Utafiti waonesha Wahindi wanapinga ndoa za imani mbili tofauti

Majimbo kadhaa nchini India yameanzisha sheria tata inayopiga marufuku mapenzi ya imani tofauti

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Majimbo kadhaa nchini India yameanzisha sheria tata inayopiga marufuku mapenzi ya imani tofauti

Raia wengi nchini India wanajichukulia kuwa wapenda dini na nchi yao lakini wanapinga ndoa ambazo wahusika ni wa imani tofauti, kulingana na utafiti uliofanywa na kituo cha Pew Research.

Watu wa imani mbalimbali nchini humo walisema kusitisha ndoa ambazo wahusika ni wa imani mbili tofauti kwao ni kipaumbele.

Utafiti huo unawadia baada ya kuanzishwa kwa sheria katika majimbo kadhaa ya India inayochukulia ndoa za watu ambao dini zao ni tofauti kuwa kitendo cha uhalifu.

Kituo cha Pew kilihoji watu 30,000 kote nchini India wa lugha 17 tofauti.

Waliohojiwa walikuwa wanatoka majimbo 26 na maeneo matatu tofati ya utawala.

Kulingana na utafiti huo, asilimia 80 ya Waislamu waliohojiwa walihisi kuna umuhimu wa kusitisha watu kutoka jamii yao kuoana na watu wa dini nyingine. Karibu asilimia 65 ya Wahindu pia nao walikuwa na hisia sawa na hizo.

Utafiti huo pia uliulizia juu ya uhusiano kati ya imani tofauti na mataifa tofauti na kubaini kuwa Wahindu "wanachukulia utambulisho wa dini yao na utaifa wao kama vyenye uhusiano wa karibu sana".

Karibu theluthi mbili ya Wahindu (asilimia 64) walisema ni muhimu kuwa wa dini moja ili kuwa "Mhindu halisi".

Utafiti huo ulibani kwamba licha ya kushirikishana maadili fulani na imani za kidini, watu wa jamii kuu wa dini za Hindu "mara nyingi huwa hawahisi kama kuna mengi wanayofanana".

"Wakati huo huo, Wahindu walionesha shauku ya kuvumilia dini za wengine na kuendelea kupendelea kudumisha jamii za dini zao katika mazingira tofauti," utafiti huo umeonesha.

Wengi wao walionesha kwamba wanapendelea kutokuwa na watu wa dini tofauti na zao katika maeneo ya makazi au vijijini mwao.

Ndoa kati ya Wahindu na Waislamu zimekuwa zikikosolewa katika familia za Kihindu zenye msimamo mkali lakini sasa hivi pia, wanandoa wanakabiliwa na vikwazo vya kisheria.

Sheria Maalum ya Ndoa ya India inahitaji kutolewa kwa ilani ya siku 30 kwa wanandoa wa imani tofauti.

Na baadhi ya majimbo ya India yakiongozwa na chama tawala cha Bharatiya Janata (BJP) yamechukua hatua zaidi na kuanzisha sheria ambazo zinapiga marufuku "kubadilisha dini kwa kulazimishwa" au kwa kilaghai.

Na ni kutokana na hili mrengo wa kulia wa makundi ya Wahindu wanayataja mapenzi ya aina hiyo kuwa "mapenzi ya jihad" dhana isiyokuwa na msingi wowote ambapo wanaume Waislamu wanashutumiwa kwa kuhadaa wanawake wa Kihindu eti nia yao kuu ikiwa ni kuwabadilisha dini ili wawe Waslamu.

Wanandoa wa imani tofauti wanakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo za kijamii na sheria mpya iliyoanzishwa

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Wanandoa wa imani tofauti wanakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo za kijamii na sheria mpya iliyoanzishwa

Kupinga uhusiano wa imani tofauti ni jambo ambalo Sumit Chauhan na mke wake Azra Parveen wanaweza kujihusisha nalo kwa kari

Bwana Chauhan anatoka familia ya Wahindu, ingawa anajitambua kama wa tabaka la Dalit ambalo awali lilifahamika kuwa la (wasioguswa) huku mke wake Bi. Parveen yeye akiwa ni wa dini ya Kiislamu.

Bwana Chauhan alisema kuwa jamaa zake wa Kihindu "walikuwa na dhana potovu kuhusu jamii ya Kiislamu, lakini akawashawishi mama yake, dada yake na kaka yake."

Hata hivyo, kwa Bi. Parveen, mambo hayakuwa rahisi. Familia yake ilikataa wawili hao waowane, anasema. Na walichoamua kufanya ni kufunga ndoa yao kisiri na familia ya Bi. Parveen ikasusia na hawakuwa wanazungumza nao kwa kipindi cha karibu miaka mitatu, Bwana Chauhan amesema.

Na hata ingawa sasa hivi wanazungumza, wazazi wa Bi. Parveen bado hawawezi kutambua ndoa yao hadharani.

"Mwaka jana, dada mdogo wa mke wangu aliolewa lakini sisi hatukualikwa," Bwana Chauhan amesema. "Huna haja ya kubadilisha dini ya mtu ili kumuoa unayempenda."