za wakimbizi zianzishwe karibu na mpaka na misaada ya "dharura" itolewe kwa watu wanaofika kutoka maeneo yaliyojitenga. Vyombo vya habari vya serikali ya Urusi viliripoti kwamba mabasi kadhaa yaliyokuwa yamewabeba wakaazi wa eneo hilo yalikuwa yakielekea Urusi.
Wizara ya mambo ya nje ya Marekani iliita tangazo la kuwahamisha watu kuwa ni hatua ya "hila" ya Moscow "kuvuruga ulimwengu kutokana na ukweli kwamba Urusi inajenga vikosi vyake katika kujiandaa kwa shambulio". Ikulu ya White House ilisema uhamishaji huo ni mfano wa Moscow kutumia habari potofu kama kisingizio cha vita.
Siku ya Ijumaa usiku, idara ya ujasusi ya kijeshi ya Ukraine ilisema kuwa imepokea taarifa kwamba vilipuzi vilitegwa katika vituo vya miundombinu huko Donetsk kwa ajili ya maandalizi ya kile kinachoitwa shambulio la uwongo - operesheni iliyofanywa kwa nia ya kumlaumu mpinzani kwa hilo.
Hapo awali, mamlaka zinazotaka kujitenga zilisema kuwa jgari iliyokuwa imeegeshwa ililipuliwa karibu na jengo la serikali huko Donetsk. Maafisa wa Marekani na Ukraine walisema lilikuwa ni shambulio lililopangwa ili kuzua hali ya wasiwasi.
Urusi imekuwa ikiunga mkono uasi wenye silaha katika eneo la Donbas mashariki mwa Ukraine tangu mwaka 2014. Takriban watu 14,000 - ikiwa ni pamoja na raia wengi - wamekufa katika mapigano.
Wakati huo huo Bw Putin alisema hali mashariki mwa Ukraine inazidi kuwa mbaya. Katika mkutano na waandishi wa habari, alitoa shutuma zisizo na uthibitisho wa "ukiukwaji mkubwa na wa utaratibu wa haki za binadamu" na kuweka katika sheria "ubaguzi wa idadi ya watu wanaozungumza Kirusi" nchini Ukraine.
Alisema bado yuko tayari kujadili mzozo huo na viongozi wa Magharibi, lakini aliwashutumu kwa kupuuza wasiwasi wa usalama wa Urusi, na akaonya kwamba mpango wowote lazima ujumuishe ahadi ya kisheria kwamba muungano wa usalama wa Nato utasimamisha upanuzi wake kuelekea upande wa mashariki.
Siku ya Jumamosi, Rais Putin anatarajiwa kusimamia mazoezi makubwa ya vikosi vya kimkakati vya makombora ya nyuklia ya Urusi.
Wakati huo huo Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky anatazamiwa kusafiri hadi Ujerumani kukutana na viongozi wa nchi za Magharibi katika mkutano wa usalama, huku mazungumzo kati yake na Makamu wa Rais wa Marekani Kamala Harris yakitarajiwa.