Ushelisheli: Taifa la kisiwa linalowinda dola milioni 50 zilizotoweka

Chanzo cha picha, Getty Images
Raia sita mashuhuri wa Ushelisheli akiwemo mke wa Rais wa zamani wanakabiliwa na mashtaka katika kashfa ya ufisadi inayohusisha dola milioni 50 za msaada wa kigeni zinazokosekana, jambo ambalo limewafurahisha baadhi ya wakazi wa visiwa hivyo lakini kuwa hatari kwa wengine, kama Patrick Muirhead anaripoti.
Derrick Labrosse, mvuvi mwenye umri wa miaka 25, anatengeneza mitego kabla ya kuiweka kwa uangalifu katika mashua yake ndogo ya kwenye eneo la kustarehe la ufuo wa Anse à la Mouche.
Vidole vyake hufanya kazi kwa ustadi kwa miundo ya mianzi inayojulikana kama kazye. Alijifunza mbinu hii ya kitamaduni ya uvuvi kutoka kwa baba na babu yake ambao walileta chakula cha jioni cha familia kwenye meza mbele yake na ambayo leo hii huleta kipato cha kutosha kulisha mpenzi wake na binti yao wa miaka sita.
Lakini asubuhi ya leo, Bw Labrosse, kama Washelisheli wengi, anatafakari jinsi angeweza kufaidika na pesa zilizotoweka.
"Pesa hizo, dola milioni 50 ilikuwa zawadi kwa Washelisheli na hatukupata," anasema, huku macho yake meusi yakionyesha uchungu.
Ni pesa nyingi ambazo karibu hakuna hata mmoja wa watu 100,000 wanaoishi sehemu hizi maarufu kwa utalii magharibi mwa Bahari ya Hindi, anayeweza kufikiria kulipwa maishani au hata kuiba.
Lakini yadaiwa ziliibwa.
Msaada uliotoweka
Pesa hizo zilikuwa zawadi kwa jamhuri hiyo ndogo miaka 20 iliyopita kutoka Umoja wa Falme za Kiarabu, zilizokusudiwa kusaidia visiwa hivyo vinavyokabiliwa na uhaba wa fedha za kigeni na kulipia mahitaji ya msingi kama mchele, unga na mafuta ya kupikia.
Mchango haujawahi kufika. Badala yake, kulingana na nyaraka za mashtaka katika Mahakama ya Juu, uliibwa na mshirika wa karibu wa Rais wa zamani Albert René, ukaporwa kwa usaidizi kutoka kwa wengine kupitia ubinafsishaji usio na thamani wa mali ya umma, na kutawanywa kwenye akaunti za benki kote ulimwenguni.
Washtakiwa sita hawajazungumza rasmi kuhusu mashtaka hayo.

Washtakiwa sita
Mukesh Valabhji, mfanyabiashara na mshauri wa zamani wa uchumi wa Rais René
Laura Valabhji, mke wake ambaye ni mwanasheria
Leslie Benoiton, kanali wa zamani katika jeshi, mtoto wa René
Lekha Nair, afisa wa zamani wa serikali katika wizara ya fedha
Maurice Loustau-Lalanne, waziri wa zamani wa fedha na waziri wa utalii
Sarah René, mama wa taifa wa zamani, mjane wa René

Mvuvi huyu, kama watu wengine wengi hapa, ana matumaini kwamba fedha hizi zitarejeshwa.
Anaweka imani yake katika serikali mpya ya Rais Wavel Ramkalawan, ambaye chama chake cha Linyon Demokratik Seselwa kilishinda mamlaka katika uchaguzi miezi 14 iliyopita, akiahidi kukomesha ufisadi ambao ulikumba utawala wa miaka 43 wa chama cha René.
Rais Ramkalawan, kasisi wa Kianglikana, alikuwa sehemu ya upinzani wa chinichini hapo mwanzo Alitumia miaka 30 kupambana na ukandamizaji wa serikali ya chama kimoja chini ya René na mrithi wake, James Michel. Hatimaye aliufagia utawala uliopita, ulioongozwa na Danny Faure katika uchaguzi wa Oktoba 2020.
Janga la Covid lilimkaribisha Bw Ramkalawan katika Ikulu, na kuathiri kwa haraka uchumi wa visiwa hivyo unaotegemea utalii.

Chanzo cha picha, Getty Images
Kupatikana kwa shehena kubwa ya silaha za kijeshi katika nyumba za washukiwa wawili kumechochea kashfa hiyo.
Inakisiwa kuwa baadhi ya pesa zinazokosekana bado ziko kwenye akaunti za benki na zimekuwa zikipata riba katika kipindi cha miaka 20 iliyopita.
"Tunatumai milioni hizo 50 hadi sasa zitakuwa zimezalisha mamia ya milioni na tunatarajia kupata kila kitu," anasema.
"Utawala huu hauna uvumilivu kabisa kwa rushwa na tutajaribu kurudisha kila senti kwenye hazina ya serikali kwa sababu pesa hizo zilikuwa za watu wa Ushelisheli na uhalifu huu hautasamehewa."
Mkutano wa eneo la siri
Jukumu la kutafuta mamilioni ya pesa zilizotoweka na wale walioiba ni la May de Silva, Kamishna wa tume ya kupambana na rushwa nchini humo. Mshauri wa usimamizi, aliyerudi nchini mwake baada ya elimu na kazi nchi za ng'ambo, anakutana nami eneo la siri, chumba cha ofisi zisizo na vifaa katika mji mkuu, Victoria.
"Lazima nifahamu sana hatari zilizopo. Serikali imeweka mipango ya kulinda usalama wangu binafsi," anasema.
"Maamuzi tunayofanya yanaathiri watu katika nyadhifa za juu. Wana msimamo mkali sana, wana mtandao mzuri, sio tu nchini Ushelisheli lakini pia nje ya nchi."
Ana kesi 55 za ufisadi za kushughulikia ikijumuisha ya kukosekana dola milioni 50. Lakini, kwa usaidizi kutoka kwa wachunguzi wa Uingereza na Umoja wa Ulaya, amedhamiria kurudisha pesa hizo nyumbani.
"Ukiweka pesa zako benki tutazipata," anasisitiza, "na ikiwa haukuweka pesa benki itabidi ueleze pesa za kununua nyumba na magari yako zilitoka wapi. Tumetoka mbali sana katika suala la habari za kidijitali - tutafikia."

"Pia tunahitaji kutuma ujumbe mzito kwa bara la Afrika kwamba tunahitaji kusafisha vitendo hivi," Rais Ramkalawan anasema.
"Licha ya sisi kuwa wadogo, tunaongoza kwa mfano. Tunatumahi hii itaenea katika sehemu zingine za Afrika na rasilimali za bara letu kuu zitatumika vizuri," anaongeza kwa kujigamba.
Bw Labrosse, mvuvi, ana matumaini makubwa kwa mamilioni yaliyopotea. Kwake, ni wakati wa kulipwa.
"Fedha zitakazopatikana zinaweza kutumika kujenga barabara bora na nyumba zaidi. Tunaweza kujenga hospitali mpya na shule," anasema kabla ya kuondoka na mitego yake, "na labda wanaweza kutoa bonasi kidogo kwa kila mtu. "












