Mzozo wa Msumbiji: Rais Samia azuru Kaskazini mwa Msumbiji-eneo lenye wapiganaji wa kijihadi

Rais wa Tanzania Samia Sululu Hassan amezuru kaskazini mwa Msumbiji- ambako wanajeshi wake sehemu ya vikosi vya kikanda vinavyokabiliana na makundi ya kijihadi.

Mwenzake wa Msumbiji Filipe Nyusi alikuwa katika mkoa wa Cabo Delgado kumpokea.

Rais Samia alisema kwa vile yeye ni mgeni katika nafasi ya Urais wa nchi yake na katika kanda hiyo, alifika Msumbiji kwa ajili ya kusalimiana na Mkuu wa Nchi ya Msumbiji, pamoja na jifahamisha kuhusu matatizo yanayokumba maendeleo ya amani na usalama na jinsi nchi hizo mbili zinavyoweza kufanya kazi pamoja.

"Unapokuwa mgeni, unahitaji kuwatembelea majirani zako- kwa hivyo nimekuja kumsalimu ndugu yangu na pia kujadili amani na usalama na jinsi tunaweza kufanya kazi pamoja," alisema.

Mwishoni mwa mazungumzo hayo, Rais Nyusi aliangazia uhusiano baina ya nchi hizo mbili, ambao ulianza kipindi cha kabla ya uhuru wa Msumbiji, pamoja na nia ya haraka ya Tanzania kutaka kikosi chake kipatikane kupambana na ugaidi huko Cabo Delgado.

"Tuna uhusiano wa muda mrefu." alisema

Rais Nyusi alikubali ushirikiano ulikuwa muhimu, kutokana na wanajihadi kutotilia maanani mipaka: "Gaidi anavuka mipaka yetu - yuko hapa au pale, kwa hiyo sisi... tuna nia ya kujadili suala hili kwa kujitolea zaidi."

Aidha katika hotuba yake, Rais wa Msumbiji alisema kwamba majeshi ya Tanzania pamoja na majeshi ya Msumbiji yatachambua, katika siku zijazo, uboreshaji wa mikakati ya kupambana na ugaidi.

Katika taarifa iliyotolewa na Ikulu ya Tanzania, Rais Nyusi aliishukuru nchi hiyo kwa mchango wake katika kulinda amani kaskazini mwa Msumbiji kupitia wanajeshi wake walio katika jeshi la Pamoja la SADC katika Jimbo la Cabo Delgado.''

Hii ndio kauli ya kwanza kutoka kwa kiongozi wa juu wa nchi kuthibitisha hilo.

Taarifa hiyo pia imeelezea kwamba Tanzania itaendelea kukuza ushirikiano kati yake na Msumbiji kutokana na uhusiano ambao umekuwepo kwa muda mrefu.

Hivi karibuni vikosi vya jeshi la Msumbiji kutangaza kuwa vimemkamata kiongozi wa kijihadi, raia wa Tanzania, katika wilaya ya Nangade kaskazini mwa jimbo la Cabo Delgado.

Kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 39, anayejulikana kama Ali, alikamatwa pamoja na wanamgambo wengine wa Kiislamu sita wenye uhusiano na kundi la Islamic State, maafisa wa kijeshi wameeleza.

Kukamatwa kwake kunajiri huku kukiwa na hali mbaya ya usalama katika wilaya hiyo, na mfululizo wa mashambulizi ya wanajihadi katika siku za hivi karibuni.

Nchi za Jumuiya ya maendeleo ya Kusini mwa Afrika pia zilipeleka wanajeshi kaskazini mwa Msumbiji mwezi Agosti kusaidia vikosi vya nchi hiyo ambavyo vimekuwa vikikabiliwa na wakati mgumu kudhibiti wavamizi hao.

Zaidi ya watu 800,000 wametoroka makwao kufuatia mzozo ambao umelikumba taifa hilo la Afrika lenye hifadhi kubwa ya gesi

Pia unaweza Kusoma: