Zijue siasa nyuma ya ziara ya Muhoozi Kainerugaba nchini Rwanda

    • Author, Ezekiel Kamwaga
    • Nafasi, Mchambuzi

Askari huyo, Ronald Arinda (23), alikamatwa na maofisa usalama wa Rwanda Novemba mwaka jana katika mazingira ya kutatanisha - viongozi wa mkoa wa mpakani wa Kabale nchini Uganda wakidai alitekwa akiwa hajavuka mpaka; ingawa taarifa rasmi ya Muhoozi aliyoitoa kupitia mtandao wa kijamii wa twitter ilieleza kwamba aliingia Rwanda kwa shughuli zake binafsi. Arinda ni askari wa kikosi cha makomandoo (SFC) wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Uganda (UPDF).

Hata hivyo, kwa wafuatiliaji wa siasa za Afrika Mashariki na eneo la Maziwa Makuu kwa ujumla, ziara ya Muhoozi ina tafsiri nyingi kuliko kitendo cha kurejea na mwanajeshi mmoja baada ya kutoa ombi maalumu kwa Rais Kagame. Kuna mambo mengi ya kuyatazama katika mkutano huu kwa mipango ya mfupi, wa kati na ujao.

Kuna nini kati ya Uganda na Rwanda?

Rwanda na Uganda zimekuwa na uhusiano unaoyumbayumba tangu mwaka 2017, kutokana na hatua ya serikali ya Uganda kuwakamata raia kadhaa wa Rwanda wanaoishi nchini humo kwa madai ya kujihusisha na vitendo vya hujuma na ujasusi dhidi yake. Mzozo huo ulisababisha kufungwa kwa mpaka wa Gatuna/Katuna unaounganisha nchi hizo mbili.

Huu si mgogoro wa kwanza baina ya Uganda na Rwanda. Hizi ni nchi ambazo zimekuwa na uhusiano usiotabirika katika kipindi cha miaka 30 iliyopita. Mwishoni mwa miaka ya 1990, nchi hizi mbili ziliwahi kupigana vita ndani ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) - kutokana na kile kinachoelezwa kama kuwania utajiri wa mali asilia za taifa hilo tajiri kwa mali asilia zaidi katika ukanda huo.

Mgogoro huo ulishangaza wengi kwa sababu majeshi ya nchi hizo mbili yalishirikiana kwa karibu wakati wa mapambano ya kijeshi yaliyomuondoa madaraka Mobutu Sesseseko na kumwingiza Laurent Desire Kabila. Ugomvi ulianza baada ya Kabila kuingia madarakani na mataifa hayo mawili yakijikuta yana ushawishi mkubwa katika kuendesha siasa na uchumi wa DRC.

Katika kitabu cha Do not Disturb kilichoandikwa na mwandishi Michela Wrong, aliyekuwa Mkuu wa Ujasusi wa Jeshi la Rwanda, Patrick Karegeya, anaeleza ilivyokuwa vigumu kwa watu waliokuwa wakifahamiana kwa muda mrefu kuanza kushambuliana kama maadui kwenye uwanja wa vita ndani ya DRC.

Karegeya - aliyeuawa nchini Afrika Kusini miaka michache iliyopita, alizaliwa, kusoma na kufanya kazi katika vyombo vya ulinzi na usalama vya Uganda - kama ilivyokuwa kwa Kagame aliyekuwa Mkuu wa Ujasusi ndani ya Jeshi la Uganda mara baada ya Jeshi la NRA lililoongozwa na Museveni kuingia madarakani mwaka 1986 baada ya vita ya msituni viliyouondoa madarakani utawala wa Jenerali Tito Okello Lutwa.

Jambo ambalo limekuwa likijirudia mara kwa mara ni uwezo wa Rwanda na Uganda kugombana na kupatana kila mara. Kama kuna marais wawili wa Afrika wanaofahamiana pengine kuliko wengine ni Museveni na Kagame. Kama kuna marais ambao inaonekana hawaaminiana kuliko wengine pengine ni Museveni na Kagame.

Kupitia mtandao wa twitter, Muhoozi aliandika: "Uganda na Rwanda ni kitu kimoja". Ujumbe huo uliendana na maneno kwamba yeye binafsi (Kainerugaba) kuna nyakati aliwahi kuitwa Mnyarwanda na baadhi ya watu. Alimaliza andiko lake hilo kwa kueleza imani yake kwamba maraisi wawili wa nchi hizo watamaliza hali ya sasa ya kutokuamiamina.

Kwanini Muhoozi?

Hatua ya Museveni kumtuma mwanaye mkubwa kwenda kukutana na kiongozi wa serikali ya nchi nyingine imezua mjadala nchini Uganda. Mtoto huyo wa Rais ni Kamanda wa vikosi vya ardhini vya jeshi la Uganda-na kwa hiyo ni mmoja wa maofisa wa ngazi za juu wa taasisi hiyo yenye mamlaka na ushawishi mkubwa ndani ya taifa hilo.

Hata hivyo, kama safari hiyo ingekuwa ya kijeshi - Rais Museveni angeweza kumtuma Mkuu wa Jeshi la Uganda kwenda kukutana na Rais Kagame au Mkuu wa Majeshi ya Rwanda. Kama ziara hiyo ingekuwa ya kiserikali, angeweza kwenda Rais mwenyewe au kumtuma mmoja wa mawaziri wake waandamizi. Hata hivyo, katika mazingira ya sasa ya kutokuaminiana kimahusiano baina ya nchi hizo mbili, inaonekana kwamba alitakiwa kutumwa mtu ambaye si rasmi kiserikali wala kijeshi lakini ana mamlaka.

Hapo sasa ndipo anapoingia Luteni Jenerali Muhoozi Kainerugaba.

Huyu si askari au kamanda wa kawaida wa UPDF. Huyu ni mtu ambaye Kagame anamfahamu akiwa amemwona tangu angali mdogo. Kimsingi, katika enzi zake ndani ya UPDF, Kagame alikuwa na kazi maalumu ya kulinda usalama wa familia ya Rais. Ni wazi kwamba Rais huyu wa Rwanda kwa sababu zilizo wazi anamuona Muhoozi kama mwanawe wa kumzaa.

Ni jambo la kawaida pia kumuona Muhoozi akichapisha picha za Rais Kagame na hayati Emmanuel Gisa (Fred Rwigyema) - Kamanda wa zamani wa UPDF na mmoja wa waanzilishi wa Jeshi la RPF, na kuwataja kama miongoni mwa watu waliofanya atamani siku moja aje kuwa askari kama wawili hao - wengine katika orodha yake huwa ni baba yake, Museveni, na Caleb Akandwanaho (Jenerali Salim Saleh) ambaye pia ni baba yake mdogo (mdogo wa Museveni).

Kwa hiyo, katika mazingira ambayo Rwanda na Uganda bado hazijarejesha rasmi uhusiano wa kawaida - Muhoozi ana sifa kubwa mbili; mosi kwamba anamwakilisha Amiri Jeshi Mkuu na pia anazungumza kwa niaba ya baba. Inawezekana pia, kwamba Museveni amepeleka ujumbe kwa Kagame ambao hamwamini mtu mwingine yeyote kuufikisha zaidi ya mwanaye.

Muhoozi 'Project'?

Mwaka 2013, aliyekuwa Mratibu wa Usalama wa Taifa wa Uganda, Jenerali David Sejusa (Tinyefuza), aliandika barua katika gazeti binafsi la Daily Monitor akidai kuwepo kwa kile alichokiita Muhoozi Project. Aliueleza mpango huo kuwa ni mkakati wa kuhakikisha Muhoozi anakuwa Rais wa Uganda baada ya baba yake kuondoka madarakani. Katika barua yake hiyo, Sejusa alidai maisha ya watu kama yeye na aliyekuwa Waziri Mkuu, Stephen Amama Mbabazi, yalikuwa hatarini kwa sababu wapishi wa mpango huo wako tayari kuondoa 'vikwazo' vyovyote vinavyoweza kujitokeza.

Ziara hii ya siku moja ya Muhoozi imeibua upya hoja hiyo. Kuna sababu chache za kueleza hili. Kwanza, Muhoozi amekutana na Mkuu wa Serikali wa Taifa lingine katika tukio lililopangwa vizuri kiasi kwamba mamilioni ya Waganda wameona. Pili Muhoozi alisafiri na ndege rasmi ya serikali, alipokewa kwenye uwanja wa ndege wa Kigali na Naibu Balozi wa Uganda nchini Rwanda na alikutana na Kagame katika ofisi rasmi ya Rais.

Na kuna lingine ambalo ni mahsusi kwa Uganda. Tangu kupinduliwa kwa Milton Obote mwaka 1972, marais wa Uganda waliokaa madarakani walau kwa muda mrefu ni wanajeshi - Idi Amin na Museveni. Kuna utamaduni unaanza kujengeka Uganda kwamba ili mtu awe kiongozi ni lazima awe na walau sifa mojawapo kati ya mbili; awe mwanajeshi au apendwe na wanajeshi.

Katika mkutano wake na Kagame, Muhoozi ambaye tayari ni mwanajeshi na anakidhi sifa hiyo ya kwanza, amefanya jambo moja tu la wazi - amerejea nyumbani na askari wake aliyeshikwa mateka. Kwa wanajeshi, hakuna kamanda mwenye maana kuliko yule anayehakikisha askari wake waliokwenda uwanja wa mapambano wanarudi wakiwa salama.

Muhoozi mwenyewe atasema kilichofanyika ni kitu cha kawaida na alimwomba tu Rais Kagame amwachie askari mwenzake, lakini ukweli ni kwamba kitendo cha kurejea na askari aliyetekwa kinamweka katika sura ya kipekee ndani ya UPDF.

Nini kitafuata?

Kitendo cha DRC kuruhusiwa kujiunga na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), kinamaanisha kwamba Rwanda na Uganda hazitakuwa na sababu tena ya kupigana ndani ya taifa hilo kuwania chochote. Ni wazi zitataka kutumia hili kuona zitanufaikaje na fursa mbalimbali zilizopo.

Kagame tayari amekutana mara kadhaa na Rais Felix Tshisekedi wa DRC kuzungumzia masuala ya uhusiano wa kibiashara na kiuchumi. Uganda tayari imeingia makubaliano kadhaa na DRC kuhusu ujenzi wa miundombonu itakayotumika kuunganisha nchi hizo mbili.

Wawili hao pia ni miongoni mwa viongozi wachache wa Afrika ambao angalau bado wana ushawishi katika jumuiya ya kimataifa wanakoshiriki katika masuala kadhaa ya kiulinzi, kiusalama, kibiashara na kiuchumi. Migogoro baina yao ina athari kubwa katika duru za kimataifa.

Museveni na Kagame pia wanaanza kuona ukweli kwamba muda si mrefu wataanza kuachia madaraka kwa kizazi kipya cha viongozi wa nchi zao; kwa kupenda au pengine kwa kung'amua na kuzingatia hali halisia, wanaweza kuwa wameanza kupanga maisha baada ya muda wao madarakani.

Mustakabali wa Rwanda, Uganda na DRC katika miaka mingi ijayo hautakuwa tena mikononi mwa akina Museveni na Kagame. Ukweli huu pengine unaweza kuwaweka mezani miamba hawa na kuzirejesha nchi hizi kwenye uhusiano wa zamani.

Na kama hilo litatokea katika siku za karibuni, kuna mtu mmoja jina lake litatajwa tena na tena, nalo ni Luteni Jenerali Muhoozi Kainerugaba. MKUTANO baina ya Rais Paul Kagame wa Rwanda na mtoto mkubwa wa Rais Yoweri Museveni, Luteni Jenerali Muhoozi Kainerugaba, umemalizika Jumamosi Januari 22, 2022 na tayari matunda ya kwanza ya mkutano huo yameonekana - kitendo cha kuachiwa mwanajeshi aliyekamatwa kwa madai ya kufanya ujasusi.