Netflix: Filamu ya kwanza ya Kiarabu yazua mzozo wa kimaadili

Filamu ya kwanza ya lugha ya Kiarabu iliyoonyeshwa kwenye Netflix imezua mjadala mkali nchini Misri kuhusu madai ya ukosefu wa maadili na kudhoofisha maadili ya kitamaduni.

Filamu hiyo inahusisha mijadala ya ngono na mahusiano ya nje ya ndoa na inaonyesha wahusika wakinywa pombe.

Filamu hiyo iliyorekodiwa Lebanon ni marudio ya filamu ya Kiitaliano ya mwaka 2016 kwa jina Perfect Strangers.

Waigizaji wa Misri na wakosoaji wa filamu pia wameonyesha kuunga mkono filamu hiyo.

Maudhui ya filamu hiyo, iliyouzwa na Netflix kama Perfect Strangers na ambayo jina la Kiarabu linatafsiriwa kama Marafiki Wapendwa Zaidi, inahusu marafiki saba wanaokutana kwa chakula cha jioni. Wanaamua kucheza mchezo ambao kila mtu anaweka simu yake ya mkononi kwenye meza, na kuruhusu ujumbe au simu yoyote mpya kusomwa au kupokelewa na kila mtu.

Mbunge na mwandishi maarufu wa Televisheni Mustafa Bakry alisema kuwa aliwasilisha malalmishi yake kwa spika wa Bunge la Misri kuhusu waandaaji filamu hao. Bw. Bakry alitoa wito kwa mamlaka nchini kusitisha ushirikiano na Netflix "kwani hii si filamu yake ya kwanza inayolenga maadili na mila za jamii za Misri na Kiarabu".

Wakili wa Misri Ayman Mahfouz alisema aliwasilisha kesi mahakamani dhidi ya watengenezaji filamu akiwatuhumu "kuendeleza mapenzi ya jinsia moja", tovuti ya Al-Watan inaripoti. Lawama hizo pengine zinatokana na kujumuishwa kwa mhusika ambaye anashiriki mahusiano ya jinsia moja kwenye filamu.

Bw Mahfouz alisema pia ametuma onyo la kisheria kwa wizara ya utamaduni ili kuzuia filamu hiyo isioneshwe nchini Misri, kulingana na tovuti ya Cairo 24.

Akijibu wito wa kutaka filamu hiyo kupigwa marufuku nchini Misri, Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Kazi za Kisanaa alisema nchi hiyo haiwezi kupiga marufuku filamu hiyo kwa sababu ni ya Kilebanon, tovuti ya Darb inayounga mkono upinzani inaripoti.

'Haki ya kutotazama'

Waigizaji wengi mashuhuri na wakosoaji wameitetea vikali filamu hiyo, na wamekataa shutuma dhidi ya watengenezaji wake wa filamu.

Wakati wa mazungumzo ya simu kwenye kipindi cha mazungumzo cha Al Hikaya, mkosoaji wa sanaa Magda Moris alisema Marafiki Wapendwa "hawakuhimiza mapenzi ya jinsia moja au kukiuka maadili ya familia".

"Hatuwezi kupiga marufuku filamu hii nchini Misri na wale wanaopinga wana haki ya kutotazama,"aliongeza kusema.

Tuvuti ya Ahl Masr inaripoti kuwa muigizaji mkongwe wa kike Elham Shahin alipinga jaribio la kupeleka bunge suala hilo.

"Bunge halihusiani na Netflix na wabunge sio walezi wa umma," alisema. "Kuna filamu za ujasiri zaidi kwenye Netflix."

Kampeni ya chuki

Mmoja wa mastaa wa kike wa filamu hiyo, Mona Zaki, amekuwa mlengwa wa kampeni mbaya mtandaoni kuhusu tukio ambalo anavua nguo zake za ndani.

Hashtag Kiarabu iliyo na majina ya muigizaji huyo na filamu husika ilikuwa miongoni mwa mada zilizojadiliwa sana nchini Misri , ikiwa na zaidi ya ujumbe 17,000.

Watumiaji wengi walimshutumu kwa "kukiuka maadili ya jamii", kama mmoja alivyoiita. Mtumiaji mwingine alitweet kwamba filamu hiyo ilikuwa "kutoweka kwa maadili" ndani ya wigo wake wa kazi.

Mamlaka ya wasanii ilitoa taarifa ikisisitiza kwamba "itamuunga mkono mwigizaji huyo ikiwa mtu yeyote atajaribu kuchukua hatua za aina yoyote dhidi yake", tovuti ya Darb inaripoti.

"Mamlaka hii haitakaa kimya kuhusu jaribio lolote la kuwanyanyansa wasani wa Misri kutotokana na kazi zao," taarifa hiyo ilisema.

Mwigizaji wa Misri Elham Shahin pia alimtetea Bi Zaki, akimtaja kama "msanii aliyekomaa, mwaminifu na mwenye uigizaji [ujuzi] mzuri", Darb pia anaripoti.

Vile vile, mchambuzi mashuhuri wa filamu Tariq al-Shennawi aliambia kituo cha Televisheni cha ETC TV nchini Misri kwamba "eneo hilo halistahili mabishano yote haya yanayolizunguka, na hatukuona chochote ambacho kinaashiria unyonge au kuchochea hasira na hakuna sehemu ya mwili wake inayoonekana [ bila nguo kwenye filamu]".

Pia unaweza kutazama: