Ubakaji wa ndoa:Sio hatia kwa mwanamume kumbaka mkewe India -Lakini kwanini iwe hivi?

Muda wa kusoma: Dakika 4

Nchini India, jamii iliyojikita katika mila za mfumo dume, ndoa ni takatifu na sio kosa kwa mwanamume kumbaka mkewe.

Lakini katika wiki za hivi karibuni, korti zimetoa maamuzi yanayokinzana juu ya ubakaji wa ndoa, na kusababisha wito mpya kutoka kwa wanaharakati kutaka kuharamishwa kwa ubakaji ndani ya ndoa.

Siku ya Alhamisi, Jaji NK Chandravanshi wa mahakama kuu ya Chhattisgarh aliamua kwamba "kujamiiana au tendo lolote la ngono la mume na mkewe haliwezi kuwa ubakaji hata ikiwa ni kwa nguvu au dhidi ya matakwa yake".

Mwanamke huyo alikuwa amemshtumu mumewe kwa "ngono isiyo ya kawaida" na kumbaka akitumia vitu.

Jaji alisema mtu huyo anaweza kushtakiwa kwa ngono isiyo ya kawaida lakini akamwondolea kosa kubwa zaidi la ubakaji kwani sheria ya India haitambui ubakaji wa ndoa.

Uamuzi huo ulizua hasira kwenye mitandao ya kijamii ikiwemo kutoka kwa mtafiti wa jinsia Kota Neelima ambaye aliuliza "ni lini mahakama zitazingatia kusikiza kisa cha upande wa mwanamke?"

Wengi walijibu ujumbe wake katika twitter wakisema sheria za zamani za ubakaji lazima zibadilishwe - lakini kulikuwa na maoni kinzani pia

Mtu mmoja alijiuliza "ni aina gani ya mke atalalamika juu ya ubakaji wa ndoa?"; mwingine alipendekeza "lazima kuwe na kitu kibaya na tabia yake"; wakati wa tatu alisema "ni mke tu ambaye haelewi majukumu yake ndiye angefanya dai kama hilo".

Sio tu mitandao ya kijamii, suala la ubakaji wa ndoa pia linaonekana kuwa limegawanya idara mahakama.

Wiki chache tu nyuma, mahakama kuu katika jimbo la kusini la Kerala iliamua kwamba ubakaji wa ndoa ulikuwa "msingi mzuri" wa kuitisha talaka.

"Tabia mbaya ya mume kupuuza uhuru wa mke ni ubakaji wa ndoa, ingawa tabia kama hiyo haiwezi kuadhibiwa, iko katika sura ya ukatili wa mwili na akili," Majaji A Muhamed Mustaque na Kauser Edappagath walisema katika agizo lao la 6 Agosti.

Walielezea kuwa ubakaji wa ndoa ulitokea wakati mume aliamini kuwa anamiliki mwili wa mkewe na kuongeza kuwa "dhana kama hiyo haina nafasi katika sheria za kisasa za kijamii".

Sheria ambayo Jaji Chandravanshi aliitaja ni Sehemu ya 375 ya Kanuni ya Adhabu ya India.

Sheria ya enzi za ukoloni wa Uingereza, ambayo imekuwa ikitumiwa India tangu 1860, inataja "misamaha" kadhaa - hali ambazo ngono haitajwi kama ubakaji - na moja wapo ni "na mtu aliye na mkewe mwenyewe" ambaye sio mtoto.

Wazo hilo limetokana na imani kwamba idhini ya ngono "inatolewa moja ka moja " katika ndoa na kwamba mke hawezi kuiondoa baadaye.

Lakini imezidi kupingwa kote ulimwenguni na kwa miaka mingi, zaidi ya nchi 100 zimepiga marufuku ubakaji wa ndoa. Uingereza pia iliipiga marufuku mnamo 1991, ikisema "idhini ya kukubai" haiwezi "kutudumishwa sana" siku hizi.

Lakini licha ya kampeni ndefu ya kuharamisha ubakaji wa ndoa , India inabaki kati ya nchi 36 ambazo sheria hiyo zinatumika ikiacha mamilioni ya wanawake wakiwa wamenaswa katika ndoa zenye ghasia .

Kulingana na utafiti wa serikali, 31% ya wanawake walioolewa - karibu mmoja kati ya watatu - wamekabiliwa na unyanyasaji wa kimwili, kingono na kihisia kutoka kwa waume zao.

"Kwa maoni yangu," anasema Profesa Upendra Baxi, profesa wa sheria katika Chuo Kikuu cha Warwick na Delhi, "sheria hii lazima iondolewe."

Kwa miaka mingi, anasema, India imepiga hatua katika kushughulikia unyanyasaji dhidi ya wanawake kwa kuleta sheria dhidi ya unyanyasaji wa nyumbani na unyanyasaji wa kijinsia, lakini haijafanya chochote juu ya ubakaji wa ndoa.

Katika miaka ya 1980, Prof Baxi alikuwa sehemu ya kundi la mawakili mashuhuri ambao walikuwa wametoa mapendekezo kadhaa juu ya kurekebisha sheria za ubakaji kwa kamati ya bunge.

"Walikubali maoni yetu yote isipokuwa ile ya kukataza ubakaji wa ndoa," aliiambia BBC.

Jaribio lao la baadaye la kufanya mamlaka kupiga marufuku ubakaji wa ndoa pia haikufanikiwa.

"Tuliambiwa wakati haukuwa sawa," Prof Baxi alisema. "Lakini lazima kuwe na usawa katika ndoa na upande mmoja hauwezi kuruhusiwa kutawala mwingine. Huwezi kudai ngono kutoka kwa mwenzi wako."

Serikali imekuwa ikisema kuharamisha ubakaji wa ndoa "unaweza kudhoofisha" taasisi ya ndoa na kwamba inaweza kutumiwa na wanawake kuwanyanyasa wanaume.

Lakini katika miaka ya hivi karibuni, wake na mawakili ambao hawajapendezwa na sheria hiyo wamekuwa wakienda kortini wakitaka "sheria hiyo dhalilishi" ipigwe marufuku.

Umoja wa Mataifa, Human Rights Watch na Amnesty International pia wameelezea wasiwasi wao kuhusu India kukataa kufanya hivyo.

Majaji wengi pia wamekiri kwamba wanasumbuliwa na sheria hiyo ya zamani ambayo haina nafasi katika jamii ya kisasa na walitaka bunge kuharamisha ubakaji wa ndoa.

Sheria hii ni "ukiukaji wazi" wa haki za wanawake, na kinga inayowapa wanaume ni "isiyo ya kawaida" na sababu kuu ya kuongezeka kwa kesi za korti, Bi Neelima anasema.

"India ina sura ya kuwa ya kisasa sana, lakini kwaruza juu kidogo na unaona sura halisi. Mwanamke hubaki kuwa mali ya mumewe. Ubakaji ni uhalifu nchini India sio kwa sababu ya mwanamke kukiukwa, lakini kwa sababu yeye ni mali ya mwanaume mwingine. "

Bi Neelima anasema "nusu ya India ambayo ni ya kiume ilipata uhuru wakati India ikawa nchi huru mnamo 1947, nyingine - ya kike - nusu bado haijawa huru. Tumaini letu liko katika mahakama".

Inatia moyo kwamba korti zingine "zimekiri kutokuwa kawaida kwa kinga hii", anasema. Lakini haya ni "mafanikio madogo, yaliyotawaliwa na hukumu zingine za kisheria".

"Hii inahitaji uingiliaji kati, na lazima ibadilike katika maisha yetu. Vizuizi ni virefu zaidi linapokuja suala la ubakaji wa ndoa," anasema.

"Hii inapaswa kuwa imetatuliwa. Hatupiganii vizazi vijavyo, bado tunapambana na makosa ya kihistoria. Na vita hivi ni muhimu."