Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Baye Modou Fall: Mfungwa wa Senegal aliyetoroka gerezani mara 12
Mtoro sugu wa jela amewafanya Wasenegal wajiulize mengi baada ya kusema kuwa ametoroka gereza mara 12.
Baada ya kutoroka mwezi Mei, Baye Modou Fall alieleza jinsi alivyotoroka gerezani baada ya kuvunja kifaa cha kuingiza hewa ndani ya gereza na kupanda juu ya ukuta kwa kutumia kamba.
Anasema amekuwa akisubiri kesi yake kwa miaka tisa na baadhi ya mawakili wanasema kesi yake inaonesha haja ya kufanyika kwa mageuzi katika mfumo wa mahakama wa Senegal. .
Je Baye Modou Fall ni nani?
Baye Modou Fall mwenye umri wa wa miaka 32 anajieleza binafsi kama mfanyabiashara, aliyerithi mali kutoka kwa marehemu baba yake.
Lakini amekuwa ndani na nje ya gereza tangu amekuwa kijana, na mara nyingi kutokana na mashitaka ya wizi.
Anasisitiza kuwa sio mtu mwenye fujo na hatumii silaha.
Hajawahi kusoma katika shule ya taifa, lakini alisoma katika shule ya Koran kabla ya kujifunza kompyuta katika warsha tofauti.
Alikamatwa mara ya kwanza katika mji wa kwao Diourbel, kilomita 160 (mauli 100 ) mashariki mwa mji mkuu wa Senegal Dakar, alipokuwa mtoto
Na kwa mara ya kwanza alitoroka kutoka katika mahabusu iliyokuwa katika gereza la Diourbel.
Amekuwa akikabiliwa mara kwa mara na mkono wa sheria, kabla ya kukamatwa katika mwaka 2015 lakini mwaka uliofuatia alifanikiwa kutorokea katika nchi jirani ya Gambia.
Nyumbani Senegal.
Baada ya miezi mitano nchini Gambia, alikamatwa tena nchini Senegal, karibu na mpaka wan chi hiyo na Guinea.
Miaka minne baadaye, hatimaye alipatikana na hatia ya wizi katika mwaka 2000, lakini alikuwa bado anasubiri kesi yake juu ya mashitaka mbali mbali alipotoroka gereza wiki iliyopita.
Maafisa bado hawajathibitisha madai ya Fall kwamba alitoroka gerezani mara 12.Wakili wake wa zamani, Abdoulaye Babou, aliiambia BBC kwamba ametoroka gereza walau mara 10.
'Sio superman'
Nchini Senegal amepewa jina bandia la Boy Djinné, linalomaanisha mvulana war oho katika lugha ya Wolof, lakini wakili wake wa zamani anadhani kuwa jina hili halionesha tabia yake halisi.
"Vyombo vya habari vimemfanya kuwa superman. Ana nguvu ya ajabu," Bw Babou anasema.
"Hana umbo kubwa. Ni mwembamba sana, mfupi na ni mtu mwenye aibu sana.
"Hawezi kukutazama machoni. Sio mwizi. Hajawahi kumuua mtu yeyote ," anasisitiza Bw Babou, ambaye alimtetea Fall kwa miaka 10.
Baada ya kutoroka gerezani hivi karibuni, Fall alisema kwenye mahojiano na televisheni kwamba alikuwa ametoroka kwasababu kesi yake ilichukua muda mrefu.
Alisema kuwa amekuwa gerezani kwa miaka tisa akisubiri kesi yake ya wizi na kukwepa mamlaka.
"Kosa la kutoroka ni hukumu nyingine, ninafahamu hilo. Lakini kwasababu nimekuwa gerezani kwa miaka tisa bila kosa lolote, kutoroka huku ni kafara kwangu. Ninapambana ili ukweli ujitokeze.
Niliamua kujichukulia sheria mkononi mwangu mwenyewe
"Nilifahamu kila mara ningeweza kutoka nje ya gereza wakati wowote, mchana au usiku," aliiambia televisheni ya Senegal ITV .
"Hakuna usalama ninakofungwa katika Penal Camp, hata kama watu wanasema kinyume.
Pia alielezea jinsi alivyotoroka, kwa kuvunja kifaa cha kuingiza hewa ndani ya gereza na kukwepa kwa kupita juu ya ukuta katika gereza kwa kutumia kamba iliyokuwa imefungwa kwenye mnara wa umeme.
Alisisitiza kuwa hakuna yeyote aliyewahi kumsaidia kutoroka.
Maafisa, hatahivyo, wanapinga maelezo yake.
Inspekta wa kikanda wa magereza mjini Dakar Dakar Mbaye Sarr anasisitiza kuwa Fall amekuwa akifungwa katika eneo la gereza lenye usalama wa hali ya juu na kwamba lazima alipata usaidizi.
Anasema ameanza uchunguzi na walinzi waliokuwa zamu kati ya saa 11.00 na saa 12 .00 asubuhi wanahojiwa.
Mkurugenzi wa gereza pia amepewa majukumu mengine huku uchunguzi ukiendelea.
Fall hatimaye alikamatwa tena karibu na mpaka na nchi ya Mali, ambako aliripotiwa kujaribu kutoroka kwenye pikipiki.
'Muathiriwa wa mfumo mbovu '
Kisa cha Fall kinaonesha tatizo la ufungaji wa muda mrefu wa washukiwa kabla ya kesi zao nchini Senegal.
Sheria ya kanuni za adhabu haiweki ukomo juu ya muda ambao mshtakiwa anaweza kushikiliwa, wakati akisubiri kesi dhidi yake.
Baadhi wanasema kisa cha Fall kinaelezea haja ya mageuzi katika mfumo wa mahakama wa Senegal.
" Wakati mtu fulani yuko gerezani, anapaswa kuachiliwa au kushitakiwa mahakamani, vinginevyo anapaswa kuachiliwa kwa dhamana," anasema wakili Msenegal Ousmane Sèye.
Amesema kuwa baadhi ya watu wamewekwa katika mahabusu kwa muda mrefu zaidi ya muda wa hukumu ambayo wangepewa.
"Ndio maana nadhani mageuzi makubwa ya mfumo wa mahakama wa Senegal yanahiytajika."
Bw Babou anadhani mteja wake wa zamani ni muathiriwa wa mfumo mbovu.
"Yuko mahakamani na hafahamu kuhusu matokeo ya kesi hizi licha ya barua alizotuma kwa maafisa na ambazo hazijibiwi. Hapewi fursa ya kushitakiwa mahamani. Sio haki."
Kwa miaka mingi wanaharakati wa haki za binadamu wamekuwa wakikosoa magereza kwa kujaa wafungwa kupita kiasi na kutoa wilto wa njia za kupunguza hukumu.
Mafanikio yalipatikana mwaka 2020 wakati maafisa waliporuhusu kuanzishwa utaratibu wa kumuwekea mfungwa kifaa cha kielektroniki ambacho kiliwafahamisha polisi alipo kama mbadala wa gereza.
Hii itaruhusu kijfungo cha nyumbani badala ya kuwafunga mahabusu na hata kuweza kuwafuatilia baadhi ya wafungwa waliopatikana na hatia.
Bado mfumo huu haujaanza kutekelezwa, lakini serikali ilisema kuwa kituo cha ufuatiliaji wa mfumo huu kinabuniwa.