Kwa nini jeshi la Marekani lina wasiwasi na China na Urusi juu ya 'viumbe vya ajabu angani'?

Keyframe #1

Chanzo cha picha, US Department of Defence

Serilkali ya Marekani imetoa rasmi ripoti iliyokuwa ikisubiriwa kwa hamu kuhusu viumbe visivyotambulika vinavyopaa angani.

Hiki ndicho tunachokifahamu kufikia sasa.

Ripoti hiyo ilitakiwa na Bunge la Wawakilishi la Marekani baada ya matukio kadhaa kuripotiwa kutoka katika jeshi la Marekani juu ya kuonekana kwa viumbe vinavyosafiri angani vikiwa kwenye mwendo wa kasi.

Lakini kukiwa na ushahidi kidogo kuthibitisha au kukanusha uwepo wa viumbe hivyo, vya anga vyenye kuvuka magalaksi, bado hakujabainika ikiwa kuna chochote ambacho kinaweza kubadilika.

Viongozi wa ngazi za juu za kijeshi wameonya kuwa, kama si viumbe vya ajabu, basi vitu hivyo huenda ikawa ni teknolojia ya ajabu ya maadua wa Marekani, mataifa kama Urusi au Uchina.

Ripoti hiyo inasemaje?

Jopo lililoandaa ripoti hiyo lilibaini kuwa "hakuna kinanochoonesha wazi kwamba kuna chochote kisichokuwa cha duniani" kwa ndege lakini pia haikutupilia mbali uwezekano wa hilo.

Maelezo ambayo yangeweza kutolewa yalijumuisha vyombo vya kawaida vinavyopaa angani kama vile ndege zisizokuwa na rubani na ndege mnyama, mambo mengine ya ajabu ya angani kama vijipande vya barafu, maendeleo mapya ya serikali ya Marekani au mashirika ya kibinafsi na teknolojia za mahasimu wa kigeni. Ripoti hiyo pia ilijumuisha kundi la "mengineo".

Maafisa hao pia walitathmini matukio 144 yaliyotokea miongo miwili iliyopita ikiwemo video tatu ambazo zilitolewa na Pentagon mwaka jana na kuzielezea kama zenye kuonesha "viumbe vya angani visiyoelezeka".

Maelezo ya video, Viumbe wa ajabu waliothibitishwa na Marekani kuwepo angani

Makao makuu ya jeshi la Marekani, Pentagon ilianzisha jopo kazi kuchunguza matukio ya angani yasiojulikana mnamo mwezi Agosti mwaka jana kufuatilia vyombo vya angani vinavyopaa visivyotambilika.

Jukumu la jopo hilo lilikuwa ni "kubaini, kutathmini na kuorodhesha" matukio hayo pamoja na "kuvibaini vyombo husika" hasa kuhusu "uhalisia na chimbuko", Pentagon au makao makuu ya Wizara ya Ulinzi Marekani imesema.

Baadhi ya taarifa zinazochukuliwa kuwa za siri kwenye ripoti hiyo zilikabidhiwa wabunge mapema mwezi huu.

Kwanini sasa suala hili linafuatiliwa kwa karibu sasa?

Shinikizo la umma kwa Marekani kuweka wazi kile inachojua kuhusu viumbe hivi vya kigeni na vya ajabu angani limekuwa likiongezeka kwa miongo kadhaa sasa huku makundi ya kiraia yakisema kuwa ushahidi wa uwepo wa viumbe hivyo umedidimzwa na serikali.

Pentagon imekuwa ikikusanya data kimya kimya tangu mwaka 2007 kama sehemu ya mpango maalumu wa kijeshi uliokuwa usiojulikana sana.

Pesa za kufadhili mpango huo zilitokana na ombi la Seneta wa Nevada wa chama cha Democratic ambaye aliwakilisha eneo lake lenye kambi ya kijeshi ambako wataalamu wa nadharia za kisiri wanaamini kuwa kuna mengi ya kisiri yaliyokusanywa kutoka kwenye chombo kisichojulikana kilichoanguka katika mji wa Roswell ambayo yamefanyiwa utafiti tangu mwaka 1947.

Objects in the sky photographed in Massachusetts in 1952

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Vitu visivyojulikana vilipigwa picha katika anga la Massachusetts, Marekani mwaka1952

Waliokuwa maafisa wa ngazi ya juu na hata waliokuwa Marais hivi karibuni waliwahi kutathmini ikiwa ni suala hilo lina ukweli wowote. Hatimaye nuru imechomoza juu ya hilo.

Aliyekuwa Meneja wa Kampeni wa Hillary Clinton, John Podesta, ambaye alifuatilia nadharia za jopo la viumbe vya angani visivyojulikana, aliahidi katika kampeni ya mwaka 2016 kwamba Bi Clinton atatoa taarifa ya serikali inayosemekana kuwa siri kuhusu vitu hivyo ikiwa angeshinda urais.

Katika mahojiano mwaka jana, aliyekuwa rais wa MarekaniDonald Trump alisema kwamba hawezi kutoa taarifa hiyo - hata kwa familia yake mwenyewe kuhusu kile alichojifunza juu ya vitu hivyo vya angani visivyojulikana.

"Sitawaeleza kuhusu ninachokijua, lakini inafurahisha sana," alisema.

Aliyekuwa Rais wa Marekani Barack Obama aliweka wazi zaidi mnamo mwezi Mei aliposema katika kipindi cha kwenye televisheni kinachosimamiwa na James Corden kwamba: "Nilipoingia madarakani niliuliza… Je kuna maabara ambako tunahifadhi majaribio na vyombo vya angani? Na unajua walifanya utafiti kidogo na majibu yakawa ni hapana."

"Ukweli uliopo, na hapa nalizungumzia hili kwa uzito mkubwa, kuna video na rekodi zinazoonesha uwepo wa vyombo na viumbe kwenye anga, ambavyo hatujavijua hasa ni nini," Bwana Obama aliendelea kusema.

"Hatuwezi kuelezea mwendokasi wa vifaa hivyo au njia vinavyotumia... na, nafikiria kwamba watu wanalichukulia hili kwa uzito mkubwa kujaribu kuchunguza na kujua ni nini hasa."

Ni ushahidi gani uliopo?

A sign in San Francisco shows an alien abduction

Chanzo cha picha, Getty Images

Maafisa wengine wa jeshi la Marekani na wa mashirika ya Kiintelijensia wameelezea juu ya kuonekana kwa viumbe na vitu vya ajabu angani huku baadhi ya ripoti hizo zenye uhakika zaidi zikitoka kwa marubani ambao binafsi wamewahi kushuhudia viumbe hivyo karibu kabisa na silaha za kijeshi na vituo vya mafunzo wakiwa kwenye chumba cha rubani.

Mnamo mwezi Machi, aliyekuwa mkurugenzi wa Usalama wa Taifa wa Trump, Bw John Ratcliffe - ambaye awali alisimamia mashirika yote 18 ya kiusalama - alizungumzia kwa kifupi mazingira hayo kupitia shirika la habari la Fox News na kusema: "Ukweli ni kwamba, kumekuwa na matukio mengi ya angani yanayoonekana sasa hivi kuliko yale ambayo yamezungumzwa wazi kwa umma."

"Unazungumzia viumbe na vifaa ambayo vimeonekana na marubani wa jeshi au picha zao kunaswa na satelaiti ambavyo vipo katika mizunguko ambayo ni vigumu kuifuatilia, ambayo hatuna teknolojia ya kuifuatilia au kasi yake ni juu zaidi kuliko hata sauti."

Kupitia shirika la habari la CBS katika mahojiano ya dakika 60 mwezi uliopita, waliokuwa marubani wa jeshi la majini walizungumzia kuona chombo katika Bahari ya Pasifiki kilichoonekana kuakisi mienendo yao.

Je ni nchi gani zingine zinazofuatilia viumbe hivyo visivyojulikana?

Sign for Little A'Le'Inn and flying saucer hanging from tow truck, Rachel, Nevada

Chanzo cha picha, Getty Images

Seneta mstaafu Reid ametetea dola milioni 22 sawa na (£16m) alizopata kutoka kwa mpango wa kufuatilia viumbe hivyo unaosimamiwa na Pentagon, akisema nchi nyingine pia zinafanyia utafiti suala hili.

"Tunajua kuwa China inafanya hivyo," amezungumza na jarida la Nevada Newsmakers mwaka 2019. "Tunajua kuwa Urusi, ambayo inaongozwa na jasusi, pia nayo inafanya hivyo, kwahiyo, ni muhimu ikiwa pia sisi, tutalifuatilia kwa karibu suala hili."

Utafiti uliofanywa na Wizara ya Ulizni ya Marekani "umeonesha kuwa sio watu wawili, watu wanne au sita au 20 people bali ni mamia na mamia ya watu wamewahi kuona vyombo hivyo wakati mwingine wameviona wakati mmoja," alisema.