Rumba ya Congo yashinda hadhi ya kulindwa na UNESCO

Muda wa kusoma: Dakika 3

Moja ya aina ya muziki na dansi yenye ushawishi mkubwa zaidi ya Kiafrika, rumba ya Congo, sasa ina hadhi ya kulindwa na Unesco.

Ni kilele cha kampeni za nchi mbili - Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na nchi jirani ya Congo-Brazzaville.

Zote mbili zinamiliki ufalme wa zamani wa Kongo - ambapo mtindo huo wa muziki ulianzia kulingana na ombi la pamoja la mataifa hayo mawili.

Neno "rumba" lenyewe linatokana na I neno la Kikongo navel, "Nkumba".

Rhumba ya Congo inaungana na tamaduni zingine kama muziki wa reggae wa Jamaica na chakula cha wachuuzi wa Singapore zilizo katika orodha ya Unesco ya "Urithi wa kitamaduni usioonekana wa wanadamu"

Shirika la Umoja wa Mataifa la kitamaduni linasema kutoa hadhi hii kunasaidia "kudumisha utofauti wa kitamaduni katika kukabiliana na kuongezeka kwa utandawazi".

Muziki na dansi zilikuja kuwa alama ya vita dhidi ya ukoloni katika Karne ya 20, anabainisha Mkurugenzi Mkuu wa Unesco Audrey Azoulay, akiongeza kuwa ni "asili ya kisiasa ya muziki huu ambayo inawapa msukumo wasanii wengi duniani kote leo".

Licha ya asili yake ya Kiafrika, rumba katika akili za watu wengi nje ya bara imekuwa ikihusishwa na densi ya Kilatino. Hakika, rumba ya Cuba ilipewa hadhi ya urithi wa kitamaduni usioonekana wa UNESCO mnamo 2016.

Rumba "imekuwa sehemu ya utambulisho wetu, vizazi vya Afrika na sisi sote, katika enzi zote," alisema waziri wa Utamaduni wa DR Congo Catherine Kathungu Furaha mapema mwaka huu. "Tunataka rumba itambuliwe kuwa yetu ndio utambulisho wetu.

"Wazee wetu waliopelekwa nje ya nchi walipotaka kukumbuka historia yao, asili yao, kumbukumbu zao, walicheza ngoma ya kitovu."

Mtindo wa rumba ulioibuka nchini Cuba katika Karne ya 19 ulitokana na upigaji ngoma wa watumwa kutoka Afrika ya kati, ambao wakati huo uliunganishwa na nyimbo za wakoloni wa Uhispania wa Cuba.

Lakini mdundo ulihifadhi asili yake ya kipekee - kiasi kwamba, wakati rekodi za vinyl ziliposafirishwa hadi Afrika ya kati katika Karne ya 20 ilitambuliwa mara moja kama rumba.

Miongoni mwa magwiji wa mwanzo wa rumba ya Kongo walikuwa Wendo Kolosoy, Paul Nkamba, Franco na TPOK Jazz, Tabu Ley Rochereau na Dk Nico.

Wakati mataifa ya Kiafrika yakipigania uhuru kutoka kwa watawala wao wa kikoloni, The Independence Cha Cha ya Le Grand Kallé iliwatia moyo watu wengi na kuonekana kama wimbo wa kwanza wa Afrika nzima.

Baadaye muongo huo ulishuhudia kuwasili kwa Zaïko Langa Langa na nyota yake ya kuzuka Papa Wemba. Miongoni mwa wafuasi wake wengi alikuwa Koffi Olomidé, ambaye bado anajulikana leo pamoja na nyota wachanga kama vile Fally Ipupa.

Kuna mjadala kuhusu iwapo wanamuziki wa rumba ya kizazi kipya umesalia na asili ya mziki huo.

"Hatukutumia ngoma, tulitumia maracas - na hatukuitupa, ilikuwa na upole. Hiyo ni rumba. Unapocheza rumba na watu wasakata densi, huwa wametulia," Dawa Lusambu, Mkurugenzi wa sanaa wa TPOK Jazz, talimwambia mwandishi wa BBC Emery Makumeno mjini Kinshasa.

"Sio kama vijana wa leo, ambapo unacheza rumba na kutoa jasho. Hiyo sio rumba."

Si hivyo, anasema mwanamuziki Fred Kabeya: "Rumba bado ni rumba - tunajaribu kuongeza ladha zaidi na nyimbo zaidi, lakini kwa kuzingatia rumba halisi ya Congo kwenye msingi wake."

Hakuna shaka kwamba ushawishi wa rumba unaonekana duniani kote, na wapenzi wake wanasema ni sawa kwamba hii itambuliwe na Unesco na kufaidisha kizazi kijacho cha wanamuziki.

"Hatupaswi kupumzika," Prof André Yoka Lye Mudaba, wa baraza la kitaifa la kukuza rumba nchini DR Congo, aliambia BBC. "Hii ni motisha kwa sera madhubuti ya kuimarisha taaluma ya tasnia ya ubunifu."