Chanjo ya Covid 19: Mataifa ya Afrika yashindwa kufikia lengo la WHO

    • Author, Peter Mwai
    • Nafasi, BBC Reality Check

Lengo la kufikia 40% ya viwango vya chanjo kamilifu katika kila nchi hadi kufikia mwisho wa mwezi Disemba halijafanikiwa barani Afrika.

Shirika la Afya Duniani (WHO) liliweka lengo hilo mapema mwaka huu, lakini ni takribani asilimia 9 tu ya watu barani Afrika wamepatiwa chanjo kamili hadi sasa.

Ni nchi gani za Afrika zimefikia lengo?

Ni nchi saba pekee barani zimefikia lengo la 40%.

Tatu kati ya hizi ni mataifa ya visiwa vidogo ambapo changamoto za vifaa ni rahisi kukabiliana nazo. Seychelles na Mauritius zimechanja kikamilifu zaidi ya 70% ya wakazi wake huku Cape Verde ikichanja karibu 45%.

Katika nchi za bara ni Morocco, Tunisia, Botswana na Rwanda pekee ndizo zimevuka lengo hilo.

Nchi za kusini mwa bara zinafanya vizuri zaidi kuliko maeneo mengine ya kusini mwa jangwa la Sahara

Mpaka kufikia Disemba 30, nchi chini ya nusu katika bara hilo zilikuwa zimepata chanjo kamili kwa zaidi ya 10% ya watu wote (lengo ambalo WHO iliweka kufikia mwishoni mwa Septemba, na ambalo halijafikiwa na mataifa mengi ya Afrika).

Nchi nyingi, ikiwa ni pamoja na baadhi ya nchi kubwa zaidi barani, hadi sasa zimechanja chini ya 5% ya idadi ya watu wao.

  • Nigeria imechanja asilimia 2.1
  • Ethiopia 3.5%
  • Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo 0.1%.
  • Nchi pekee katika bara ambayo haijaanza mpango wa chanjo ni Eritrea.

WHO imeweka lengo zaidi ya kufikia asilimia 70 kwa nchi zote ifikapo Juni 2022, lakini hii pia inaweza ikashindikana barani Afrika. "Kwa jinsi mambo yanavyoendelea, utabiri ni kwamba Afrika inaweza isifikie lengo la chanjo ya asilimia 70 mpaka itakapofika Agosti 2024," anasema mkurugenzi wa WHO kanda ya Afrika Matshidiso Moeti.

Kwa nini nchi za Kiafrika zinachangamoto ya chanjo?

Miundombinu duni ya afya, ukosefu wa pesa kwa ajili ya mafunzo na kupeleka wahudumu wa afya, pamoja na maswala ya kuhifadhi chanjo yote yamechangia.

Hili limekuwa suala kubwa kwa sababu ingawa usambazaji wa kimataifa umeboreka, ugawaji na usimamizi wa chanjo katika baadhi ya maeneo ya dunia uko nyuma.

WHO na kituo cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa Afrika (CDC) wameelezea wasiwasi kwamba baadhi ya chanjo zilizotolewa kwa misaada zimefika zikiwa na ufinyu wa taarifa na muda mchache wa kuhifadhi.

Wanataka chanjo zikae kwenye makabati chini ya miezi miwili na nusu baada ya kuwasili na kwa nchi kufahamishwa mwezi mmoja kabla chanjo hazijafikia.

Pia kuna hofu kwamba kusitasita kwa chanjo na kutilia shaka pia inaweza kuwa ni sababu ingawa ni vigumu kukadiria athari. Mwezi Novemba, WHO iliangazia viwango vya chini vya chanjo miongoni mwa wafanyakazi wa afya barani Afrika, ambayo ilisema kuna uwezekano wa kuwepo kwa sababu ya kusitasita kwa chanjo pamoja na upatikanaji wake.

Changamoto za upatikanaji wa chanjo

Mataifa ya Kiafrika yanategemea chanjo kutokana na mikataba waliyoingia na misaada pamoja na mpango wa kimataifa wa kugawana chanjo wa Covax, ambao unanuiwa kusaidia nchi maskini zaidi kupata chanjo.

Mapema mwaka huu nchi nyingi zilihangaika kupata vifaa, ingawa hali imeimarika sana katika miezi michache iliyopita. Nchi tajiri zaidi zilitangaza misaada kupitia Covax au moja kwa moja kwa mataifa ya Afrika katika mkutano wa kilele wa G7 nchini Uingereza mwezi Juni.

Matatizo yanayoikabili sasa yanahusiana zaidi na utaratibu wa utoaji ndani ya nchi badala ya usambazaji wa chanjo zenyewe.

"Huku vifaa vinavyoanza kuongezeka, ni lazima sasa tuimarishe umakini wetu katika vikwazo vingine vya chanjo. Wanajumuisha ukosefu wa fedha, vifaa, wahudumu wa afya na uwezo wa kuwa na baridi kwa muda mrefu pamoja na kukabiliana na kusitasita kwa chanjo," anasema Matshidiso Moeti.

Kulingana na data za hivi karibuni za WHO, Kati ya chanjo zilizotolewa hadi sasa barani Afrika, 63% zinasimamiwa. Ingawa, karibu nusu ya nchi zimetumia chini ya 50% ya dozi zilizopokelewa.

Ni nini kilisababisha uhaba wa chanjo mapema?

Tatizo kubwa linaloukabili mpango wa Covax - ambao mataifa mengi ya Afrika yalikuwa yakitegemea - ilikuwa utegemezi wake wa chanjo kutoka Taasisi ya Serum ya India, kampuni kubwa zaidi ya kutengeneza chanjo duniani.

India ilisitisha uuzaji nje wa chanjo mwezi Aprili ili kutatua mahitaji yake ya dharura, na watengenezaji wengine walikabiliwa na maswala ya kuongeza uzalishaji.

Nchi tajiri pia zilikuwa zimetia saini mikataba na watengenezaji kwa ajili ya chanjo za baadae mwezi Julai 2020 wakati zikiwa bado katika maendeleo na zikifanyiwa majaribio.

Walipewa kipaumbele na watengenezaji na kufanya kuwa vigumu kwa mpango wa Covax, Umoja wa Afrika na nchi moja moja kupata dozi. Septemba, taarifa ya Covax ilisema inapunguza makadirio yake ya idadi ya dozi ambayo anatarajia kupokea kwa mwaka huu wote na hadi 2022.

Taarifa iliyotolewa mwezi Desemba ilisema kwamba ingawa usambazaji wa Covax ulikuwa umeongezeka, bado kulikuwa hakuna uhakika juu ya idadi ya dozi ambayo inaweza kupata.

WHO inasema Afrika inahitaji zaidi ya dozi za chanjo milioni 900 ili kuwachanja kikamilifu asilimia 40 ya wakazi wake.

Kufikia Disemba 30, Afrika ilikuwa imepokea zaidi ya dozi milioni 474 kwa jumla kutoka mpango wa Covax pamoja na mpango wa kupata chanjo wa Umoja wa Afrika kupitia mikataba baina ya nchi.