Algeria: Moto wa msituni uliosababisha kifo cha msanii

Mwandishi wa BBC Kayleen Devlin anasimulia hadithi ya kutisha ya jinsi maisha ya msanii mchanga ambaye alikuja kusaidia kupambana na moto wa misitu nchini Algeria yalivyokatizwa na watu.

Mnamo tarehe 9 Agosti, Algeria ilikumbana na moto mbaya zaidi katika historia ya nchi hiyo: baadhi ya moto 71 ilienea katika majimbo 18, na kuwaka kwa siku tatu.

Angalau watu 90 waliuawa huku wengine wengi wakijeruhiwa.

Eneo la Kabylie, mashariki mwa mji mkuu Algiers, ndilo lililoathiriwa zaidi.

Picha nyingi na video zimeibuka kwenye mitandao ya kijamii zikionyesha nyumba zilizojengwa maeneo ya kilima zikiwaka moto.

Wanakijiji waliokata tamaa walionekana wakitoroka nyumba zao na kujaribu kuzima moto kwa mafagio ya muda, matawi, na ndoo za maji.

Siku mbili baada ya moto kuzuka, msanii Djamel Ben Ismail aliweka ujumbe kwenye mtandao wa Twitter akisema atasafiri zaidi ya maili 200 (322km) kutoka nyumbani kwake Miliana "kusaidia marafiki zetu " kukabiliana na moto.

Kwenye ukurasa wake wa Facebook, aliandika tena wito wa kukata tamaa wa msaada wa haraka.

Alielezewa kama "msanii, kijana anayependa gita na maisha yake ... sio mtu mwenye vurugu" na mmoja wa marafiki zake.

Hata hivyo, alipofika mkoa wa Tizi Ouzou wa Algeria, eneo la Kabilye, maisha ya msanii huyo yalikatizwa ghafl

Mnamo Agosti 11, picha za kutisha zilianza kusambazwa zikionyesha Bw. Ben Ismail akishambuliwa.

Alishukiwa kwa madai ya uwongo ya kuanzisha moto, na wenyeji walimtesa na kumteketeza moto kabla ya kuchukua mwili wake na kuupeleka kwenye uwanja wa kijiji.

Video hizo mara moja zilisababisha hasira ya kitaifa.

Kaka ya msanii huyo baadaye aliwahimiza watumiaji wa mitandao ya kijamii kufuta picha za shambulio hilo.

Mama yake, alisema, bado hajaelewa ilivyotokea hadi mtoto wake akafariki dunia.

Baba wa Bw. Ben Ismail alisema "mevunjika moyo ".

"Mwanangu aliondoka hapa kwenda kusaidia ndugu zake kutoka Kabyle, mkoa anaopenda sana. Walimchoma amoto kiwa hai," alisema.

Kulingana na ripoti zingine za vyombo vya habari vya eneo, machafuko na uvumi vilienea katika maeneo yote ya Tizi Ouzou, na wakaazi wengine wakaanza kushuku watu wanaoendesha magari yenye nambari za usajili ya mikoa mingine.

Hofu hii na wasiwasi inadaiwa kusababishwa na tuhuma za kumchoma moto mvulana huyo.

Jioni kabla ya kifo cha Bw. Ben Ismail, Waziri Mkuu Aymen Benabderrahmane alisema moto huo ulitokana na "kitendo cha jinai ".

Katika hotuba iliyotolewa kwa njia ya televisheni, aliongeza: "Uchunguzi wa awali huko Tizi Ouzou umethibitisha kuwa chanzo cha moto huu zilichaguliwa kwa uangalifu kusababisha hasara kubwa zaidi.

Siku hiyo hiyo, Waziri wa Mambo ya Ndani Kamel Beldjoud alimtembelea Tizi Ouzou, akiwaambia wanahabari kuwa moto huo umesababishwa na "wahalifu waliojaa chuki dhidi ya nchi yetu."

Kulingana na BBC Monitoring, hakuna maafisa wala vyombo vikuu vya habari nchini humo vilivyotaja mabadiliko ya hali ya hewa kama sababu ya moto, au kama sababu ya kuenea kwake.

Hii ni licha ya ukweli kwamba joto la hadi nyuzi 46 za selsiasi (115F) lilitabiriwa kwa wiki ambayo moto ulitokea.

Pia kuhusu wakati huo, ripoti kuu ya kisayansi ya UN ilionya juu ya joto kali linalozidi kuongezeka, ukame, na mafuriko ulimwenguni.

Kufuatia kifo cha Bw. Ben Ismail, hasira ya umma imechochewa na pia visasi bya matukio ya kisiasakumejitokeza.

Watumiaji wengine wa mitandao ya kijamii walisambaza picha za watu wanaodaiwa kuwa wauaji, wakijaribu kuwatambua, na wengine wengi wakijitokeza kwenye hashtag ya kudai haki itendeke.

Kufikia sasa, watu 61 wamekamatwa baada ya kifo cha msanii huyo, huku kidole cha lawama kikielekezwa kwa wanachama wa kundi la vuguvugu la Movement for the Self-Determination of Kabylie (MAK).

Vuguvugu hilo lilitangazwa kuwa shirika la kigaidi na mamlaka ya Algeria mnamo mwezi Mei.

Mnamo Agosti 17, Televisheni inayomilikiwa na serikali ilitangaza "kukiri" kutekeleza mauaji kwa wanaoshukiwa kuwa wanchama wa vuguvugu la MAK, ingawa uchunguzi bado unaendelea.