Simulizi ya kijana anayemsaidia mama yake kufa 'kifo cha heshima' Colombia

Martha Sepúlveda anafurahi kwa sababu atasaidiwa kufa siku ya Jumapili Octoba, 10 mwendo wa saa moja asubuhi.

Anatabasamu huku akila vitafunio na kunywa bia katika mgahawa mmoja mjini Medellín, ijapokuwa kifo kinamkodolea macho.

Martha ana furaha kwa sababu amefanikiwa kupata idhini ya mahakama ya kusaidiwa kufa kupitia utaratibu unaofahamika kama euthanasia.

Nchini Colombia, euthanasia iliharamishwa mwaka 1997, lakini ilifanywa sheria 2015.

Julai iliyopita, Mahakama ya Kikatiba nchini humo iliwapa haki ya kifo cha heshima, watu ambao "wanapitia uchungu wa kimwili na kiakili" kutokana na jeraha au ugojwa ambao hauna tiba.

Martha Sepúlveda ni mtu wa kwanza kupewa idhini kufanyiwa utaratibu wa kusaidiwa kufa ijapokua ugonjwa anaougua haukuwa umefikia kiwango cha kumlazimu kuchukua hatua hiyo.

Kulingana na shirika la EFE, Wizara ya Afya imefanya jumla ya taratibu 94 za euthanasia nchini kuanzia Aprili 2015 hadi Mei 8,2020

Kwa Martha, tangu alipopatikana na ugonjwa unaoathiri mfumo wa neva na ambao hauna tiba maisha yaligeuka kuwa mateso.

Kugundua kuwa chake kitakuwa kifo cha pole pole na cha uchungu ambacho kitadumu kwa miaka kadhaa, kulimkosesha matumaini ya kuishi.

Hadi alipomwambia Federico, mwana wake wa pekee mwenye miaka 22, kwamba anataka kwenda mahakamani kuwasilisha ombi la kutaka kusaidiwa kufa.

Madaktari hawakumpatia matumaini kwa sababu moja ya mashrati yaliyowekwa na sheria ya Colombia kupata utaratibu huo ni kwamba muda wa mgonjwa kuishi uwe chini ya miezi sita.

Martha, angeliweza kuishi na ugonjwa huo kwa angalau miaka mitatu. Hata hivyo, alipambambana mahakamani hadi akafikia lengo lake.

Cha kushangaza ni kuwa idhini ya kumwezesha kusaidiwa kufa ilimpatia raha na utulivu mkubwa.

"Mama yangu amekuwa mtulivu na mwenye furaha tangu alipoambiwa anaweza kufa kwa sababu maisha yake hayakuwa mazuri kabisa," anasema mwanawe wa kiume katika mahojiano na BBC Mundo.

Na hivi ndivyo anavyochukulia uamuzi huo- ana furaha kwa sababu atakufa.

"Nina bahati," alisema kwenye mahojiano yake ya mwisho katika runinga ya Caracol TV. "Nacheka zaidi, Napata usingizi mwanana."

"Mimi ni Mkatoliki, Najichukulia kuwa muumini sana. Lakini Mungu hataki kuniona nikiteseka."

"Ugonjwa niliyonayo ya lateral sclerosis- unaoathiri mfumo wa neva, jambo zuri kwangu ni kupumzika."

Ifuatayo ni simulizi ya mwanawe wa kiume, Federico Redondo Sepúlveda, katika mahojiano ya ana kwa ana aliyofanya na BBC Mundo.

Mama yangu alipatikana na ugonjwa unaoathiri mfumo wa neva mwishoni mwa 2018.

Alipokelea taarifa hizo kwa njia ambayo sio ya kawaida. Alicheka na kusema "nina ugonjwa ambao utaniua ndani ya miaka mitatu." Lakini alisema maneno hayo kana kwamba anafanya utani.

Mama yangu ni mtu ambaye amekuwa na msimo huru kuhusu kifo. Amekuwa akisema "Siogopi kufa, ila naogopa kile kitakachoniua", ndio sababu aliamua kupigania kupata haki ya ''kufa kifo cha heshima''.

Hakutaka maisha ya kuwa kitandani hadi umauti utakapomfika. Hatua ya mwisho ya mgonjwa anayeugua amyotrophic lateral sclerosis- unaoathiri mfumo wa neva, ni kushindwa kuzungumza, kushindwa kumeza chakula... yaani ni hali ngumu sana ambayo hastahili kupitia.

Kushindwa kutembea

Mwanzoni hali yake haikuwa mbaya vile. Lakini baadaye alianza kuishiwa na nguvu miguuni, hadi alihitaji usaidizi kutembea au alilazimika kutembea mwendo mfupi. Muda ulivyosonga ndivyo hali yake iliendelea kudhoofika kwani alihitaji kusaidiwa kutembea kila mahali hata ndani ya nyumba.

Mapema mwaka huu alilazimika kutafuta usaidizi wa kwenda chooni. Kisha ilibidi asaidiwe kuoga, kuvalia nguo na kadhalika. Wakati mwingine hata kupiga mswaki na kula nishida kwa sababu amepoteza nguvu sana.

Kilichomuathiri zaidi ni kuona jinsi hali yake ilivyozoroteka kiasi cha kushindwa kabisa kujifanyia vitu vya kawaida na vya kila.

Siku moja aliniambia: "Bora niombe kusaidiwa kufa." Kusema kweli sikutilia maanani.

Lakini aliponiambia hivyo tena mara ya pili, Nilisikitika sana. Haikuniingia akilini nakwa siku kadhaa nilipata usumbufu wa kimawazo. Nilijipata nikisema, "Hapana, mama yangu hajatimiza muda wa kuondoka." Ningelisema, "Mama tafadhaliusifanye hivyo. "

Ninajiona kuwa mtu huria sana, nilifikiri kuwa haki ya euthanasia ni haki ambayo inapaswa kulindwa, lakini sikuwahi kufikiria nitajipata katika hali hii.

Lakini baada ya kutafakari kwa makini madhila anayopitia, nilijiambia: " Nadhani njia pekee ya kuonesha upendo wangu kwake ni kuheshimu na kukubali uamuzi aliofikia.

Nataka kuwa na mama yangu sijali yuko katika hali gani. Lakini kufanya hivyo nitakua na ubinafsi kwa kuweka mbele mahitaji yangu bila kujali hali anayopitia.

Tumekuwa Pamoja kwa miaka 22. Maisha yangu yalikuwa yamezingirwa na upendo wake kwangu. Akiondoka itabidi nianze upya Maisha. Ndio sababu mwanzoni ilikua vigumu sana kwangu kuridhia ombi lake.

Nilipokua nikimhudumia nilifanya hivyo kwa hisia mchanganyiko. Kwa upande mmoja nilipenda kumhudumia kwa sababu, nilihisi nalipia fadhila aliyonifanyia maishani mwangu.

Lakini pia nilikuwa nikifikiria juu ya kile alichokuwa akiniambia: "Mwanangu, huu sio uzima, sistahili kuishi hivi."

Ni wazi nina huzuni. Nasikitika sana, nahisi ... kukata tamaa kwa namna fulani. Itakuwa jambo la kushangaza sana nikisema nimeridhia ombi lake kwa moyo mkunjufu.

Lakini pia nifarijika kwamba mama atakamilisha maisha yake duniani vile alivyotaka.