Mgogoro wa Afghan: Rais na makamu wa rais wa Afghanistan waondoka nchini kwao baada ya Taliban kudhibiti miji yote mikuu

Chanzo cha picha, Getty Images
Rais Ashraf Ghani ameondoka nchini kwake, taarifa zinasema zimenukuu maofisa wa Afghanistan.
Taarifa ya kuondoka kwake imekuja mara baada ya Taliban ilivyofikia katika pembezoni mwa Kabul.
Makamu wa rais Amrullah Saleh naye aripotiwa kuondoka.
Taarifa za Bwana Ghani kuondoka zimekuja wakati ambao kumekuwa na mvutano mkubwa wa miji yote mikuu ya Afghanistan kudhibitiwa na wanamgambo wa Taliban.
Ofisi ya rais imeiambia Reuters kuwa "hawawezi kusema lolote kuhusu kuondoka kwa rais Ashraf Ghani kwasababu za kiusalama".

Wakati huohuo msemaji wa Taliban ameiambia BBC "hakutakuwa na visasi kwa watu wa Afghanistan.
Suhail Shaheen amewaakikishia wananchi kuwa ;"Tunawahakikishia raia wa Afghanistan, haswa wa mji wa Kabul, kuwa mali zao na maisha yao yatakuwa salama - hakuna atakayelipa kisasi kwa yeyote.
"sisi ni watumishi wa watu wa taifa hili."
Raia wengi wa Afghans wanahofia kurejea kwa ukatili uliofanyika mwaka 1990, ambapo watu waliuawa, walipigwa mawe na wasichana walipigwa marufuku kwenda shule.

Wanamgambo wa Taliban wamekaribia kuithibiti nchi nzima ya Afghanistan, huku mji mkuu wa nchi hiyo Kabul ukiwa umedhibitiwa pia na serikali.
Mapema leo Jumapili wanamgambo hao wameinyakua Jalalabad, bila mapigano. Jiji hilo lipo Mashariki mwa nchi.
Hatua hiyo ilifuatia kudhibitiwa kwa kwa mji muhimu wa shughuli za kiseriali wa Mazar-i-Sharif uliopo kaskazini hapo jana Jumamosi.
Kuzidiwa haraka kwa vikosi vya majeshi ya serikali kumemuweka Rais Ashraf Ghani katika shunikizo kubwa la kujiuzulu.
Rais Ghani anaonekana yupo njia panda katika kuamua la kufanya kati ya kujisalimisha au kuendeleza mapambano ya kudhibiti makao makuu ya nchi, Kabul.

Chanzo cha picha, Getty Images
Wakati huohuo, Marekani imeanza kuwaondoa wafanyakazi wake wa ubalozi jijini Kabul. Jumapili asubuhi wafanyakazi hao wamepelekwa uwanja wa ndege ambako wameonekana wakipanda ndege sita kubwa za kijeshi. Marekani imepeleka wanajeshi 5,000 kusaidia operesheni hiyo.
Rais Joe Biden ametetea uamuzi wa kuongeza kasi ya Marekani kuondoka Afghanistan, akisema hawezi kuhalalisha uwepo wa Marekani Afghanistan bila kikomo huku nchi hiyo ikikabiliwa na mgogoro mkubwa wa ndani.
Nini kilitokea Jalalabad?

Chanzo cha picha, EPA
Taarifa za Jumapili asubuhi zilisema wanamgambo wa Taliban walidhibiti jiji hilo ambalo ni makao makuu ya jimbo la Nangarhar, bila kusikika milio ya risasi.
"Hakuna mapigano yoyote yanayoendelea Jalalabad kwa sasa kwa sababu gavana amesalimu amri kwa Taliban," afisa mmoja aliliambia shirika la habari la Reuters.
"Kuwaruhusu Talibani ilikuwa ndiyo njia pekee ya kuyanusuru maisha ya raia."
Mwandishi wa habari Tariq Ghazniwal amechapisha kwenye akaunti yake ya mtandao wa twitter picha zinazodaiwa kuonesha gavana wa jimbo akikabidhi mamlaka kwa Taliban.
Kunyakuliwa kwa Jalalabad kunaamanisha kwamba Taliban wamefanikiwa kudhibiti barabara zinazounganisha Afghanistan na Pakistan.
Hayo yalitokea saa chache baada ya mji wa Mazar-i-Sharif - makao makuu ya jimbo la Balkh na jiji la nne kwa ukubwa nchini Afghanistan - kutekwa bila mapigano yoyote.
Abas Ebrahimzada, mbunge kutoka Balkh, ameliambai shirika la habari la Associated Press kuwa jeshi la taifa lilikuwa la kwanza kujisalimisha, hali iliyosababisha vikosi vingine vinavyoiunga mkono serikali na wanamgambo wengine kusalim amri.
Sasa wanamgambo wa Taliban wanadhibiti makao makuu ya majimbo 23 kati majimbo 34 ya Afghanistan.

Kimetokea nini Kabul?
Zaidi ya watu laki tano wameyakimbia makazi yao kutokana na mapigano na wengi wamekimbilia Kabul.
Baadhi yao waliokuwa wameyakimbia maeneo yanayodhibitiwa na Taliban wamesema wanamgambo hao walikuwa wakizitaka familia kukabidhi kwao wasichana na wanawake ambao hawajaolewa ili wawe wake wa wapiganaji.
Muzhda, 35, mwanamke ambaye hajaolewa na alikimbilia Kabul kutoka Parwan akiwa na dada zake wawili, amesema anaweza kujiua badala ya kulazimishwa kuolewa na Taliban.
"Nalia usiku na mchana," aliliambia shirika la habari la AFP.
Wanawake kutoka maeneo yanayodhitiwa na Taliban wamedai pia kuwa wanalazimishwa kuvaa burka - vazi linalofunika mwili mzima hadi sura - na wanamgambo wanaripotiwa kuwapiga watu kwa tuhuma za kukiuka sheria za kijamiii.

Chanzo cha picha, EPA
"Mungu epusha ,tutaona vita huko Kabul," mkazi wa mjini Sayed Akbar, 53, aliiambia New York Times. "Watu hapa wamepitia miaka 40 ya mateso. Barabara ambayo tunaitembelea imejengwa juu ya mifupa ya watu."
Kijana mmoja mwenye miaka 17-, kwa jina Abdullah, ameiambia AFP kuwa familia yake ilikimbilia kaskazini mwa mji wa Kunduz baada ya mji wao kudhibitiwa na Taliban na sasa wanalala kwenye maturubai huko Kabul .
Alisema yeye na vijana wenzie wa Kunduz wamekuwa wakilazimishwa kubeba mabomu ya wanajeshi.

Chanzo cha picha, AFP
Wakazi wa Kabul wamekuwa katika foleni ndefu kwenye benki wakitoa akiba zao.Baadhi ya benki yameripotiwa kuishiwa fedha.
Kulikuwa na ghasia kwenye gereza la Pul-e-Charkhi ambalo liko pembezoni mwa mji mkuu , wakazi wa eneo hilo wanasema walisikia milio ya risasi kutoka kwenye gereza hilo.
Katika mahojiano ya TV , siku ya Jumamosi , rais Ashraf Ghani alisema kipaumbele chao ni kuwarejesha askari wa Afghan ili kuzuia uharibifu zaidi na watu kukimbia makazi yao.
Tamko hilo limetolewa huku kukiwa na tetesi kuwa bwana Ghani inawezekana anataka kujiuzulu.














