Mambo tisa ya kushangaza kuuhusu Mwezi na Marekani ilipotaka kuulipua

Chanzo cha picha, EPA
Umbo la mwezi hubadilika na hata rangi yake, lakini tangu jadi binadamu amekuwa akivutiwa na maumbile yake. Kuna Mwezi Mpevu, Mwezi Mwandamo, Hilali na hata wakati mwezi hupatwa na jua.
Hapa tumekuandalia mambo tisa ya kushangaza kuuhusu Mwezi.
1. Mpango wa Marekani kuulipua Mwezi
Marekani wakati mmoja ilitaka kuulipua Mwezi kwa kutumia bomu la nyuklia
Marekani ilikua inataka sana kulipua bomu la nyuklia mwezini.
Lengo lilikuwa ni kuonyesha ubabe wa Marekani kuiwezesha kuitia kiwewe Urusi na washirika wake wakati wa vita baridi, hasa baada ya Muungano wa Usovieti kuongoza katika jitihada za kupeleleza na kutalii anga za juu, hasa baada ya kurusha satelaiti ya kwanza kwenye mzingo wa dunia, satelaiti ya Sputnik 1 mnamo 4 Oktoba 1957.
Wataalamu walikuwa pia wanachunguza madhara ambayo yangesababishwa na mlipuko mkubwa wa nyuklia kwenye mazingira.
Mradi huo wa siri ulipewa jina 'A Study of Lunar Research Flights', au 'Project A119' na ulianzishwa mwaka 1958.
Utafiti hata hivyo ulikuwa umeanza kisiri mwaka 1949 katika kituo cha utafiti kuhusu silaha cha ARF katika Taasisi ya Teknolojia ya Illinois.
Mlipuko wa bomu hilo ungekuwa mkubwa sana hivi kwamba ungeonekana kutoka duniani.
Mpango huo haukutekelezwa kutokana na wasiwasi kwamba raia hawangeupokea vyema na pia hatari kwa binadamu iwapo mpango huo ungeenda mrama na ulifutwa rasmi Januari 1959.
Aidha, kiongozi wa mradi huo Leonard Reiffel alihofia hatua kama hiyo ingekuwa hatari kwa juhudi za baadaye za kupeleleza zaidi kwenye Mwezi na pia mpango wa kuwapeleka binadamu wakaishi huko.
Taarifa za kuwepo kwa mpango huo zilifichuliwa mwaka 2000.
Je lengo na madhumuni yake ilikuwa nini?
Marekani ilitaka kuuonesha ulimwengu kwamba haikupoteza ushindani wa angani kabla ya ushindani wenyewe kuanza.
Taifa hilo lilitaka kuonesha ishara za hakikisho kwamba wakomyunisti hawakuwa mbele na kwamba Spuntnik haitafuatiwa na mvua ya makombora ya nyuklia kutoka kwa Muungano wa Usoveti kuelekea Marekani.
Taifa hilo lenye uwezo mkubwa duniani lilitaka kuonesha ulimwengu kwamba linaendelea katika ushindani huo wa angani. Hivyobasi lilihitaji kuchukua hatua kubwa sawa na kuulipua mwezi .
Kwa kutekeleza shambulio, Marekani haikuwa na lengo lolote bali tu kuonesha ulimwengu kwamba inaweza kufanya kitu tofauti.
Hatahivyo mpango huo ulifutiliwa mbali - lakini sababu yake haijajulikana hadi leo.
Kile kilichopo ni uvumi kutoka vyanzo tofauti .
Wengine wanasema kwamba Wana Anga wa Marekani walisitisha mpango huo kutokana na hatari ambayo ingewafikia wanadamu walio ardhini{ kwa mfano iwapo mradi huo ungefeli na kusababisha janga}.
Wengine wanasema kwamba wanasayansi walikua na wasiwasi hatua hiyo huenda ingechafua mwezi kwa mionzi na hivyobasi kuzuia miradi yoyote siku zijazo kwenda mwezini.
Pengine huenda mipango ya wanaanga hao ingefutwa iwapo umma ungeona kwamba ni mpango wa kuangamiza urembo wa mwezi badala ya kuonesha ubabe wa wanasayansi wa Marekani.
2. Mwezi si tufe
Mwezi una umbo la yai. Ukiuangalia kile unachokiona ni moja ya sehemu ndogo za kando. Si kitu kilicho na umbo lililo sawa kwa uzito- eneo lake la kati la uzito haliko kabisa katikati mwa Mwezi bali karibu kilomita 2 kutoka sehemu ambayo inadhaniwa kuwa ndicho kitovu cha Mwezi.
3. Hatuuoni mwezi wote.
Kwa kila wakati fulani sisi huona asilimia 59 ya Mwezi. Uliobakia asilimia 41 hauwezi kuonekana kutoka duniani. Na kama huwezi kuamini, kama unaweza kwenda anga za mbali na kusimama eneo hilo la asilimia 41 huwezi kamwe kuiona dunia!
4. Mwezi wa Samawati ulitokana na volkano

Chanzo cha picha, Barcroft Media/Getty Images
Umewahi kusikia kuhusu Mwezi wa Samawati au Buluu ambao kwa Kiingereza huitwa Blue moon? Matumizi ya msemo huu yanaaminika kuanzia mwaka 1883 kufuatia kulipuka kwa mlima wa volkano wa Krakatoa nchini Indonesia. Vumbi kubwa lilijaa angani hivi kwamba wakati uliuangalia Mwezi, ulionekana kama ulikuwa na rangi ya samawati.
Kwa kweli ni kitu ambacho hakikuwa cha kawaida ndio kikachangia msemo "once in a blue moon" ikimaanisha kitu ambacho ni nadra sana kutokea.
5. Kupatwa kwa mwezi 'kulikosababishwa na joka'

Chanzo cha picha, SOPA Images/Getty Images
Imani za kale za Kichina zilisema kuwa kupatwa kwa jua kulisababishwa na joka kulimeza jua.
Kuzuia hilo watu walipiga kelele sana wakati wa kupatwa kwa jua kumfanya joka aogope na atoroke.
Pia waliamini kuwa chura mkubwa aliishi kwenye Mwezi akiketi juu ya shimo kubwa. Mashimo makubwa kwenye Mwezi hayakusababishwa na wanyama wowote bali yalisababishwa na mawe makubwa ya anga za juu kuugonga mwezi takriban miaka bilioni 4.1 iliyopita.
6. Mwezi unapunguza kasi ya dunia.
Wakati mwezi unakaribiana sana na dunia kile kinachaoitwa Perigee hutokea. Hii inamaanisha kuwa nguvu za kuzunguka kwa dunia hutwaliwa na Mwezi kidogo kidogo hali ambayo husababisha dunia kupunguza kasi yake kwa karibu milisekunde 1.5 kwa kila karne moja.
7. Mwangaza wa mwezi
Jua lina mwangaza wenye nguvu mara 14 zaidi ya ule wa Mwezi unapokuwa mpevu. Ili Mwezi mpevu upate kuwa na mwangaza sawa na wa jua unahitaji kuwa na Miezi 398.110. Wakati wa kupatwa kwa Mwezi wakati mwezi unaingia kwenye kivuli cha dunia viwango vya joto mwezini vinaweza kushuka hadi karibu nyuzi joto 500F (260 celsius) katika kipindi cha chini ya dakika 90
8. Leonardo da Vinci aligundua kuwa mwezi haukuwa na umbo la hilali

Chanzo cha picha, Getty Images
Wakati Mwezi unaonekana kuwa umbo la hilali, kile tunachokiona ni mwanga wa jua ukimulika sehemu ya Mwezi. Eneo jingine la mwezi halionekani vizuri, kulinngana na hali ya hewa. Leonardo da Vinci ndiye mtu wa kwanza anayejulikana kugundua kuwa mwezi haukuwa unapungua au kuongezeka. Ni kuwa sehemu yake nyingine ilikuwa imefichwa.
9. Kutoa majina kwenye Mwezi

Chanzo cha picha, Universal History Archive/Getty Images
Muungano wa Kimataifa wa Anga za Juu ndio huyapa majina mashimo yaliyo kwenye Mwezi na pia mawe, sayari na vitu vingine vinavyopatikana anga za juu. Mashimo makubwa kwenye mwezi yamepewa majina ya wanasayansi, wasanii na wapelelezi maarufu. Mashimbo yanayopatikana karibu na shimo kubwa la Apollo hupewa majina ya Wamarekani na yale yanayozunguka shimo kubwa la Mare Moscoviense hupewa majina ya Warusi.












