Je 5G ni tishio kwa safari za ndege kwa kiasi gani?

A woman using her phone at an airport

Chanzo cha picha, Getty Images

Mashirika 10 mashuhuri ya ndege nchini Marekani yanaonya kuwa uzinduzi wa huduma za 5G unaweza kuwa hatari.

Yanasema teknolojia hiyo mpya inaweza kufanya maelfu ya safari za ndege kucheleweshwa na huenda sehemu kubwa ya ndege za Marekani kukwama kwa muda usiojulikana.

Je, 5G inawezaje kutatiza usafiri wa anga wa Marekani?

5G inategemea ishara za redio. Nchini Marekani, masafa ya redio yanayotumika kwa 5G ni sehemu ya masafa yanayojulikana kama C-Band.

Masafa haya yanakaribiana na yale yanayotumiwa na vidhibiti vya redio kwenye ndege, ambavyo hupima urefu wa ndege juu ya ardhi, lakini pia hutoa data kwa usalama na mifumo ya kuongoza ndege.

Wasiwasi kwamba huduma ya C-Band na 5G inaweza kuingiliana na vifaa vya kielektroniki vya ndege na kuvuruga utendakazi wa vifaa hivyo hasa wakati ndege inapolekea kutua.

Tishio hili ni hatari kiasi gani kwa ndege?

Ni hatari sana.

Mwishoni mwa 2020, RTCA - shirika la Marekani ambalo hutoa mwongozo wa kiufundi kuhusu masuala ya anga - ilichapisha ripoti kuhusu mada hiyo.

Ramani

Ilisema kuna "uwezo wa athari kubwa kwa shughuli za anga nchini Marekani, pamoja na uwezekano wa kutokea kwa janga na kusababisha vifo vingi, endapo hakutakuwa na mikakati inayofaa ya kudhibiti hatari hiyo".

Hivi majuzi, mamlaka ya kudhibiti wa usafiri wa anga nchini Marekani, FAA, ilionya kuwa muingilio wa 5G unaweza kuathiri mifumo kadhaa ndege ya Boeing 787 Dreamliner.

Hii inaweza kufanya iwe vigumu kupunguza kasi ya ndege inapotua, na kuifanya iondoke kwenye njia ya kurukia.

Usafiri wa ndege utafanywa vipi kuwa salama?

Ndege hazitaruhusiwa kutumia vidhibiti vya redio ili kuzuia muingiliano wa masafa hayo.

Lakini hatuoa hiyo huenda ikafanya baadhi ya ndege kushindwa kutua, kwa mfano kukiwa na hali mbaya ya hewa.

Mashirika ya ndege ya Marekani, ambayo yanawakilisha mashirika 10 ya ndege, yameonya kwamba hii inaweza kusababisha safari zaidi ya 1,000 kucheleweshwa au kuahirishwa hali ya hewa ikiwa mbaya, kumaanisha wakati mwingine "idadi kubwa ya watu wanaosafiri watavurugiwa mipango yao".

Pia imeonya kuwa sehemu kubwa ya mifumo ndege za Marekani "hazitatumika" kutokana na muundo wa uendeshaji wa mifumo hiyo.

A number of aeroplanes lined up in an airport

Chanzo cha picha, Getty Images

Je nchi zingine zinazotumia 5G piazina hofu?

Sio kwa kiwango sawa na Marekani. Hii ni kwa sababu ya jinsi huduma za 5G zinavyozinduliwa kutoka nchi moja hadi nyingine.

Katika Muungano wa EU, kwa mfano, mitandao hufanya kazi kwa masafa ya chini kuliko yale ambayo watoa huduma wa Marekani wanapanga kutumia - kupunguza hatari ya muingiliano wa masafa. Milingoti ya 5G pia inaweza kufanya kazi kwa nguvu ndogo.

Hata hivyo, baadhi ya nchi zimechukua hatua madhubuti ili kupunguza hatari zinazoweza kutokea.

Nchini Ufaransa, kuna eneo linalojulikana kama "buffer zone" karibu na viwanja vya ndege ambapo mawimbi ya 5G yamedhibitiwa, huku antena zikipaswa kuinamishwa chini ili kuzuia mwingiliano wa mawimbi.

Mamlaka za Marekani zinachukua hatua gani?

Wadhibiti nchini Marekani tayari wamechukua hatua kadhaa.

FAA imeanzisha maeneo ya hifadhi ya muda karibu na viwanja vya ndege 50, ambapo watoa huduma za 5G watapunguza shughuli zao. Lakini hatua hiyo ni ndogo sana ukilinganisha na Ufaransa, kwani wasambazaji huduma wa Marekani watafanya kazi kwa viwango vya juu zaidi.

Pia imeanza kubainisha ni vidhibiti gani vinaweza kutumika kwa usalama katika maeneo ambayo yanatoa huduma ya 5G - ambayo si ya kuaminika na itahitaji kubadilishwa.

Pia imetambua viwanja vya ndege ambapo mifumo ya GPS inaweza kutumika kuongoza ndege zinazoelekea kutua badala ya vidhibiti vya redio.

Lakini mashirika ya ndege yanasisitiza kuwa hii haitoshi: wanadai mtandao wa 5G haufai kuwekwa hata kidogo ndani ya maili mbili ya viwanja vya ndege vilivyoathirika.

Je! makampuni ya 5G yamesema nini?

Verizon na AT&T tayari yameahirishamara mbili uzinduzi wa mtandoa wa 5G, na wamekubali hatua ya kutengwa kwa eno salama ya kudhibiti mawimbi ya 5G

AT&T and Verizon store fronts and entrances at a mall in northern Idaho.

Chanzo cha picha, Getty Images

Pia walisema kwamba 5G tayari imezinduliwa katika nchi 40.

Mwezi uliopita shirika la mwasiliano la Marekani CTIA lilishutumu mashirika usafiri wa anga kwa "kueneza hofu", na kuonya kuwa kuchelewesha kuanzishwa kwa 5G kunaweza kusababisha madhara ya kiuchumi.