Wabrazil watumwa wa kingono: ‘Walitulazimisha tufanye mapenzi hadi mara 15 kwa siku’

mujer

Chanzo cha picha, Getty Images

Hatua zote zinafuatiliwa kwa mbali kwa njia ya simu ya rununu.

Kamera iliyofichwa kwenye chumba cha kulala na vitisho vya kutuma video za ngono kwa jamaa wa karibu vinaonekana. Pasipoti, nyaraka zao na pesa zilizochukuliwa vinaonekana.

Wamepigwa marufuku kuwasiliana na marafiki.

Utaratibu uliopo ni kuwalazimisha waathirika kushiriki ngono na wateja 15 hadi 20 kila siku.

Haya ndio yaliokuwa maisha ya kila siku ya wanawake watatu wa Brazil waliookolewa na polisi kutoka kwa kazi ya utumwa wa kingono huko North West London, katika uchunguzi tata ulioanza Machi mwaka jana.

Kesi hiyo ilimalizika mnamo Agosti 9, wakati Shana Stanley, mwanamke wa miaka 29, na Hussain Edanie, mtu wa miaka 31, walipokiri makosa ya kufanya uasherati na kuandaa safari kwa nia ya kunyanyasa wengine, ambako kulihusisha wanawake watatu wa Brazil na mwathirika mmoja wa Mwingereza.

Walihukumiwa na kufungwa jela: Edani alihukumiwa kifungo cha miaka 8 na miezi 2, na Stanley naye, kifungo cha miaka 3 na miezi 7.

Maelezo ya kesi hiyo yalipatikana na BBC News Brazil pekee na inaonyesha hatari kubwa zinazohusiana na ahadi za kirahisi rahisi tu za kusafiri na kupata udhamini au ufadhili wa masomo nje ya nchi.

"Waliniuzia ndoto ambayo iligeuka kuwa jinamizi," anasema mmoja wa Wabrazil, ambaye bado anaendelea kupona kutokana na msururu wa matukio ya unyanyasaji aliyokumbana nayo katika ulimwengu wa mji mkuu wa Uingereza.

Katika ripoti hii utambulisho wa waathirika wote ulifichwa.

"Cheti chako cha kifo"

Wabrazil hao watatu walifika England mnamo mwaka 2020, baada ya kupata "ufadhili wa masomo" wa kozi ya somo la Kiingereza ambayo ingedumu kwa wiki chache tu.

Polisi hawakutoa maelezo juu ya jinsi waathiriwa hao walivyopatikana.

Muda mfupi baada ya kuwasili, wakawa wahanga wa soko lenye faida kubwa la usafirishaji haramu wa binadamu ambalo, kulingana na UN, linaathiri watu milioni 2.5 kila mwaka na thamani yake inasemekana kuwa zaidi ya dola bilioni 30 za Kimarekani.

"Shukrani kwa ujasiri na uhodari wa waathiriwa hao, tuliweza kukusanya ushahidi usioweza kukanushwa ambao ulimwacha Edani na Stanley bila chaguo jingine lolote zaidi ya kukiri makosa yao ambayo yatazuia wengine kudhurika," anasema mpelelezi Pete Brewster, mmoja wa waliohusika na uchunguzi huo.

Hussain Ednanie y Shana Stanley

Chanzo cha picha, Policía británica

Maelezo ya picha, Hussain Ednanie na Shana Stanley walihukumiwa kwa kesi iliyohusisha Wabrazil.

Yote hayo yalianza baada ya mmoja wa Wabrazil kuomba polisi msaada mnamo mwezi Machi mwaka jana, baada ya makabiliano na mwanamke aliyehukumiwa hivi karibuni mahakama ya Uingereza.

Wakati wanapigana, mwathirika alijaribu kuita polisi, lakini alisukumwa na Stanley, ambaye wakati huo, kulingana na rekodi rasmi, alimtishia kwa kumwambia kuwa: "Ulijiwekea mwenyewe sahihi kwenye cheti chako cha kufariki dunia."

Hii ilikuwa kichocheo cha Mbrazil huyo kusisitiza juu ya kutafuta ulinzi wa polisi na kuonyesha picha za aliyeamua kumnyanyasa, na kupendekeza uchunguzi juu ya Utumwa wa kisasa na Utumiaji wa Watoto vibaya kufanywa na Timu ya Polisi wa Jiji la London.

Katika ushuhuda wake, mwathiriwa alisema kwamba muda mfupi baada ya kuanza kozi yake ya somo la Kiingereza huko Manchester, alialikwa kusafiri kwenda London kukutana na mwanamke ambaye alikuwa amezungumza naye juu ya ufadhili wake wa masomo.

Baada ya kukutana naye, alisikia kwamba atalazimika kutia saini mkataba la sivyo "hataweza kurudi Brazil ", "badala yake atalazimika kuishi mitaani London" na "hataiona familia yake tena.".

Udhibiti

Mkataba huo, kulingana na polisi, ulimtaka Mbrazili huyo "auze mwili wake."

Aliwaambia wachunguzi kwamba hakuwa na njia mbadala na kwamba alisaini hati hiyo kwa kuhofia kutoweza kurudi Brazil.

Historia hiyo ilijirudia na Wabrazil wengine, ambao pia walikuja England baada ya kuahidiwa kusoma Kiingereza, kupata malazi na tikiti zilizolipiwa.

Polícia británica

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Mmoja wa waathirika aliomba usaidizi kwa polisi.

Walihitajika kupata mapato ya $ 690 kwa siku.

Na kwa mabadilishano yake, walipokea malipo ya kila wiki ya dola za Marekani 345, pamoja na dola 70 za Kimarekani kwa ajili ya chakula.

Ili kufikia bei ya juu iliyoainishwa na wanyanyasaji, mara nyingi wanawake hao walilazimika kukutana na wateja 15 hadi 20 kwa siku moja, kulingana na polisi.

Kiasi kilichotwaliwa na wenzi hao kingetumika, kulingana na wao, kulipia gharama za kusafiri ambazo wasichana waliamini kuwa wamepata bure.

Katika vyumba vya kulala, kila kitu kilipigwa picha na kamera zilizodhibitiwa na wenzi hao.

Waliwaambia waathirika kuwa watatuma picha hizo kwa familia zao "ikiwa hawatafanya kile walichoombwa."

Kiwango cha udhibiti wa wanawake hao wa Brazil kilikwenda mbali zaidi.

Wanawake hao wachanga walipokea simu za rununu kutoka kazini, ambazo walipata habari juu ya ratiba za wateja kupitia mtandao wa WhatsApp na nyendo zao zote zilifuatiliwa kwa GPS.

Kwa muda, walilazimishwa kuongozana na mtu mwingine wakati wanaenda kufanya kozi yao ya Kiingereza, lakini muda si muda walilazimika kuachana na masomo.

Sheria

Chini ya sheria ya Uingereza, ukahaba au kutoa huduma za ngono kwa ajili ya pesa ni shughuli ya kisheria.

Kwa upande mwingine, utekelezaji wa ukahaba - kupitia takwimu maarufu kama 'pimps' - na uwepo wa madanguro ni marufuku katika eneo lolote lile.

Polisi wa London walisema "wanachukua ripoti zote za utumwa wa kisasa kwa uzito mkubwa sana na wamejitolea kuwashtaki wale ambao wanahusika katika uhalifu huu mbaya.

Walisema pia kwamba "wanahimiza mtu yeyote ambaye amepata uhalifu kama huo kuripoti" na kwamba malalamiko yao "yatashughulikiwa kama suala unyeti" na kufanyika kwa "uchunguzwa wa kina kwa uangalifu."

Mujer

Chanzo cha picha, Getty Images

Namna wenzi walivyopatikana na hatia

Mnamo mwezi Aprili 2020, mwezi uliofuata malalamiko ya Mbrazili, polisi wa London walitoa hati za kufanya msako dhidi ya anwani za wenzi hao waliowaleta Wabrazil na kupata simu za rununu, nyaraka, orodha za bei na masanduku ya kondomu.

Maelfu ya pauni ziligunduliwa katika amana za pesa kwenye akaunti za benki za wenzi hao.

Ilikuwa baada ya upekuzi huu ndipo wachunguzi waliweza kumtambua mwathirika Mwingereza, mwanamke ambaye alisema alitafutwa na maajenti wanaoshughulika na wanamitindo.

Baada ya kupokea zawadi na kulipwa gharama zote na wenzi hao, walimlazimisha "alipe deni " na akawa hana budi zaidi ya kukubali kufanya kazi ya ukahaba.

"Edani na Stanley waliwashawishi waathirika na ahadi za uwongo za kuwadanganya na kuwatumia kwa faida zao za kibinafsi za kifedha. Hawakuwa na heshima kabisa kwa waathiriwa au hata kujali ustawi wao, kiasi cha hata kuwalazimisha kufanya kazi kwa saa nyingi kuliko walivyokubaliana kwa malipo kidogo sana, hata wakati hawakuwa wanahisi vizuri," anasema mpelelezi Brewster.

"Kitu pekee kilichokuwa muhimu kwao kilikuwa ni pesa ngapi wangeweza kupata."