Siasa za Tanzania:Kwanini uhusiano wa serikali ya Tanzania na upinzani umeendelea kuzorota?

    • Author, Rashid Abdallah
    • Nafasi, Mchambuzi, Tanzania

Ushindani katika siasa ni jambo lisiloepukika. Ndio msingi wa uwepo vyama vingi. Kushindana kwa sera, hoja, kupingana na kukosoana. Uhusiano wa utawala na vyama vya upinzani sio kama wa mume na mke. Ingawa kinyume chake haupaswi kuwa wa uadui na uhasama.

Upande mmoja wa Muungano, visiwani Zanzibar kwa sasa hali imetulia kwa kuwepo maridhiano kati ya utawala na upinzani. Chama tawala kinafanya siasa zake na upinzani unafanya za kwake. Pia, kuna ushirikiano wa pande hizo mbili katika serikali.

Upande wa Tanzania bara uhusiano wa utawala na upinzani umekuwa wa uhasama kwa takribani miaka sita sasa. Mivutano ya panda hizo mbili ni mikubwa. Na bado nyota njema ya kupunguza joto aijachomoza.

Sera hai za Magufuli!

Mwezi Julai na mwanzoni mwa Agosti mwaka huu; vyombo vya usalama vimeendesha operesheni kadhaa za kuwakamata wafuasi na viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), sanjari na kuvamia mikutano yao ya ndani.

Wafuasi wa Chadema takribani 10 akiwemo Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe walikamatwa jijini Mwanza Julai 20. Mwenyekiti huyo bado ameshikiliwa kwa tuhuma za vitendo vya ugaidi, shitaka ambalo halina dhamana.

Mara baada ya maandamano ya Baraza la Wanawake Chadema (BAWACHA), mbele ya Ubalozi wa Marekani jijini Dar es Salaam Julai 28, kushinikiza kuachiwa kwa Mbowe. Chama hicho kilitoa taarifa ya kukamatwa baadhi ya washiriki wa maandamano hayo.

Chadema ilieleza pia kwa vyombo vya habari, kati ya Agosti 3 na 5 wafuasi wake wapatao 41 walikamatwa. Miongoni mwao ni walioandamana nje ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam.

Nchini Tanzania maandamano na mikutano ya kisiasa ni halali kisheria.

Licha ya mambo hayo kuendelea kuugonganisha utawala na upinzani. Wengi wa waliokamatwa katika operesheni hizo tayari wameachiwa.

Swali ni; siasa za namna hiyo zitakwenda hadi lini?

Miaka yote ya msigano, chama tawala kwa upande wake, Chama cha Mapinduzi (CCM) hakionekani kukumbana na vuta nikuvute na Polisi. Hata wakati wa utawala John Pombe Magufuli, vyombo vya habari viliripoti uwepo wa mikutano ya hadhara ya CCM wakati mikutano ya upinzani ikizuiwa.

Pia vyombo vya habari viliripoti uwepo wa mikutano ya ndani ya CCM wakati mikutano ya ndani ya vyama vya upinzani ikikumbana na uvamizi wa mara kwa mara na kamatakamata isiokwisha kutoka kwa Jeshi la Polisi.

Na sasa hali inaonekana kurudi kama zamani. Ni rahisi kusema, zile sera zinazokosolewa na wengi ambazo zinakandamiza uhuru wa kisiasa zimeendelea kuwa hai hata baada ya alieziasisi kufariki - yaani hayati Magufuli.

Utamaduni wa ukandamizaji

Licha ya ukosolewaji mkubwa juu ya kinachoendelea katika siasa za Tanzania, alipoulizwa katika mahojiano na Shirika la Utangazaji la Uingereza, BBC, ikiwa Tanzania ni nchi inayofuata demokrasia. Rais Samia alieleza na kurudia kwamba nchi hiyo ni ya kidemokrasia sana.

Lakini nimemuuliza Mhadhiri wa Sayansi ya siasa na utawala kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam,

Dk. Muhidin Shangwe, kipi hasa kinausukuma utawala wa CCM wakati wa Magufuli na sasa kutoruhusu mikutano ya kisiasa na maandamano?

"Huku kubinya haki za kisiasa dhidi ya vyama vya upinzani, ni mbinu ya utawala kuendelea kubaki madarakani. Wanakataza vyama kufanya siasa au kuviwekea mipaka. Wakati katiba haisemi hivyo. Wakizuia hiyo mikutano hawataji kifungu chochote cha sheria kutetea hizo marufuku. Ni utamaduni wa ajabu unaota mizizi."

Kikao cha Samia na Upinzani

Aprili 22 mwaka huu, akitoa hotuba yake ya kwanza iliyotoa dira ya serikali yake ndani ya Bunge jijini Dodoma, Rais Samia alieleza azma yake ya kutaka kuonana na vyama vya kisiasa nchini.

Kikao hicho kilitegemewa na wengi kufanyika mara moja tu baada ya tamko hilo. Ila mambo yamekwenda kando ya matarajio ya wengi. Hadi sasa bado hakijafanyika.

Alipoulizwa kuhusu ahadi hiyo na BBC, Rais Samia alieleza bado ana nia ya kukutana na viongozi wa upinzani. Ingawa hakuweka wazi siku rasmi ya kukutana nao.

Utawala wake ulipongezwa ndani na nje kwa kubadili msimamo juu ya janga la Uviko 19. Msimamo ulioacha nyuma sera za mtangulizi wake. Pia, alifufua uhuru uliokufa kwa kuvitoa vifungoni baadhi ya vyombo vya habari.

Mvutano wa sasa kati ya utawala na upinzani umechochewa zaidi na dai la upinzani la kuendelezwa kwa mchakato wa upatikanaji wa katiba mpya. Huku utawala ukieleza kuwa mchakato huo utakuja baada ya kueka uchumi wa nchi sawa.

Ilitarajiwa kikao cha pande hizo mbili kingeondosha huu mvutano wa sasa. Ikiwa utawala na upinzani ungekaa meza moja na kukubaliana wakati upi wa kuendelea na katiba mpya. Na namna gani upinzani uendelee kufanya siasa bila kuekewa vikizingiti na utawala.

Waswahili husema, lililo baharini hungojewa ufukweni. Watanzania wataendelea kuvuta subira kungonjea kile kilichoahidiwa na Rais Aprili 22 kule Dodoma na kikarudiwa kuahidiwa katika mahojiano na BBC. Muda wa kusubiri upo!.

Kivuli cha Magufuli ndani ya Samia

Moja ya katuni maarufu nchini Tanzania, ambayo hutembea katika mitandao ya kijamii. Ni ile inayomuonesha mwanamke aliyevaa hijabu, kasimama mbele ya mimbari. Nyuma yake kuna kivuli cha mwili wake ambacho kina sura ya mwanaume.

Ingawa si kazi rahisi kutafsiri katuni. Lakini kwa hakika msanii amekusudia kufikisha ujumbe ambao Watanzania wengi wanaonekana kuuwelewa hasa unaposoma maoni yao katika mitandao ya kijamii - yaani mtawala anaefuatwa na kivuli cha mtangulizi wake.

Swali linaloulizwa na wengi: Je, Rais Samia anaendeleza kwa makusudi sera za kuandama upinzani au ameshindwa kuwa na uthibiti na watendaji wake ambao wengi wao wametokea katika utawala uliopita?

Jawabu yoyote iwayo kwa swali hilo. Haindoshi ukweli kwamba Rais huyo kwa sasa ana wajibika pakubwa kwa kinachoendelea katika nchi. Bado Tanzania sio uwanja salama kwa siasa za upinzani.

Nilimuuliza tena Dk. Shangwe, utawala unatoa wapi hizi nguvu za kutoa amri zinazokwenda kinyume na sheria?

"Hayo yanaendelea kufanyika kwa sababu kuna kinga, utawala haukumbani na athari yoyote unapokiuka misingi ya katiba na sheria. Hivyo aliyefanya jana atafanya tena kesho na kesho kutwa na akija mwingine naye atafanya hivyo hivyo."