Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Safari za ndege kutoka Nairobi hadi Dubai zasitishwa
Safari za ndege zenye usafiri wa abiria kuingia na na kupitia Dubai kutoka Kenya zimesitishwa kwa muda wa saa 48 kuanzia leo.
Kulingana na agizo kutoka kwa Mamlaka ya Usafiri wa Anga ya Dubai, wateja hawatakubaliwa kusafiri kwa ndege za Emirates jijini Nairobi wakati huu. Hakuna sababu maalum iliyotolewa.
Katika taarifa kwenye tovuti yake, Emirates ilisema shughuli za abiria kutoka Dubai hadi Nairobi hazijaathiriwa.
"Wateja walioathirika hawahitaji kutupigia simu mara moja ili kusajili upya nafasi tena. Wateja wanaweza kushikilia tikiti yao ya Emirates na safari za ndege zikirejea, wawasiliane na wakala wao wa usafiri au ofisi ya kuweka nafasi ili kupanga mipango mipya ya usafiri."
Mnamo Mei, Kenya ilikataa ombi la Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) la kuongeza safari za ndege kutoka Dubai hadi Nairobi, na Nairobi hadi Dubai.
Katika hatua inayoonekana kulinda shirika la ndege la Kenya Airways, Waziri wa Uchukuzi wa nchi hiyo James Macharia alisema serikali imeazimia kunyima ndege za Emirates ruhusa ya kusafiri kati ya miji hiyo bila vikwazo.
Emirates ilifanya safari 14 kwa wiki kutoka Dubai hadi Nairobi na kurejea tena Nairobi hadi Dubai. Lakini pamoja; safari kutoka kwa mashirika yote ya ndege kutoka UAE, ikiwa ni pamoja na Etihad na Qatar Airways, ni 28 kwa wiki.
Waziri huyo ambaye wakati huo alikuwa akifika mbele ya kamati ya Seneti alieleza kuwa uamuzi wake ulilenga kulinda maslahi ya taifa ikizingatiwa kuwa mkataba wa sasa wa huduma za anga kati ya nchi hizo mbili ulikuwa wa "upande mmoja na unaopendelea Emirates".