Vita vya Afghanistan: Je rais wa taifa hilo, Ashraf Ghani ametorokea wapi?

Chanzo cha picha, Getty Images
Kundi la Taliban limetangaza kushinda vita Afghanistan baada ya kuudhibiti mji mkuu wa nchi hiyo , Kabul, na kuhitimisha karibu miongo miwili ya vita.
Wapiganaji wa kundi hilo walidhibiti pia makazi ya Rais. Serikali ya Afghanistan imevunjika baada ya Rais Ashraf Ghani kukimbia.
Msemaji wa Taliban ameiambia Al Jazeera: "Mapigano yameisha."
Kabul imekuwa kama kitovu cha ghasia, wakati huu wakazi na wageni wakijaribu kukimbia eneo hilo.
Wafanyakazi katika uwanja wa ndege wa kimataifa walikimbia na kuacha ofisi zao, wakati mamia ya watu wakikimbilia ndege, mtu mmoja aliyeshuhudia ameiambia BBC.
Kabul ulikuwa mji wa mwisho uliosalia nchini Afghanistan ambao haukuwa chini ya udhibiti wa Taliban. Baada ya miezi kadhaa ya mapigano, wanajeshi wa kundi hilo wamefanikiwa kudhibiti eneo kubwa la nchi hiyo na kusababisha hofu sio tu Afghanistan hata nje ya mipaka ya nchi hiyo.
Taliban wamefanikiwa kudhibiti maeneo mengi kufuatia vikosi vya kigeni vilivyokuwemo nchini humo kuondoka.
Rais Ashraf Ghani akimbia

Chanzo cha picha, Getty Images
Al-Jazeera, baadae iliripoti kwamba Ghani, mkewe, mkuu wa majeshi na washauri wake wa karibu wamekimbilia Tashkent, mji mkuu wa Uzbekistan.
Taarifa imetoka kwa mmoja wa walinzi wake, lakini hakuna taarifa rasmi ya nchi gani rais huyo amekwenda, na serikali yake haijazungumza lolote
Rais Ghan alituma ujumbe muda mfupi kabla ya kuondoka Kabul akionya kuwa kama vita vitaibuka mamilioni ya maisha ya watu yatakuwa hatarini.
Katika ujumbe huo kwenye mtandao wake wa Facebook Ghani alisema ameamua kuchukua uamuzi wa kuondoka bila kumwaga damu.
Alisema: "Leo napaswa kufanya maamuzi magumu, ambayo ni kupambana na Taliban wanaoutaka urais au kuokoa nchi yangu ninayoipenda - ambayo nimeilinda kwa miaka 20 iliyopita. "Naondoka sasa."
Hali ikoje sasa?

Chanzo cha picha, AFP
Kumekuwa na msongamano mkubwa wa watu na magari katika barabara kuu ya kuingia mji mkuu wa Afghanistan. Watu wanajaribu kutumia barabara hiyo kuondoka katika jiji hilo.
Hofu ni kubwa katika jiji hilo huku mataifa mbalimbali yakijaribu pia kuwaondoa raia wake.
Makamu wa Rais Amrullah Saleh naye ameondoka nchini humo, kwa mujibu wa taarifa.
Farzana Elham, mbunge kutoka Kabul, ameiambia BBC kwamba raia kadhaa wamekuwa wakijaribu kukimbia nchi hiyo ama kujificha majumbani mwao.
Wanajeshi wa zamani nchini Afghanistan wameonyesha wasiwawasi wao kwamba nchi hiyo sasa inaingia mikononi mwa "maadui" ambao wamekuwa wakikabiliana nao kwa miaka zaidi ya 20.

Chanzo cha picha, Getty Images
Marekani inapeleka zaidi ya wanajeshi 6,000 kusaidia watu kuondoka Kabul, kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa mmoja wa maafisa wa Jeshi la nchi hilo.
Mapema wiki hii, Marekani ilipeleka vikosi vya wanajeshi 3,000 nchini Afghanistan kuokoa raia wake walioko nchini humo.
Mpaka sasa jumla ya wanajeshi 6,000 wa Marekani wamepelekwa Afghanistan. Mwaka 2001, nchi hiyo ilipeleka vikosi vya wanajeshi 110,000.

Chanzo cha picha, AFP
Umoja wa Mataifa umesema nini kuhusu mzozo huu?
Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amelitaka kundi hilo la Taliban na wanamgambo wake kuhakikisha hali inakuwa ya utulivu nchini humo ili kuokoa maisha ya raia.
Katika taarifa rasmi iliyotolewa na msemaji wake, Gutteres ilisema haki za binadamu na uhuru wa watu lazima zizingatiwe.
Katibu mkuu huyo alionyesha hasa wasiwasi wake kuhusu haki za wanawake akisema lazima haki zao zilindwe.














