Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Siasa za Tanzania; Upi mustakabali wa uhusiano wa 'mashaka' kati ya Msajili, vyama vya siasa na Polisi?
- Author, Markus Mpangala
- Nafasi, Mchambuzi, Tanzania
Uamuzi wa vyama vinne vya upinzani vyenye nguvu kususia mkutano ulioitishwa na Ofisi ya Msajili wa vyama vya siasa nchini Tanzania ni kielelezo cha uhusiano usioridhisha kati yake na vyama pamoja na Jeshi la Polisi ambalo mara kadhaa limelaumiwa na viongozi, wanachama na wafuasi wa upinzani na wanaharakati kuwa kiini cha migogoro ya pande hizo na mwendelezo wa kuporomoka uhuru wa kujieleza kwa kipindi cha miaka sita ambacho kimeshuhudia madhila makubwa kwa baadhi ya wanasiasa, vyama, viongozi na shughuli za kisiasa kwa ujumla wake.
Vyama vilivyotangaza kutoshiriki mkutano huo ni CUF, NCCR-Mageuzi, ACT-Wazalendo na Chadema kwa nyakati tofauti vimetangaza kutoshiriki kikao kati ya wadau wa siasa, Msajili na Jeshi la Polisi ambacho kimepangwa kufanyika Oktoba 21, 2021 katika makao makuu ya nchi hiyo jijini Dodoma.
Hata hivyo, Ofisi ya Msajili wa vyama vya Siasa kupitia Msajili Msaidizi, Sisty Nyahoza tayari ametangaza kuwa mkutano huo utafanyika kama ulivyopangwa kwani unahusisha wadau wengi vikiwemo vyama 19 vyenye usajili wa kudumu hivyo kukosekana kwa wadau wachache hakuwezi kuzuia mkutano kufanyika.
Duru za kisiasa zinaeleza kuwa sababu zilizochangia vyama hivyo kugomea mwaliko ni matokeo ya mwenendo usioridhisha wa Msajili wa vyama vya siasa, Jaji Francis Mutungi, Jeshi la Polisi pamoja na hali ya kisiasa yenye vikwazo vya kuminywa sauti za wanasiasa wa upinzani na vyama vyao, wanaharakati, watu binafsi, vyombo vya habari pamoja na 'kamata kamata' na mashtaka dhidi ya wafuasi wa upinzani, ni miongoni mwa mambo ambayo yamechangia kudorora kwa heshima na uhusiano wa taasisi za kisiasa machoni pa umma.
Kwa mujibu wa Katiba ya Tanzania, vyama vya siasa vipo chini ya Ibara ya 3 na sheria namba 5 ya vyama vya siasa. Pia shughuli za vyama hivyo zinafafanuliwa katika Ibara ya 11 ya vyama vya siasa, ambapo Jeshi la Polisi na Ofisi ya Msajili ni wadau wa masuala ya kisiasa ambao wanawajibika katika ulinzi na usalama na kusimamia na kulea vyama vya siasa.
Sababu za vyama vya upinzani kususia
Septemba 6 na 7 mwaka huu vyama hivyo vilitoa matamko kwa nyakati tofauti kuelezea dhamira zao za kususia mkutano huo huku vikitoa malalamiko na masharti mbalimbali.
Matamko ya vyama hivyo yalitolewa na Edward Simbeye (Mkuu wa Idara ya Uenezi na Mahusiano ya Umma wa NCCR-Mageuzi), John Mrema (Mkurugenzi wa Itikadi,Uenezi na Mambo ya Nje wa Chadema, na taarifa rasmi ya chama cha ACT Wazalendo ilitolewa na Salim Bimani pamoja na Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba, ambapo wameeleza yafuatayo;-
• Mkutano umeitishwa na wadau ambao walikata maridhiano ya kisiasa na wanaongoza kuvunja Katiba kuzuia shughuli za siasa.
• Kuzuiwa vikao vya Kamati kuu za vyama vya siasa kwa kile kinachoitwa 'Intelijensia ya polisi' kubaini viashiria vya uvunjifu wa amani ikiwa ni kinyume cha hali halisi.
• Jeshi la Polisi ni watuhumiwa namba moja katika kuvunja sheria na kudaiwa kukandamiza vyama vya siasa na kuwakamata wanasiasa wa upinzani.
• Msajili kutumia vibaya Ofisi yake kukandamiza vyama vya upinzani na kukipendelea chama tawala - Chama Cha Mapinduzi (CCM) kufanya shughuli za siasa kwa uhuru kwa takriban miaka sita mfululizo tangu mwaka 2015.
• Viongozi wakuu wa chama watakuwa kwenye mkutano mkuu wa Kitaifa wa Haki,Amani na Maridhiano ulioitishwa na Kituo cha Demokrasia Tanzania.
• Viongozi, Wanachama na wafuasi wao kukamatwa sehemu mbalimbali kwa madai ya kufanya shughuli za kisiasa.
Je, vyama vya upinzani vimetoa masharti gani?
• Chama cha NCCR Mageuzi kinataka kukutanishwa na viongozi wenye dhamana ya Usalama wa raia na vyama vya siasa au rais wa Tanzania.
• ACT Wazalendo kimetoa sharti la kujumuishwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi kwenye mkutano huo.
• Chadema ambacho kiliomba maridhiano tangu sherehe za uhuru mwaka 2019 kinataka kukutana na rais Samia Suluhu Hassan peke yake.
• Vyama vyote vinataka kuruhusiwa shughuli za kisiasa ikiwemo mikutano ya hadhara, vikao vya ndani kwa uhuru.
• Upande wao chama cha CUF kinakubaliana na madai mengi yaliyotolewa na vyama vingine.
• Kuondoa upendeleo unaofanywa na Msajili na Jeshi la Polisi kwa chama tawala, CCM
• Wimbo wa haki umeimbwa na vyama vyote, ambavyo vinataka kuona inatendekea bila ubaguzi kuanzia uchumi na jamii.
Madai ya Ofisi ya Msajili kuvivuruga vyama vya upinzani yanathibitishwa na hofu ya Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar Othman Masoud wakati wa mahojiano ya Kipindi cha Medani za Siasa cha Star TV yaliyofanyika mnamo Oktoba 2, 2021.
"Hiki tunachokifanya kulea makosa ya Msajili wa vyama vya siasa anaweza kupindua na kuondoa serikali kirahisi tu kwa kusema kuwa rais si mwanachama wa chama hiki,"
Katibu Mkuu wa ACT Wazalendo, Ado Shaibu wakati wa ziara ya kichama katika majimbo ya Mkuranga, Rufii na Kibiti mkoani Pwani mnamo Septemba 18, 2021, alisema "Hakuna sheria inayotutaka tutoe taarifa ya Kikao cha ndani, Sisi ACT Wazalendo tutafanya tena vikao bila kificho wala kungojea ruhusa ya Jeshi la Polisi."
Ni zipi athari za kisiasa?
Ufa mkubwa baina ya taasisi umejitokeza. Uhusiano kati ya wadau wakubwa wa siasa ambao ni vyama, Msajili na Polisi umeingia doa na kutengeneza uhasama baina yao ndani ya taifa moja.
Kwanza; Matabaka ya kisiasa; vipo viashiria vya upendeleo wa kisiasa kuonesha wazi kuwa kiini cha matabaka kinajengwa kwa umahiri na viongozi wenye dhamana, ambao hao hao baadaye watashangaa itakapotokea usahama baina ya matabaka hayo.
Mifano midogo ni hivi karibuni ambapo Jeshi la Polisi lilizuia mbio za mazoezi ya Baraza la Wanawake wa Chadema (Bawacha) kwa madai ya kuzusha hisia za kisiasa. Wakati Bawacha wakuzuiwa, Jeshi la Polisi halikuchukua hatua hiyo dhidi ya Umoja wa Vijana wa Chama tawala(UVCCM) na Umoja wa Wanawake wa CCM ambao walifanya mazoezi hayo huku wakipewa ulinzi.
Kuzuiwa kufanya makongamano ya Katiba, mathalani Chadema walilalamikia hatua ya Polisi kuondoa mahema na kufunga ofisi za chama hicho na kuchukua viti vilivyoandaliwa kukaliwa na wageni huko Musoma mkoani Mara. NCCR-Mageuzi kuzuiwa kufanya mkutano wao wa ndani. Hali hii ni kama Jeshi la Polisi linafanya ndivyo sivyo, kisha lianze kusaka watu wengine kuwa vyanzo vya hali hiyo.
Pili, jitihada kubwa zinafanyika kuharamishwa karibu kila kitu cha kisiasa na kujumuishwa katika maneno machache yafuatayo; Mikutanao ya hadhara na shughuli za kisiasa ni kama haramu. Vikao vya ndani vya Kamati Kuu za vyama ni kama haramu. Makongamano ya kisiasa ni kama haramu. Uanaharakati ni kama haramu. Kuwa mwanasiasa wa vyama vya upinzani ni kama haramu. Kile kinachoonekana kuwa upendeleo kwa chama tawala ni kama halali. Uanachama na ufuasi wa upinzani ni kama haramu. Elimu ya uraia ni kama haramu.
Hannah Njulumi, Mwanahabari mwandamizi wa masuala ya siasa na utawala bora kutoka Redio A.FM ya jijini Dodoma amemwambia mwandishi wa makala haya, "kwanza ni aina ya msuguano ambao kwa kipindi hiki na siasa za Rais Samia hauna maslahi yoyote, si kwa chama tawala wala kwa upinzani, unaendeleza uhasama uliokuwepo kipindi cha Rais John Magufuli (aliyefariki dunia Machi 17, 2021) lakini kwa wakati huu Samia hahitaji kabisa mbinu za kisiasa za uhasama na kulumbana kati ya Msajili wa vyama vya siasa na vyama vya upinzani kwa sababu haonekani kuwa na mpango wa kutumia njia hiyo kama kujilinda kisiasa. Msajili na Polisi wote wanatakiwa kuwa wapya kiuongozi kwa kufuata mwelekeo huu si kubaki kudemka kwa mbinu zinazodidimiza taifa na kujenga matabaka kuanzia kwenye siasa hadi huduma za jamii. Taifa la Tanzania halina utamaduni wa kujengwa kwa amri za kijeshi, bali demokrasia."
Upinzani wanaweza kuwa na imani na Msajili?
Richard Ngaya, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine anajibu swali hilo kwa kusema, "Kwa vyama vya siasa ukiachilia mbali chama tawala vinafahamu wazi kuwa Ofisi na Msajili ni moja ya Ofisi isiyo na mamlaka yoyote kisiasa bali hupokea maagizo kutoka chama tawala. Kifupi ni jambo la ajabu mtu anayetarajiwa kuteuliwa na Rais ambaye kimsingi ni Mwenyekiti wa chama kimojawapo cha siasa kusimama katikati akiwa mwamuzi wa mchezo wa siasa. Zaidi imejidhihirisha wazi mara nyingi namna Msajili alivyoshindwa kusimama katikati wakati wa kushughulikia changamoto kwenye vyama mbalimbali.
Aghalabu amekuwa mtu wa kutoona makosa yoyote kwenye chama tawala bali upinzani huwa wakiteleza kidogo tu anawahi kuwaandikia barua za onyo ama kujieleza, kwa mfano tukio la Julai mwaka huu aliwataka Chadema kueleza sababu za kuwafukuza uanachama wabunge 19 wa viti maalumu. Msajili alieleza kuwa alipokea malalamiko kutoka kwa wabunge hao. Huu ni mfano wa mazingira magumu yanayochangia msuguano na kukosekana imani, ingawaje mazingira hayo yanaweza kupunguzwa ili kuleta usawa. Viasharia vyote vya upendeleo viondolewe na kujenga imani."
Hata hivyo, licha ya kunyooshewa kidole mara kadhaa, Ofisi ya Msajili wa vyama vya siasa imekuwa ikisema kuwa yenyewe inafuata taratibu za sheria na kanuni zilizopo bila kupendelea upande wowote na kwamba ni wajibu wa kila mdau kufuata taratibu hizo kikamilifu.