Jinsi sera mpya ya watoto 3 inavyozidi kuwaumiza Wachina

Uamuzi wa China wa kuruhusu watu kuwa na hadi watoto watatu umeendelea kuibua gumzo mitandaoni baadhi yao wakihoji ikiwa hatua hiyo huenda imechelewa.

Tangazo hilo limetolewa baada ya data ya sensa kuonesha kushuka vibaya kwa viwango vya watu kuzaana.

Baadhi yao - hasa vijana wa sasa - wanauliza jinsi tangazo hilo la Jumatatu ambalo pia linalenga kuchelewesha umri wa kustaafu litakavyotekelezwa.

Wengine walitoa wito kwa jamaa zao kufidiwa kutokana na usumbufu wa kiakili waliopata kutokana na hamu ya kutaka kuwa na zaidi ya mtoto mmoja miaka ya nyuma.

Chini ya sera kali ya kuwa na mtoto mmoja iliyoanzishwa nchini China mwaka 1979, familia zilizokiuka sheria hiyo zilipigwa faini, kupoteza kazi na hata wakati mwingine kulazimishwa kutoa mimba.

Wanaharakati wanasema pia ilisababisha maswala kama mauaji ya watoto wachanga wa kike, kutoripotiwa inavyostahili kuzaliwa kwa watoto wa kike.

Maelezo kadhaa ya jinsi familia zilivyoteseka wakati huo sasa yameibuka mtandaoni kujibu sera hiyo mpya.

'Kila mtu amekuwa data'

Mtu mmoja katika mtandao wa kijamii wa Weibo huko China alidai mama yake alilazimishwa kutumia mbinu ya mpango wa uzazi (IUD) baada ya kumzaa kama mtoto wa pili, akiongeza kuwa mpaka leo anakabiliwa na athari zake.

"Sera hii mpya ni ishara ya kutojali - haiangazii usumbufu wa kimawazo iliyosababishia watu. Kila mtu amegeuzwa kuwa data, badala ya watu kuonekana na kuheshimiwa," aliandika katika mtandao wa Weibo akitumia akaunti ya siri inayojulikana kama Chillsyrup.

Watu wengi walikumbuka kisa cha Feng Jiamei ambaye alilazimishwa kutoa mimba ya miezi saba kwasababu alishindwa kulipa faini ya kuzaa mtoto wa pili.

Maafisa wa jiji waliomba msamaha baada ya picha inayomuonesha Bi Feng na mtoto wake aliyetolewa tumboni kabla ya muda wake wa kuzaliwa kufika, kuwashangaza watumiaji wa mitandaoni.

Mwingine anayefahamika kama Jia Shuai aliandika....kuwa mtoto haramu aliyelelewa vijijini, anakumbuka alivyoruka kwenye kidimbwi kujificha asionekane na maafisa wa uzazi wa mpango.

"Ukishindwa kulipa faini, baadhi ya maafisa wangelichukuwa vitu kwenye nyumba yenu au kuondoka na mifugo wenu. Ni kumbukumbu ya kustaajabisha" aliandika.

Mtumiaji mwingine wa ntandao alidai kuwa dada yake mdogo bado yuko hai kutokana na huruma ya daktari ambaye alimwachia mama yake atoroke hospitali, baada ya kuagizwa aende akatoe mimba ya miezi nane.

Huku hayo yakijiri mtengenezaji filamu Zhang Yimou na mke wake- ambao walipigwa faini kubwa ya dola milioni 1.2m (£842,850) mwaka 2014 kwa kukiuka sera ta nchi hiyo ya kuwa na mtoto mmoja - pia alitoa kauli yake kuhusu tangazo hilo jipya.

"Tulikamilisha wajibu kabla ya muda," wanandoa hao waliandika kwenye mtandao wa Weibo, wakiambatanisha na emoji ya kunyoosha mikono.

Shirika la kutetea haki la Amnesty International limesema sera hiyo, sawa na iliyotangulia, bado inakiuka haki ya kingono na ya uzazi.

"Serikali haina mamlaka ya kudhibiti idadi ya watoto watu wanatakiwa kuwa nao. Badala ya 'kudhibiti' sera yake ya uzazi, China inatakiwa kuheshimu maisha ya watu na kukomesha njia yoyote ya kuwaamulia watu jinsi ya kupanga familia zao," alisema mkuu wa shirika hilo nchini China, Joshua Rosenzweig.

Kizazi kilichojipata katika njia panda'

Lakini wengi wanaokosoa sera hii mpya ni vijana wa kizazi cha sasa, ambao walilalamikia "kuchanganyikiwa" kizazi ambacho kimejipata katikati njia panda kuhusu ya sera hiyo.

"Kwa wale tuliozaliwa baada ya miaka ya 1980 na 1990 - hatupumui. Serikali inatuhamasisha tuzae watoto, lakini bado wakati huo huo inataka tufanye kazi kwa muda mrefu. Haya ni maisha gani?" Mmoja aliuliza.

Kwa zaidi ya miongo minne, umri wa kustaafu nchini China haujabadilishwa, miaka 60 kwa wanaume na 55 kwa wanawake.

Lakini siku ya Jumatatu China ilisema itachelewesha kwa awamu miaka ya kustaafu, ijapokuwa haikutoa maelezo.

"Sitaki hata mtoto mmoja, itakuwa watatu ," Mwingine wanandika.

Kwanini wanawake wa China hawataki watoto zaidi?

Hadi maelezo zaidi yatakapotolewa, baadhi ya watu katika mitandao ya kijamii wanatilia shaka kubadilishwa kwa sera hiyo kutachangia ongezeko la watoto wanaozaliwa.

Wakati China ilipofutilia mbali sera yake ya kuwa na mtoto mmoja mnamo 2016 na kuruhusu watu kuwa na hadi watoto wawili, ilishindwa kubadili msimamo wa watu juu ya suala hilo.

"Kama kulegeza sera ya uzazi ingelikuwa na ufanisi, sera ya sasa ya watoto wawili ingelikuwa imeonesha ufanisi wake pia," Hao Zhou, mchumi mwandamizi wa Commerzbank, aliliambia shirika la habari la Reuters Jumatatu.wa.