Fahamu matukio machungu yalotia doa utamu wa soka nje ya uwanja

Michuano ya Euro 2020 imekamilika mwishoni mwa wiki hii na ambapo Italia imefanikiwa kutwaa kombe hilo ikiilaza England kwa mikwaju ya penati baada ya kwenda sare ya 1-1 mpaka dakika 120 zinakatika.

Lakini michuano hii imemalizika kwa mguu wa kushoto kufuatia vitendo vya ubaguzi wa rangi wanavyofanyiwa wachezaji watatu wa England waliokosa penati katika mchezo huo.

Jadon Sancho, Bukayo Saka na Marcus Rashford walikosa penati zao na kuiwezesha Italia kutwaa kombe hilo. Kwa siku ya tatu sasa wamekuwa wakibaguliwa kwa ngozi zao, kwa sababu wote ni weusi na kutukanwa matusi ya aina yote huku wengine wakitoa mpaka vitisho vya kifo.

England hawajahi kutwaa kombe lolote katika michuano hiyo ya Euro na hii ilikuwa fainali yao ya kwanza. Lakini pia haijawahi kufika fainali yoyote wala kutwa kombe lolote kubwa tangu ifanye hivyo miaka 55 iliyopita. Kwa hiyo mchezo wa fainali dhidi ya Italia ulikuwa una maana kubwa na kuleta mhemko mkubwa wa kihisia kwa mashabiki wa England.

Lakini yapo matukio ya kutia uchungu katika soka, yaliyotokana na ama matokeo ama matukio ya kisoka na kugharimu maisha ya wanasoka,washabiki ama viongozi wa soka. Ingawa katika soka kuna kushinda, kufungwa ama kutoka sare, kwa ujumla washabiki wengi wa soka wanetamani kushinda tu na kupata furaha, matokeo yakienda tofauti wako baadhi wanaoshindwa kuvumilia na kusababisha dhahma kwa wengine hasa wachezaji ambao kwa namna moja ama nyingine wanawatafsiri kusababisha kushindwa kwao.

Haya ni matukio machache tu kukuonyesha soka lilivyo tamu, lakini chungu kwa wengine matokeo yakienda kombo.

1: Andrés Escobar

Timu ya taifa ya Colombia iliingia katika mashindano ya kombe la dunia mwaka 1994 ikiwa na matumaini ya kufika angalau robo fainali. Kwa namna ilivyoundwa na wachezaji wengi walioonekana wazuri, mashabiki wengi waliamini timu yao ilistahili kufika mbali. Lakini mambo hayakwenda kama walivyotamani na walitolewa mapema tu.

Lakini kutolewa kwao wakamtupia lawama Andrés Escobar Saldarriaga, mlinzi kitasa ambaye alikuwa anajulikana kama baba mwenye nyumba 'The Gentleman', kwa uwezo wake wa kucheza soka la uhakika.

Nini kilitokea? Katika mechi ya pili ya makundi ya Colombia dhidi ya Marekani, Escobar alijifunga akiwa katika harakati za kuzuia krosi ya kiungo wa Marekani John Harkes, mpira ukamgonga na kujaa wavuni, mechi ikaisha kwa Marekani kushinda 2-1.

Escobar aliyewahi kuzichezea klabu za Atletico Nacional na BCS Young boys, akauawa siku chache baada ya kombe la dunia kwa kupigwa risasi. Alivamiwa usiku na watu watatu waliompiga risasi sita kama mtangazaji alivyotangaza goli hilo la kujifunga mara sita.

Kama hatua ya kulaani tukio hilo na kuendelea kumuenzi mchezaji huyo. Mamlaka katika jiji la Medellin alikozaliwa zikamjengea sanamu Escobar mwaka 2002 kumpa heshima, na kila mwaka kuna siku maaalumu ya kukumbuka kifo chake ambapo mashabiki hutembelea kaburi lake na kuweka mashada ya maua.

2: Abbas Rahim Zair

Utawala wa Rais Saadam Hussen nchini Iraq uligubikwa na matukio mengi ya kughadhabisha. Katika maisha ya kawaida na kivita kama ilionekana kutoshtua wengi, lakini katika soka wengi walipata mshangao baada ya mtoto wake mmoja kuwaaadhibu wachezaji wa timu ya taifa kila wanapofungwa, ama kumuadhibu mchezaji aliyesababisha timu kufungwa ama aliyeshindwa kuisaidia timu ya taifa hilo kushinda.

Abbas Rahim alikuwa moja ya nguzo za soka la Iraq katika uhai wake. Alizaliwa Januari 25 1979, na alikuwa kiungo matata akichezea timu ya taifa ya Iraq kwenye michuano ya bara ya Asia mwaka 2000 na klabu za Al-Shorta na Al-Zawraa.

Lakini kwenye moja ya mechi za kufuzu kombe la Asia, dhidi ya Falme za Kiarabu, Abbas Rahim Zair alikuwa miongoni mwa wapiga penati kuamua timu itakayosonga mbele. Huku akisali na kuomba asikose, Zahiri aliinuka na kupiga mkwaju huo na kwa bahati mbaya alikosa.

Siku mbili baada ya timu kurejea Iraq kutoka Jordan ulikopigwa mchezo huo, alikamatwa akafungwa machoni na kitambaa na kuwekwa jela kwa wiki tatu kwa wito wa Uday Hussein, mtoto mkubwa wa Rais Sadam Hussein

Wakati huo, kuchezea timu ya taifa ilihitaji moyo sana, na linapofika kwenye kupiga penati hakuna aliyetaka kufanya hivyo. Katika mchezo ambao Zahir alikosa penati, ni wachezjai watatu tu ndio waliokubali jukumu la kupiga penati, wengine wote waligoma kwa hofu kwamba wakikosa, watakutwa na dhahma.

"Wengi wa wachezji waligoma hata kuugusa tu mpira, lakini tuligundua pia kwamba kama kila mtu atagoma kupiga penati, maana yake, sote tutapata dhabu kali," alisema kiungo huyo.

3: William Tesillo

Kama kuna mchezaji alikuwa katika wakati mgumu mwaka 2019 ni William Tesillo, alikosa penati katika mchezo wa robo fainali ya michuano ya Copa America dhidi ya Chile na kusababisha Colombia kutolewa.

Hakulala, alilazimika kujificha na kuishi kwa mashaka kwa majuma kadhaa, kutokana na kuwindwa na mashabiki wa Colombia wakitaka kufanya kile walichokifanya mwaka 1994 kwa Andres Escobar.

Colombia ni moja ya nchi ambazo, watu wake wana kichaa cha soka, wanatamani matokeo mazuri wakati wote. Daniela Mejia, mke wa Tesillo alikuwa anatumiwa meseji na mashabiki zinazosema 'tunamtakia mumeo yale yaliyomtokea Escobar'.

"Wamemwambia kwa kumuandikia kabisa mke wangu, na mie pia," Tesillo aliliambia gazeti la El Pais kuhusu vitisho vya kuuawa kwake.

Baba yake na Tesillo alilazimika kutembea kwenye radio za nchi hiyo kumuombea msamaha mwanae na kuwataka watu waelewe kwamba mpira ni mchezo wa makosa.

"Natumaini watu wataelewa kwamba ni mpira," aliiambia Radio Caracol.

Mambo ya baba yake yalikubalika, na mpaka sasa Tesillo anayendelea kuchezea Colombia.

4: Mashabiki kujiua

Vitendo vya kujiua kutokana na matokeo ya soka vinashuhudiwa katika maeneo mbalimbali duniani. Kwa mfano Disemba 2003 Polisi nchini Kenya ilithibitisha kijana John Jimmy Macharia,23, kujiua kwa sababu ya timu yake anayoishabikia ya Manchester United kufungwa nyumbani bao 1-0 Newcastle United.

Alijirusha kutoka ghorofa ya saba. Mkuu wa Polisi wa kaunti ya Nairobi wakati huo, Benson Kibue alisema Macharia aliwaambia wenzake haweza kuona timu yake inafungwa mara mbili mfululizo kabla ya kuruka na kufariki.

Mwaka 2005, wakati wa mchezo wa fainali ya ligi ya mabingwa Ulaya, kati ya AC Milan na Liverpool. Mpaka kipindi cha kwanza kinamalizika Liverpool walikuwa nyumba kwa mabao 3-0, Mark Houghton, 43, mshabiki kindakindaki wa Liverpool aljiua akiamini timu hiyo inafungwa.

Alikutwa na mpenzi wake jikoni, ingawa kwa bahati mbaya kwake, Liverpool iliweza kurejesha mabao yote hayo na kushinda kwa mikwaju ya penati na kutwaa kombe.

Macharia na Houghton ni mifano tu ya mashabiki wengi wanaotamani kupata matokeo mazuri na yakufurahisha, na mfano wa mchezo huu ulivyo mtamu lakini wenye kuhitaji subra ya kupokea matokeo ya aina yoyote, vingine unaweza kuupenda sana na kuuuchukia sana.