Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Mali :Assimi Goïta afanya Mapinduzi ya pili ya kijeshi chini ya mwaka mmoja
Rais wa Mali na Waziri mkuu wameondolwa madarakani na afisa wa jeshi ambaye aliongoza maasi ya mwaka jana na kuteuliwa kuwa makamu wa rais katika serikali ya mpito
Kanali Assimi Goïta amesema rais Bah Ndaw na waziri mkuu Moctar Ouane walishindwa kutekeleza majukumu yao na walikuwa na njama ya kuhujumu mchakato wa mpito nchini humo .
Kiongozi huyo mkuu wa kijeshi aliyehusika na uasi uliomuondoa madarakani rais Ibrahim Boubacar Keita mnamo Agosti 2020 amesema amewaondoa wawili hao ofisini kwa kuvunja vipengee kuhusu utawala wa mpito
Katika taarifa iliyosomwa kwenye televisheni ya kitaifa ya umma (ORTM), Baba Cissé ambaye ni mshauri maalum wa Assimi Goita, kiongozi wa jeshi aliyeongoza mapinduzi hayo alitangaza Jumanne kuwa rais wa mpito Bah Ndaw na waziri mkuu Moctar Ouane ambao waliokamatwa siku ya jumatatu wameondolewa ofisini na yeye.
Aliwalaumu haswa kwa kuvunja vifungu vya mpito. Jana masaa machache baada ya mabadiliko ya serikali ambayo yaliondoa washiriki wakuu wawili wa jeshi , walinzi wengine wa rais na waziri mkuu waliwakamata na kuwapeleka kwenye kambi ya Kati, iliyoko karibu kilomita 15 kutoka Bamako, mji mkuu.
Mali inatarajiwa kuandaa uchaguzi wa ubunge na urais mnamo Februari 2022, lakini mivutano ya kisiasa inaweza kuhatarisha uchaguzi huu.
Yote yalianzaje?
Rais na waziri mkuu walizuiliwa na wanajeshi saa kadhaa baada ya kutangazwa kwa mabadiliko ya baraza la mawaziri ambalo lilisababisha maafisa wakuu wawili wa jeshi ambao walishiriki katika mapinduzi ya mwaka jana kubadilishwa.
Rais Bah Ndaw na Waziri Mkuu Moctar Ouane wanaripotiwa kusafirishwa na wanajeshi kwenda kwenye kambi ya jeshi ya Kati karibu na mji mkuu, Bamako.
Katika mabadiliko ya baraza la mawaziri, waziri wa zamani wa ulinzi Kanali Sadio Camara na waziri wa zamani wa usalama Kanali Modibo Koné waliachwa nje .
Hakuna maelezo yaliyotolewa kwa kutengwa kwao.
Nafasi zao zilipaswa kuchukuliwa na Jenerali Souleymane Dacouré na Meja Jenerali Mamadou Lamine Diallo mtawalia.
Miongoni mwa mawaziri waliobaki kwenye viti vyao ni Luteni-Kanali Abdoulaye Maiga katika wizara ya utawala wa maeneo na Kanali Ismaël Wagué katika wizara ya upatanisho wa kitaifa.
Baraza la mawaziri lililoundwa upya lilikuwa na mawaziri 25, kati yao wanajeshi wanne na wanawake wanne.
Katika wizara ya sheria, Doucouré Sidi Samaké alichukua nafasi ya Mohammed Sida Dicko na katika wizara ya fedha Dionké Diarra alichukua nafasi ya Alfousseyni Sanou.
Umoja wa Mataifa wataka rais kuachiliwa
Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Mali umetaka kuachiliwa mara moja kwa Rais Bah Ndaw na Waziri Mkuu Moctar Ouane, baada ya ripoti kwamba walizuiliwa na wanajeshi.
Katika ujumbe wa twitter (kwa Kifaransa), ujumbe wa Minusma pia ulitaka utulivu katika taifa hilo masikini la Afrika Magharibi.
Hatua hiyo inajiri baada ya ripoti kwamba Rais wa mpito Ndaw na Bw Ouane waliongozwa na wanajeshi kwenda kwenye kambi ya jeshi ya Kati karibu na mji mkuu, Bamako.
Hii ilileta hofu ya mapinduzi ya pili ndani ya mwaka mmoja nchini humo.
Waziri wa Ulinzi Souleymane Doucouré pia ameripotiwa kuzuiliwa.
Mwishoni mwa Jumatatu, Bw Ouane aliiambia AFP kwa simu kwamba wanajeshi "walikuja kumchukua". Shirika hilo la habari limesema laini hiyo ilikatwa.
Muungano wa Afrika, Jumuiya ya Kiuchumi ya Mataifa ya Afrika Magharibi, EU na Marekani pia walilaani kukamatwa huko , wakisema wanasiasa hao wakuu wa Mali lazima waachiliwe bila masharti yoyote.
Kwa mara nyingine Mali inaonekana kutokuwa na utulivu miezi tisa tu baada ya mapinduzi ya kijeshi ambayo yalisababisha Rais Ibrahim Boubakar Keïta kuondolewa madarakani, mhariri wa BBC wa Afrika Will Ross anaripoti.
Anasema kwamba raia wengi wa Mali walikuwa wamekaribisha kuondoka kwa Bw Keita - lakini kuna hasira kwa utawala wa wanajeshi katika serikali ya mpito na kasi ndogo ya mageuzi yaliyoahidiwa.
Mapinduzi ya zamani ya mwaka 2012 yalisababisha wapiganaji wa Kiisilamu kutumia udhaifu uliokuwepo kuchukua eneo la kaskazini mwa Mali.
Vikosi vya Ufaransa vilisaidia kurejesha maeneo hayo chini ya utawala wa serikali lakini mashambulizi yamekuwa yakiendelea
Fursa kwa makundi yaliyojihami
Kutokuwepo kwa serikali thabiti nchini Mali kunaweza kukafunfua fursa nyingine kwa makundi yaliyojihami .
Mataifa kadhaa ya eneo la Sahel - sehemu ya mataifa kadhaa ya afrika ya kati na magharibi yaliyo jangwani yapo mashakani kwa sababu ya tishio la usalama kutoka kwa makundi mbali mbali yaliyojihami .
Hali hiyo imesababisha maeneo hayo kuwa katika hatari ya kukosa kabisa uthabiti na amani na maelfu ya watu katika nchi kama vile Nigeria , Mali,Chad ,Burkina Faso na Niger wameachwa bila makao .
Ufaransa ambayo imekuwa mstari wa mbele kuzisaidia nchi hizo kukabiliana na makundi mbali mbali ya wapiganaji pia imeonekana kushindwa katika kuleta utulivu katika eneo hilo .
Hali huenda ikawa mbaya zaidi kwa sababu ya kifo cha aliyekuwa rais wa Chad Idriss Deby ambaye alikuwa mojawapo ya viongozi wanaotegemewa kupambana na kundi la Boko Haram ambalo limekuwa likizihangaisha nchi za Nigeria , Chad ,Niger na Burkina faso .
Mashambulizi yalianza lini?
Mashambulio dhidi ya jeshi na raia katika eneo lote yanatokea kila mara na yameongezeka licha ya uwepo wa maelfu ya wanajeshi kutoka nchi zote zilizoathiriwa pamoja na Ufaransa. Mwaka wa 2019 kulikuwa na idadi kubwa zaidi ya vifo vya kila mwaka kutokana na mzozo wa silaha katika eneo la Sahel tangu 2012.
Hali imezidi kuwa mbaya na hata kuanza kuyaathiri mataifa ya Afrika magharibi ambayo hapo awali yalionekana kuwa salama .
Silaha zinatoka wapi?
Kuendelea kwa mapigano nchini Libya kumesababisha kutokuwepo kwa serikali thabiti kumudu mipaka ya nchi hiyo na maeneo ya Sahel na hivyo basi silaha hatari zimezidi kupatikana katika mikono ya makundi mbalimbali ya wapiganaji .
Kundi la Boko Haram limejiingiza katika ushirikiano na mitandao ya kimataifa ya ugaidi na kuendelea kufanya mashambulizi nje na ndani ya Nigeria huku serikali ya taifa hilo ikionekana kushindwa kuchukua hatua madhubuti za kuwahakikishia raia wake usalama .
Katika shambulizi moja lililosababisha vifo vya wanajeshi 89 wa Niger mwaka wa 2019 ,Ufaransa pia ilijipata ikisajili maafa ya wanajeshi wake baada ya helikopta ya kijeshi kuanguka nchini Mali mwezi Novemba mwaka huo .
Katika maeneo ya taifa la Mauritania makundi yenye silaha kali yameendelea kufanya mshambulizi dhidi ya maafisa wa usalama na hata kushikilia miji na sehemu zenye barabara muhimu katika maeneo ya mipakani .
Tatizo hilo lilianza mwaka wa 2012 wakati makundi ya wapiganaji waliokuwa na silaha walipoungana na kuchukua sehemu ya kaskazini mwa Mali na kuifanya Ufaransa kutuma vikosi vyake ili kuwazuia kufika mji mkuu Bamako .
Mkataba wa amani ulitiwa saoni lakini utulivu haukurejea kabisa na makundi mengine mapya yalichipuka katika nchi jirani za Mali, Burkina Faso na Niger.
Idadi ya watu wanaofariki kutokana na mashambulizi ya a makundi hayo imeongezeka mara tano tangu mwaka wa 2016 na mwaka wa 209 zaidi ya watu 4000 waliripotiwa kuawa katika ,mashambulizi ya wapiganaji wa makundi mbalimbali.
Ni makundi yapi yanayotekeleza mashambulizi?
Makundi yaliyojihami na mengine yanayohusishwa na Al Qaeda na Islamic State yamekuwa yakiendeleza shughuli zake katika eneo la Sahel na Afrika magharibi .
Sababu za makundi hayo kufika maeneo ya nchi hizo ni pamoja na ;
•Ukosefu wa vikosi vya kulinda mipaka
•Ukosefu wa huduma za serikali katika baadhi ya maeneo
•Wanajeshi wanaopigana na makundi hayo hawana mafunzo ya kutosha
•Makundi hayo yanaendesha biashara zenye faida kubwa za magendo,uuzaji wa dawa za kulevya ,uuzaji wa silaha ,ulanguzi wa watu na utekaji nyara
Kando na nchi hizo za Sahel kwa jina G5 sahel kuunda kikosi cha pamoja ili kupambana na makundi ya wapiganaji ,Ufaransa imekuwa ikivituma vikosi vyake kuvipiga jeki katika kampeni hizo lakini bila mafanikio ya kutosha . kufikia mwisho wa mwaka wa 2020 ,Ufaransa ilikuwa na takriban wanajeshi 5000 katika sehemu hiyo .
Umoja wa mataifa pia una zaidi ya wanajeshi 12,000 nchini Mali ilhali Marekani ina kambi mbili za droni nchini Niger . Katika nchi za Mali na Burkina Faso makundi hayo yamehusika na mauaji ya kila mara ya raia na vikosi vya usalama .
Makundi hayo huwa hayakiri kutekeleza mashambulizi dhidi ya raia lakini makubwa yanayotekeleza mashambulio hayo huko Sahel ni ;
•Makundi yanayohusiana na Al Qaeda , Jama'a Nusrat ul-Islam wa al-Muslimin - JNIM
•Makundi mengine yaliyojihami yenye malengo ya kisiasa au kikabila
Hadi kufikia sasa serikali za nchi hizo bado hazijaweza kupata suluhisho la tatizo la usalama katika mataifa hayo.
Changamoto kuhusu hali ya kiuchumi na maisha katika jamii nyingi za maeneo yenye mizozo hiyo zimechanganyika na maslahi ya kidini ,kikabila na kuzua mseto wa mambo mengi ambayo hayatoweza kusuluhishwa katika siku za hivi karibuni .
Iwapo hapatakuwa na serikali thabiti katika mataifa yanayohusika na mizozo kama vile Libya ambako silaha nyingi zinatokea ,itakua vigumu kumaliza kikamilifu matatizo ya ukosefu wa usalama katika eneo la Sahel na afrika magharibi .