Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Afrika Mashariki: Macho yote kwenye bajeti
Leo tarehe 10/06/2021 ni siku muhimu kwa baadhi ya nchi za Afrika ya Mashariki Tanzania, Kenya na Uganda ambapo zitasoma bajeti zao za kipindi cha mwaka 2021/2022.
Hii ni moja ya bajeti kuu ya serikali hizi inayosubiriwa kwa hamu na kwa hisia tofauti na wakazi pamoja na wawekezaji waliopo katika nchi hizi tatu.
Bajeti hii inasubiriwa kwa hamu kubwa sana kutokana na hali ya mdororo wa kiuchumi uliopo duniani hivi sasa uliosababishwa na virusi vya Corona, huku hali ya kiuchumi ikionyesha kuwa mbaya zaidi kwa nchi za bara la Afrika.
Hivyobasi wananchi wanasubiri kuona namna Serikali za nchi hizi; Tanzania, Kenya na Uganda zilivyojipanga kimkakati katika kushughulika na mdororo huu wa kiuchumi uliopo hivi sasa.
Hali ya kiuchumi katika mataifa haya kwa sasa;
Tanzania
Hali ya kiuchumi chini ya uongozi wa Rais aliyepo madarakani Rais Samia Suluhu Hassan inaonekana kutokufanya vizuri kutokana na madhara makubwa yaliyosababishwa kwa ukubwa na janga la Corona(COVID-19).
Uchumi wa Tanzania unaonekana kuporomoka kutoka 6.9% mwaka 2019/2020 hadi kufikia 4.7% mwaka huu 2021.
Zipo sekta ambazo hazijafanya vizuri kwa takribani miaka miwili (2) hivi sasa na mfano wa sekta hizo ni sekta ya utalii ambapo mapato yake yameshuka kutoka trilioni 2.7 hadi kufikia shilingi bilioni 598, huku ikikadiriwa ajira kutoka sekta kushuka kutoka 622,000 hadi 146,000 na watalii wakipungua kutoka 1,867,000 hadi 437,000.
Kwa ujumla hali ya uchumi wa Tanzania siyo ya kuridhisha hata kidogo hasa kutokana na makusanyo ya mapato ya serikali kuwa siyo ya kuridhisha na hivyo kupelekea shughuli nyingi za kimaendeleo kukwama na miradi mingine kutokamilika kwa wakati.
Ongezeko la ukosefu wa ajira hasa kwa vijana wanaomaliza elimu ya juu kuendelea kuongezeka maradufu ambapo zaidi ya watu 500,000 wanakadiriwa kuongezeka kwenye umaskini wa kutisha.
Deni la taifa likiongezeka na kufikia 59% kwa mwaka 2021.
Kenya
Hali ya kiuchumi imeendelea kudorora pamoja na jitihada zinazoendelea kuwekwa na serikali ya Kenya kupitia Rais wa nchi hiyo Mhe. Uhuru Kenyatta..
Hii ni kutokana na ukweli kwamba COVID-19 haikupata kuliacha taifa hilo la Kenya salama kiuchumi.
Uchumi wa Kenya umedorora ambapo inakadiriwa kuwa umeshuka kwa 1.4% kutoka 5.4% mwaka 2021.
Ambapo inakadiriwa kwamba kwa mwaka huu 2021 uchumi utakuwa 5.0% na 5.9% kwa 2022. Hii ni kutokana na hali ya uzalishaji katika viwanda kuonekana kudorora na hali ya utalii nayo ikiwa hoi bintaabani hivyo kupelekea hali ngumu ya uchumi kwa Wakenya wengi.
Inakadiriwa zaidi ya watu milioni 2 nchini Kenya watatumbukia katika umaskini wa kutisha( extremely poverty)na takribani watu 900,000 waliopo katika ajira watazikosa ajira zao.
Deni la taifa linaonekana kupaa kutoka 61% mwaka 2019 hadi kufikia 72% mwaka 2020 hii yote ni kiashiria kwamba hali ya kiuchumi ni mbaya.
Uganda
Kutokana na madhara ya corona, Uganda imeendelea kuwa katika hali mbaya kiuchumi kwa mwaka 2019/2020.
Uchumi wa Uganda ulikadiriwa kukua kwa 6.2% ikilinganishwa na hali ilivyo hivi sasa ambapo uchumi wake umeporomoka kutokana na kusuasua kwa shughuli za uzalishaji mali ambao ulichangiwa sana na kufungiwa kwa watu (Lockdown) pamoja na shughuli za uchaguzi uliopita ambazo zilipelekea watu wengi kuingiwa na hofu ya kujihusisha na shughuli za uchumi.
Benki kuu ya Uganda (BoU), ilikuja na tathmini kupitia ripoti ya fedha februari 2021, kuwa uchumi wa Uganda utakuwa kati ya 3% - 3.5% kwa mwaka huu 2021, lakini hali bado inaonekana kuwa ngumu sana pamoja na hatua za kimkakati zinazochukuliwa na serikali ya Uganda chini ya Rais Museven.
Matarajio ya wananchi na Bajeti ya 2021/2022
Punguzo la kodi kwenye bidhaa za chakula; hivi sasa vipato vya watu katika nchi hizi vimeshuka kwa asilimia kubwa sana ukizingatiia kumekuwapo na lockdown (kufungiwa) kwa watu kwa miezi kadhaa na hivyo kufanya watu kushindwa kufanya uzalishaji na hivyo kuwapelekea kuwa katika hali ngumu sana kiuchumi.
Hivyo wananchi wanategemea kuona serikali ikipunguza kodi kwenye mazao ya chakula ili waweze kumudu gharama za kununua chakula.
Punguzo la kodi kwenye vifaa vya ujenzi pamoja na mbegu za mazao;
Gharama za ujenzi pamoja na mbegu za mazao zinaonekana kuonekana kupaa juu kiasi cha kufanya wakulima kushindwa kumudu gharama hizo na hivyo kufanya kasi ya uzalishaji kushuka katika sekta ya kilimo huku katika gharama za ujenzi kuonekana kuwa juu kiasi kwamba wananchi wanashindwa kufanya ujenzi hivyo serikali ione kwa jicho kubwa namna yakuweza kupunguza gharama ya vifaa vya ujenzi na hilo ndio tegemeo kubwa la wananchi.
Punguzo la riba za mikopo;
Wananchi wanategemea kwamba katika bajeti hii serikali itasimama na wananchi katika kuona ni kwa jinsi gani wanaweza kupata mikopo yenye riba nafuu ili wananchi hawa waweze kurejea katika shughuli zao za kiuchumi kwa kupata mikopo kupitia taasisi za kifedha zilizopo kama vile mabenki.
Malipo ya madeni;
Serikali ina madeni mengi sana hasa kutoka kwa wafanyabiashara.
Kwa mfano Tanzania wakandarasi wanadai kutokulipwa fedha zao kwa muda mrefu hivi sasa hivyo kujikuta wakishindwa kufanya kazi zao inavyotakiwa, hivyo wanategemea sana kwamba bajeti hii watapata kulipwa fedha zao na hivyo kuendeleza gurudumu la maendeleo.
Chanjo ya Corona;
Wananchi wanategemea kwamba serikali za nchi hizi tatu zitaweka fungu kwaajili ya wananchi wake kuweza kupata chanjo dhidi ya COVID-19 hasa ikizingatiwa kwamba hali ya maambukizi ikiendelea kuwepo na zaidi kukiwepo na tishio jingine la COVID - 19.
Ujenzi na maboresho ya miundombinu;
Hivi sasa barabara nyingi za vijijini zimeonekana kuwa katika hali ngumu kutokana na kuharibika sana kutokana na mvua na nyingine kusahauliwa na serikali katika kufanyiwa marekebisho hivyo ni mategemeo yao kuwa kupitia bajeti hii serikali zitatenga fungu kwaajili ya kuzifanyia ukarabati na matengenezo.
Na barabara nyingi za mijini nazo zimekuwa kero kwani zimekuwa hazifanyiwi marekebisho kwa wakati na hivyo kuleta usumbufu kwa watumiaji wa barabara hizo.
Ajira;
Asilimia kubwa ya vijana wengi hivi sasa hawana ajira.
Hivyo vijana wengi wanategemea kuwa serikali kupitia hii bajeti yake itakuja na suluhu ya ni namna gani imejipanga kimkakati katika kupambana na janga hili la ukosefu wa ajira kwa vijana wengi.
Kero ya maji;
Kuna shida kubwa ya upatikanaji wa maji safi na salama kwa maeneo mengi ya mijini na vijijini hivyo kwa bajeti hii ya mwaka 2021/2022 wananchi wanategemea sana kuona miundombinu ya maji ikienda kufanyiwa ukarabati na sehemu ambazo kuna shida ya maji serikali ikienda kuhakikisha wanapata maji safi na salama.
Upatikanaji wa dawa na vifaa tiba;
Wananchi wanategemea kuwa bajeti ya mwaka huu itaongeza fungu la kununua madawa na vifaa vya kutosha kwaajili ya mahospitali yetu kwani kumekuwepo na malalamiko mengi hasa kutoka kwenye kundi la wazee kuwa hakuna madawa na vifaa tiba katika mahospitali, vituo vya afya pamoja na zahanati.
Maboresho ya masoko ya kibiashara;
Wananchi watagemea kupitia bajeti zitakazosomwa kutakuwa na fungu lililotengwa kwa ajili ya kuboresha maeneo ya masoko mengi bado miundombinu ya masoko hayo ni magumu sana.
Masoko mengi yaliyopo vijijini ambako ndiko kuna biashara nyingi za mazao bado masoko yake yanaonekana kuwa katika hali ngumu, hivyo tegemeo la wananchi wengi ni uborershwaji wa maeneo haya muhimu kwaajili ya wafanyabishara kutekeleza majukumu yao.
Nini kifanyike kusaidia serikali kupambana na kushuka kwa uchumi kupitia uwasilishwaji wa Bajeti hizi?
Kupitia upya sera za uwekezaji, hili limeonekana kuwa changamoto kubwa sana kwa nchi zote tatu kwani sera zao za uwekezaji zimeonekana zikiwaweka wawekezaji njiapanda kutokana na mkanganyiko uliopo kwenye sera hizi na mwingiliano mkubwa wa kiutendaji.
Kuweka vipaumbele muhimu katika kunyanyua uchumi, mfano kilimo, mawasiliano, usafirishaji,ili kuweza kupambana na changamoto za kiuchumi zilizopo hivi sasa.
Na sekta hizi ni muhimu kwani zinaonekana kutokuathirika sana na janga hili la Corona.
Hivyo serikali wakifanya usimamizi mzuri utasaidia sana katika kupambana na mdororo wa uchumi.
Kuondoa kero zilizopo kwenye mipaka ya nchi zao,hili nalo litasaidia sana wafanyabiashara kuweza kutafuta masoko ya bidhaa zao na si hivyo tu bali litasaidia sana kuvutia wawekezaji hasa katika ukanda huu wa Afrika Mashariki zilizopo hizi nchi.