Freeman Mbowe: Bingwa wa mikakati ya siasa za upinzani anayewanyima usingizi watawala

chadema

Katika mfululizo wa Makala ya wiki hii tunawaangazia wanasiasa ambao wamekuwa mwiba kwa serikali zilizopo madarakani katika eneo la Afrika mashariki na jinsi wanavyoziwajibisha serikali hizo.

Baadhi ya wanasiasa ni maafisa wa serikali wanaopigana dhidi ya serikali hizo kutoka ndani.

bb

Freeman Aikaeli Mbowe ni mfanyabiashara na mwanasiasa anayekiongoza chama kikuu cha upinzani nchini humo CHADEMA. Kwa sasa anashikiliwa na dola akikabiliwa mahakamani na kesi ya ugaidi.

Katika uongozi wake ameonekana kuwa kiongozi mbunifu, anayeamini vijana, asiye mhafidhina wa kisera na mwenye uwezo wa kufanya kazi na yeyote kwa maslahi ya chama chake.

Alizaliwa Septemba 14 mwaka 1961, mwaka ambao Tanganyika ilipata uhuru wake, na jina lake linaelezwa kuakisi hilo.

Pengine kwa sababu ya kuzaliwa mwaka wa uhuru wa Tanganyika, ambayo baadaye mwaka 1964 ikaungana na Zanzibar na kupatikana Tanzania, imemfanya kuwa mpambanaji wa kipinzani, anayeamini bado Tanzania inahitaji uhuru zaidi wa fikra, baada ya ule wa bendera.

Kujiingiza kwenye siasa

Kabla ya kuwa mwanasiasa, Mbowe alikuwa anashughulika na mambo mengi binafsi ikiwemo Dj, mfanyabiashara wa kawaida na baadae kufanya kazi Benki kuu ya Tanzania kama Afisa wa Benki Kuu (BoT) akiwa chini ya Edwin Mtei na Bob Makani.

Katika harakati za kisiasa, Freeman Aikael Mbowe aliingia rasmi katika siasa mwaka 1992, akiwa miongoni mwa waasisi wa chama cha CHADEMA kilichosajiliwa kwa usajili wa kudumu mwaka 1993 chini ya sheria ya vyama vya siasa namba 5 ya mwaka 1992.

N

Chanzo cha picha, Google

Maelezo ya picha, Mbowe amekuwa na ushawishi mkubwa miongoni mwa vijana

Katika kundi la waasisi wa chama hicho, Mbowe ndiye aliyekuwa kijana mdogo zaidi, lakini aliaminika na watu ambao angalau walianza kuonesha uzoefu wao kwenye ulingo wa siasa za kawaida na wenye harakati za kuleta fikra tofauti. Miongoni mwao ni Edwin Mtei na Bob Makani, Mary Kabongo na Evarist Maembe.

Mwaka 1995, kwenye uchaguzi mkuu wa kwanza wa Demokrasia, aligombea ubunge kwa mara ya kwanza katika jimbo la Hai, Kilimanjaro na kushindwa mbele ya mgombea wa NCCR MAGEUZI Mwanahamisi Mushi aliyepata kura 29,046 (52.0%) wakati Freeman Mbowe akiambulia kura 15,995(28.6%).

Hakukata tamaa, akarejea mwaka 2000, na kushinda kwa kishindo kwa kupata asilimia 64.5%, ushindi ambao ulikuwa wa kwanza kwa idadi nyingi ya kura kwa mgombea wa upinzani. Kuanzia hapo alianza kujijenga kisiasa na kuwa na nguvu ndani ya chama, kabla ya mwaka 2004 kugombea uenyekiti na kushinda akirithi mikoba ya Bob Makani aliyeongoza chama hicho kuanzia mwaka 1999.

Nguvu yake ya ushawishi ndani na nje ya chama

Wako viongozi wengi wa kisiasa nchini Tanzania waliokaa kwenye ulingo wa kisiasa kwa muda mrefu, lakini Mbowe ni miongoni mwa wanasiasa wachache sana nchini humo hasa kutoka upizani aliyedumu na nguvu zake za kisiasa kwa muda mrefu.

Umaarufu wake, jina lake na nguvu zake kisiasa zimedumu kwa zaidi ya miaka 20 akiongoza siasa za upinzani akiwa mwenyekiti wa CHADEMA na mbunge wa jimbo la Hai mkoani Kilimanjaro.

Kuwa kwake kiongozi wa upinzani nchini humo chini ya utawala wa marais wanne tofauti kutoka chama tawala cha CCM, kumemfanya kuwa na nguvu, ushawishi na kukubalika kwake kisiasa.

Kwa sababu ya uongozi wake, Mwaka 2015, chama chake kilivuna wanachama wengi pengine kuliko wakati mwingine wowote, na kupata matokeo mazuri kwenye uchaguzi mkuu uliofanyika mwaka huo. CHADEMA kilizoa viti 73, ikiwa ni viti 25 zaidi kulinganisha na uchaguzi uliopita.

Ushawishi wake, ulikiwezesha chama chake kuungwa mkono na wanasiasa wenye majina kutoka chama tawala, kwa mfano mawaziri wakuu wa zamani, kwa mfano Edward Lowassa, aliyegombea urais na kushika nafasi ya pili kwa kupata kura zaidi ya milioni 6, ambazo ni rekodi, hakuna chama cha upinzani kilichowahi kufikisha idadi ya kura hizo.

Fredrick Sumaye, waziri mkuu aliyeongoza kwa miaka 10, chini ya utawala wa awamu ya tatu wa Rais Benjamini Mkapa, alikuwa miongoni mwa waliojiunga na CHADEMA, kwa ushawishi na nguvu ya Mbowe.

Magu

Chanzo cha picha, Hakipensheni

Maelezo ya picha, Mbowe (kulia) akiwa na aliyekuwa rais wa awamu ya nne wa Tanzania, John Magufuli

Mbali na hao, ambao baada ya uchaguzi wa mwaka huo wakarejea chama tawala,CCM, walikuwepo mawaziri waliopita, wabunge, vijana, wasomi na watu wenye majina, ambao haikuwa rahisi kipindi cha nyuma kuamini kwamba wangeweza kuwa sehemu ya upinzani.

Kwa nguvu zake, Mbowe anaonekana kama ndiye CHADEMA, wengi wanawasiwasi na anachopitia sasa na hitimisho la safari yake kama mwenyekiti wa chama hicho mwaka 2023, huenda kukakitikisa chama hicho. Ingawa kumekuwa na upinzani, wafuasi wa chama chake wakimtaka aendelee, haifahamiki kama atakubaliana nao ama la.

Bingwa wa mikakati ya kisiasa ya kipinzani inayotikisa watawala

Akiwa mmoja wa waasisi wa CHADEMA mwaka 1992, Mbowe anafahamika kama mtu mahiri kwenye kupanga mikakati ya kisiasa inayomfanya kuwa mmoja wa wanasiasa wenye nguvu za kisiasa za muda mrefu nchini humo.

Amekuwa akibuni yeye na chama chake kila aina ya mbinu ya kusaidia kukitangaza chama hicho katika sehemu mbalimbali za Tanzania.

Katika uongozi wake CHADEMA ilianza kutumia helikopta katika kampeni zake mbalimbali za uchaguzi ili kutumia muda mfupi kuwafikia Watanzania katika maeneo ambako barabara zilikuwa taabu.

Ilikuwa ngumu zamani kuona jukwaa la wanasiasa wa upinzani likikimbiliwa na wanasiasa na wasio wanasiasa hasa wasomi, lakini Mbowe amefanya hilo kuonekana kuwa jambo la kawaida. Kwa sasa mikutano ya CHADEMA inahudhuriwa hata na watu wa vyama vingine kwa sababu ya hoja za wazungumzaji, umahiri wa jukwaa, kuona helikopta na sauti nzuri kutoka kwenye majukwaa.

Lowassa

Chanzo cha picha, MUUNGWANA

Maelezo ya picha, Mbowe (Kushoto), akiwa na waziri mkuu wa zamani, Edward Lowassa, baada ya kujiunga na chama hicho na kugombea urais katika uchaguzi wa mwaka 2015

Mbowe ameruhusu pia chama chake kupokea kwa wingi wanasiasa kutoka chama tawala cha CCM, mkakati uliokisaidia chama hicho kupata wabunge wengi hasa kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2010 na mwaka 2015.

Mbowe akaleta vazi kama la kombati lililokuja kuwa mojawapo ya alama za CHADEMA. Leo ni rahisi kumtambua mwanachama wa CHADEMA kwa vazi lake zaidi, ambalo wengi wanalitumia kujitambulisha itikadi zao na wanalitumia kutamba kwa imani na muelekeo wao kisiasa.

Mbowe amekuwa mtaji wa vijana wengi wanaozungumza kwa lugha yake na uundaji wa sentensi za ushawishi zinazotofautisha uzungumzaji wa wapinzani hasa kutoka CHADEMA na wanasiasa wengine. Vijana wengi ni rahisi kuwasikia wakizungumza kama yeye, huu ni mkakati wa kukiweka chama mikononi mwa vijana.

Lakini mkakati mwingine unaotumiwa na Mbowe kupitia chama chake, ni kushirikisha wanachama wake na Watanzania wengine kila linapotokea jambo.

Misimamo yake inazikosesha usingizi Mamlaka

Wakati wote Mbowe amekuwa mstari wa mbele kwenye utekelezaji wa shughuli za chama, ikiwemo maandamano, mikutano ama matamko.

Amekuwa na misimamo isiyoyumba kwenye masuala mengi yanayohusu maslahi ya chama hicho, ama kwa mtazamo wake maslahi mapana ya watu.

''Ni haki yetu kukutana, tutahama kutoka mikutano ya hadhara na sasa tutaingia kuandamana. Tunamwambia mama Samia Suluhu, akizidi kuchelewesha jambo hili, anazidi kuleta mpasuko katika nchi hii, anavyolichelewesha anachelewesha kuwaunganisha Watanzaia, tujenge taifa moja la watu wanaopenda na kuheshimiana', alisema Mbowe katika moja ya hotuba kuhusu kuzuiwa kwa vyama vya siasa kufanya mikutano ya siasa ya hadhara.

MAHAKAMANi

Chanzo cha picha, STRINGER

Maelezo ya picha, Mbowe anakabiliwa na kesi ya ugaidi baada ya kukamatwa mapema mwezi uliopita jijini Mwanza, siku moja kabla ya mkutano wa ndani kuhusu Katiba, aliopanga kuuongoza

Msimamo wake kuhusu suala la Katiba uko wazi kabisa, akitaka nchi hiyo itunge katiba mpya akisema, katiba ya sasa ya mwaka 1977 imepitwa na wakati inahitaji mabadiliko kutokana na mabadiliko ya siasa yaliyopo tangu kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi nchini humo.

Licha ya Polisi kuzuia mikutano ya chama hicho ya kudai Katiba Mbowe aliibuka akasema;

'Kama wanataka kuwaweka ndani wanachadema kwenye hoja hii ya katiba, wapanue kwanza na magereza, kwa sababu tuko tayari wote tuwekwe ndani , na wala hatutaomba dhamana' alisema Mbowe kabla ya kulaani kitendo cha Jeshi la Polisi Mwanza, kuwakamata viongozi wa dini na wafuasi wa chama hicho.

Mbowe, aliongoza vikao vya kuwafuta uanachama viongozi wanawake 19, walioapishwa kuwa wabunge wa viti maalumu baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2020. Miongoni mwa waliofukuzwa wako vigogo waliokibeba chama hi hicho ndani na nje ya bunge, akiwemo Halima Mdee na Esther Bulaya.

Katika siasa za Tanzania, imekuwa kawaida kwa wanasiasa walioonekana kuwa wapinzani wa kweli kuhamia chama tawala,CCM. Wapo vigogo wengi wa upinzani waliorejea ama kujiunga na CCM kutoka upinzani kwa mfano mawaziri wakuu wastaafu Lowassa na Sumaye na mawaziri wa zamani Lazaro Nyalandu na Lawrence Masha.

Baadhi wengine wenye majina ni David Silinde, Joshua Nassari, Dk Godwin Mollel, Kitila Mkumbo, Mwita Waitara na Dk Vicent Mashinji, aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chadema, walirudi CCM katika katika mkakati wa kuunga mkono juhudi ulioanzishwa na CCM.

Pamoja na wimbi hilo la kuunga mkono juhudi lililoanza kushika kasi mwaka 2017 kuelekea uchaguzi mkuu wa 2020, Mbowe aliendelea kusimama kidete. Hakuunga mkono Juhudi, wala kuonyesha kutetereka kwa hatua ya wabunge wake na madiwani wake kujiuzulu na kwenda CCM na kugombea tena na wengine kushinda kupitia CCM hasa wabunge. Hilo limeendelea kuwapasua kichwa watawala.

UKAWA

Chanzo cha picha, Google

Maelezo ya picha, Mbowe akiwa pamoja na viongozi wenzake waliounda UKAWA, Prof. Lipumba wa CUF (kulia) na James Mbatia wa NCCR-Mageuzi (kushoto)

Wakati wa uchaguzi wa mwaka 2015, Mbowe aliungana na viongozi wa vyama vingine vya siasa vya upinzani kuunda Umoja wa Katiba (UKAWA), na kuachiana majimbo na kusimamisha mgombea mmoja wa Urais, Lowassa.

Kabla ya uchaguzi, aliyekuwa katibu wa chama hicho na kiongozi mwenye ushawishi mkubwa wa upinzani, Dr. Wilbrod Slaa, alijiondoa kwa kuonyesha hasira zake baada ya Mbowe kukubali Lowassa kujiunga na CHADEMA akitokea CCM na kupewa nafasi ya kugombea urais, Mbowe alisimama kidete.

UKAWA ikatikiswa pia na hatua ya Prof lipumba, aliyekuwa mwenyekiti wa CUF kujiweka kando akionesha na yeye hakuridhika na hatua ya Mbowe kumpokea Lowassa, lakini Mbowe akaendelea na msimamo huo, ambao baadae uliompa wabunge wengi zaidi kwenye bunge la nchi hiyo kuliko uchaguzi wowote uliopita.

Mbali na Misimamo hiyo, mara kadhaa amewekwa ndani, kwa kauli zake ama matendo yake, yanayoonyesha fikra zake zilivyo kidhani dhidi ya serikali ama chama tawala.

Ni mpenda demokrasia 'asiyeona' nyumbani kwake?

mbowe

Chanzo cha picha, Getty Images

Mbowe amedumu kwenye siasa za Tanzania kwa miaka zaidi ya 20, na amekiongoza chama hicho kwa zaidi ya miaka 15, kitendo hicho kinachukuliwa na wapinzani wake kama mtu anayeng'anga'ania madaraka.

Licha ya uchaguzi wa ndani ya chama chake kufanyika mara kadhaa , Mbowe ameonekana kama mtu asiyeng'oleka kwenye kiti hicho, na wengi waliojaribu walionekana kwa nje kama watu wanaotaka kuasi.

Masuala ya uchaguzi wa chama hicho, yalimuondoa Zitto Zuberi Kabwe na kina Kitila Mkumbo, waliodaiwa kutengeneza mkakati wa kumpinga kiongozi huyo kwenye uchaguzi.

Kwa sababu hiyo, baadhi wanamuona ni kama anapenda demokrasia na anapigania demokrasia ya nchi na kuacha kuipigania demokrasia ya ndani ya chama chake.

Hata hivyo Mbowe aliyekiongoza chama hicho toka mwaka 2014 ametangaza kuachia ngazi, mwaka 2023.