Patrice Lumumba: Athari za Covid zachelewesha kurejeshwa kwa jino la shujaa wa uhuru wa Congo Patrice Lumumba

Lumumba

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Ubelgiji imekiri kuhusika na kifo cha Patrice Lumumba, wakati wa vita baridi

Mabaki ya shujaa aliyepigania uhuru wa DR Congo, Patrice Lumumba yamechelewa kuwasili nchini humo kufuatia kuibuka kwa wimbi jipya la Covid-19.

Mabaki hayo yaliyochelewa kuwasili yanaaminika kuwa ni jino kutoka Ubelgiji lililopangwa kurejeshwa nchini DRC kwanza kabla ya kufanyika kwa mazishi ya heshima ya kitaifa yaliyopangwa kufanyika Juni 21, mwaka huu.

"Tunapaswa kujali afya za ndugu zetu," alisema Rais Félix Tshisekedi wa DRC.

Alisema hospitali za nchi hiyo zimejaa huku visa na vifo vitokanavyo na ugonjwa huo wa Covid1-19 vikiongozeka.

Patrice Lumumba alikuwa nani?

Lumumba

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha, Patrice Lumumba aliuawa 1961

Aliiongoza Congo kupata uhuru wake kutoka kwa Ubelgiji June, 1960 na kuwa waziri mkuu wa kwanza wa nchi hiyo.

Ingawa alikuja kupinduliwa na kufungwa jela, kabla ya kuuawa January, 1961 na na watu wanaoaminika kuungwa mkono na Marekani na Ubelgiji.

Mwaka 2002, Ubelgiji ilikubali kuwajibika na kifo chake, kitu ambacho Shirika la ujasusi la Marekani (CIA), linaamini kwamba kilichangia kusababisha vita baridi kati ya Marekani na Muungano wa Soviet.

Nchi zenye ngvu za magharibi zilihofia kwamba Lumumba angeungana na Soviet, hasa kwenye eneo la usambazaji wa madini ya uranium ya Congo.

Polisi mmoja wa Ubelgiji alikiri kuuyeyusha mwili wa Lumumba kwa tindikali, lakini akabakisha na kutunza jino lake. Mwaka jana mahakama nchini Ubelgiji iliamuru jino hilo kurejeshwa DRC, ingawa hakuna vipimo vya DNA vilivyofanyika kuthibitisha kwamba kweli lilikuwa jino la Lumumba.

Rais Tshisekedi alisema itatengenezwa makumbusho maalumu kwa ajili ya shujaa huyo wa uhuru huku kukipangwa kufanyika sherehe mbalimbali nchini humo. Hata hivyo sherehe zote za heshima zimesogezwa mbele mpaka Januari 2022 - itakapoadhimishwa miaka 61 ya kifo cha Lumumba.

Hali ni mbaya kiasi gani DR Congo?

Kwa sasa Congo inakabiliana na wimbi la tatu la maambukizi ya Covid-19, na Rais Tshisekedi alisema siku chache zijazo anaweza kutangaza hatua ngumu zaidi za kuchukuliwa ili kukabiliana na wimbi hilo.

Katika takwimu ziizotangazwa Ijumaa, kuna vifo vitatu na visa vipya 254 vya maambukizi ya Covid-19 hasa katika mji mkuu wa nchi hiyo, Kinshasa.

Tangu kuibuka kwa janga hilo, DRC yenye watu karibu milioni 80, imerekodi visa 35,000 na vifo 834 vitokanavyo na ugonjwa huo. Hata hivyo, wataalam wanasema vipo visa vingi tu ambavyo havijarekodiwa kutokana na nchi hiyo kuwa na mfumo mbovu wa afya.

DR Congo kwa sasa inaendesha kampeni ya chanjo ya corona, ikitumia chanjo ya AstraZeneca, lakini Rais Tshisekedi alisema anataka zoezi hilo liende kwa kasi kwa kutumia chanjo za aina nyingine pia.