Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Waridi wa BBC: Fahamu misukosuko aliopitia muigizaji wa Tanzania Irene Paul kabla ya kupata fursa alionayo
- Author, Anne Ngugi
- Nafasi, BBC Swahili
Jina lake mwanadada Irene Paul sio geni mno katika fani ya burudani hasa nchini Tanzania . Mwanadada huyu ana sifa za kuwa muigizaji hodari , kando na hayo yeye ni mama na mke.
Ni mwanamke aliyeshiriki filamu na vipindi kadhaa na kwa sasa anaonekana kwenye kipindi cha Jua Kali na filamu mbalimbali kwa mfano Love & Power, Kibajaji, Kalunde, Fikra Zangu, Penzi la Giza, I Hate My Birthday na nyinginezo.
Irene anatajwa kama mwanadada anayejua kuzitendea haki nafasi anazopewa kuigiza.Tulipozungumza na Irene hakutaka kukubali kwamba ana umaarufu mkubwa
"Sitaki kusema kuwa nina umaarufu mkubwa , ila ninachoweza kusema ni kuwa kazi zangu zinatambulika mno , hasa kwa kuwa ninafanya kazi na televisheni basi mtu atajulikana kwa haraka kuliko kazi nyingine "anasema Irene.
Uigizaji ambao amefaulu kuufanya kwa filamu za kiTanzania ni kwa kipindi cha miaka 11 .Muda huu Irene anasema ameutumia kujitafutia nafasi ambazo zinasongesha taaluma yake hata juu zaidi . Hivi sasa analenga kuimarisha ndoto za wanawake na wasichana katika kanda hii .
Irene Paul , alianza kwa kuwa mtangazaji kwa miaka kadhaa kabla ya kujiunga na uigizaji.
Uigizaji katika kipindi maarufu cha Jua Kali
Kipindi hiki ni cha tamthilia ambayo mwanadada huyu anaigiza kama mama wa kambo , katika familia yenye baba mzee aliye na watoto ambao mmoja wao ni umri sawia na wa mama wa kambo .
Tamthilia hiyo imelenga sana kuangazia hali zinazofanyika kwenye baadhi ya ndoa barani Afrika ambapo katika ndoa yake Irene anasema kuwa kuna vituko na vitimbi vya kila aina vinavyofanyika
"Kwa mfano kuna vituko ambavyo mama wa kambo , pamoja na watoto wa mume wanakosana .Vilveile, kuna matukio ya mume katika tamthilia hio ambapo anahusishwa kimapenzi na mwanamke mwengine ambaye ni msichana wa umri mdogo . Ukweli ni kwamba kipindi hiki kinafuatiliwa na wengi kutokana na maisha na matukio mengi yanayoonekana kwenye jamii zetu "Irene anaongezea
Tulipomuliza kuhusu nafasi anazopewa za uigizaji na maisha yake asili kama yanalingana anacheka na kusema kuwa ;
"Kwa mfano ninapopewa nafasi ya kuigiza kama mwanamke aliyesalitiwa kwenye ndoa , ninaweza kuwa simo kwenye ndoa, lakini kwasababu mimi ni mwanamke aliyesalitiwa huwa tu ninaleta hisia zilizotokea baada ya kusalitiwa na hivyo ninaweza kuigiza kwenye nafasi hizo "Irene alielezea
Lakini Je Irene Paul ni nani ?
Irene Paul anasema kuwa amezaliwa na kusomea Tanzania . Akiwa mtoto mdogo alikuwa amefahamu kwamba alipenda sana kupigwa picha , na pia akiwa shuleni alipendelea sana masomo yaliokuwa yanaegemea sanaa na mawasiliano .Kwa wakati mmoja alitamani kuwa mwanahabari katika utu uzima kwasababu alipenda ulimwengu wa kuonekana kwenye televisheni .
Anasema kuwa alikuzwa katika hali hio , hadi akasomea mafunzo ya uanahabari chuoni .
"Nakumbuka nikiwa shuleni nilikuwa ninawaeleza wanafunzi wenzangu , munaniona hivi sasa lakini mjue kwamba kuna siku mtaniona kwenye TV .Na hata kwenye uigizaji shuleni nilijitolea katika nafasi hizo na zilikuwa zinawapendeza hata walimu wangu' anasema mwanadada huyo.
Ila anasema kwamba alikuwa anatamani kuwa mtangazaji , lakini watu wengi walimshauri kuwa anafaa zaidi kwa fani ya uigizaji , hatua iliomshinikiza kujitosa katika fani hiyo.
Changamoto za Uigizaji
Irene Paul anasema kuwa kwa mtoto wa kike kuingia katika fani hiyo ilikuwa ni kama kupita kwenye ukuta.
Anasema kwamba kama mtoto wa kike alipitia changamoto chungu nzima ili kupata fursa aliona nayo kwa sasa
Anakiri kuwa alikuwa na muonekano tofauti na vigezo vilivyoakuwa vikiangaziwa miongoni mwa waigizaji .
Kwa mfano anasema kuwa alikuwa amenenepa kupitia kiasi na kwa kuwa bado alikuwa anabaleghe uso wake ulikuwa umejaa chunusi za kawaida wanawake wanapofikisha umri huo.
"Kusema kweli sikuwa mrembo , sikuwa na urembo ambao walikuwa wanatarajia , unajua katika viwango vyao vya urembo kwa mwanamke. muigizaji. kuna kipindi Tanzania ikiwa haukutajwa kama Miss Tanzania au mlibwende nafasi za kuigiza ulikuwa hupati."Irene anasema
Irene anasimulia kipindi kimoja kizito cha kutafuta nafasi za uigizaji , kisa kimoja kingali akilini mwake alipotembea hadi sehemu moja ambapo utafutaji wa waigizaji ulikuwa unafanyika .Alipofika mbele ya jopo lililopatiwa kazi hiyo anakumbuka maneno ya jaji mmoja yaliomuwacha na hisia chungu nzima .
"Aliniuliza kwani wewe unajionaje ?
Nikamwambia naweza kuigiza , hapo hapo akanitajia zaidi ya wanadada kama kumi hivi waliokuwa walimbwende Tanzania wakati huo , hata mimi nikashangaa ,akaniambia kuwa akichagua mmoja kati ya walimbwende hao atakuwa bado na salio la wengine wazuri , kisha akaniuliza hebu tuambie tumtoe nani hapo tukuweke wewe? Hapo niliishiwa na nguvu na kuona kweli sina nafasi tena . "Irene anakumbuka
Irene hakukata tamaa , alikubali kuchukua fursa za uigizaji bila malipo na pia nafasi ndogondogo ambazo zingesaidia kumuuza na kumwezesha kuendelea na azma yake ya kutaka kuwa muigizaji bora .Hayo yote Irene aliyakubali ili aweze kujulikana japo kwa mwendo wa polepole .
Irene anasema kuwa mmoja wa watu waliokuwa kwenye jopo lililomkataa wakati mmoja alikuwa miongoni mwa watu waliomchagua miaka kadhaa baadaye kuigiza kwenye filamu mbili .
Ni ajabu kwamba Irene Paul anasema kuwa miaka kadhaa baadaye alishiriki Filamu hata na waigizaji kutoka nje ya nchi . Kilichomuuza zaidi kwao ni kuwa ana uwezo wa kuigiza kwa lugha ya kiingereza . Kuanzia wakati huo Irene anasema kuwa alianza kunawiri na kutambulika kama muigizaji .
Maisha ya ndoa
Irene Paul anasema kuwa imekuwa rahisi kudumisha ndoa yake, kwasababu alikutana na mume wake wakati ambapo alikuwa katika pilka pilka za kutafuta fursa hadi kufikia wakati huu ambapo ni muigizaji tajika.
"Nafahamu kuwa ndoa za watu mashuhuri hukumbwa na changamoto , na sitaki kusema kuwa ndoa yangu haina pandashuka , lahasha."anasema Irene
Anamsifu mumewe kuwa miongoni mwa watu wanaomuunga mkono katika kazi yake
"Nakumbuka nilipoolewa mamake mume wangu alisema nitaenda kumtesa mwanawe kwasababu ya nafasi niliokuwa nayo katika uigizaji ila nikawa namweleza mama kuwa huo ni uigizaji tu .Ila kwa sasa mamake mume wangu amekubali ndoa yetu,'' anasema.
Irene paul anasema kuwa anahisi kana kwamba wanawake bado hawajakubalika hasa wanapokuwa kwenye taaluma mbalimbali , na hilo linadhihirika wazi kupitia yale aliopitia .
Lakiini ana ushauri gani kwa wanawake wanaotaka kujiungana na fai hiyo?
Anasema uigizaji haufai kuwa jaa ambapo kila aina ya watu wanatupwa ndani yake kulingana na muonekano wao na maumbile yao mazuri bali iwe na watu ambao wana elimu na maadili