Mzozo wa Israel na Palestina:Yitzhak Rabin na Yasser Arafat walikuwa nguzo muhimu kuleta amani kwa watu wao

Iwapo kuna viongozi wa Israel na Palestina ambao wangetamani sana kuwepo Amani kati ya Waisrali na Wapalestina basi ni aliyekuwa waziri mkuu Yitzhak Rabin na aliyekuwa kiongozi wa PLO na harakati za Wapalestina Yasser Arafat.

Hata hivyo miaka mingi baada ya viongozi hao kuaga dunia ,mapigano na uhasama baina ya watu wao yanaendelea na kusababisha maafa ya watu wengi na wengine kujeruhiwa .Je,walipigania nini viongozi hao na ni vipi walilipia gharama ya kutaka pawepo amani?

Mnamo tarehe 13 Septemba 1993, Arafat na Waziri Mkuu wa Israeli, Yitzhak Rabin, walitokea uwanja mdogo wa bustani wa Ikulu ya White House baada ya mazungumzo ya siri yaliyowezeshwa na wanadiplomasia wa Norway.

Pande hizo mbili zilitia saini Azimio la Kanuni, makubaliano yanayowaruhusu Wapalestina kujitawala katika Ukanda wa Gaza na mji wa Ukingo wa Magharibi wa Yeriko na badala yake PLO kutambua serikali ya Kiyahudi.

Lakini maswala ya kimsingi kama makazi ya Wayahudi kwenye ardhi inayokaliwa, mustakabali wa Wapalestina ambao walifanywa wakimbizi mnamo 1948 na mustakabali wa Jerusalem yaliachwa bila uamuzi.

Ingawa Arafat alirudi kwa ushindi huko Gaza mwaka uliofuata, mchakato wa amani ulijaa shida.

Makubaliano hayo yalifanywa kwa mujibu wa Makubaliano ya Oslo, yaliyotiwa saini Washington, D.C. mnamo Septemba 13, 1993. Huu ulikuwa mkataba wa kwanza wa moja kwa moja, wa ana kwa ana kati ya Israeli na Wapalestina na ulikubali haki ya Israeli kuwapo. Iliundwa pia kama mfumo wa uhusiano wa baadaye kati ya pande hizo mbili.

Wawili hao walionekana kama viongozi ambao wangewangoza watu watu wao kufungua awamu mpya ya uhusiano mwema na kumaliza makabiliano ya muda mrefu katika eneo hilo lenye mizozo .

Hata hivyo juhudi zao hazikuwafurahiha watu miongoni mwa watu wao na Rabin ndiye aliyekuwa mwathiriwa wa kwanza wa kujaribu kuleta Amani kati ya nchi yake na Wapalestina . Wadadisi wanasema kuuawa kwa Rabin kulivunja kabisa matumaini ya kuweza kuafikia amani kati ya pande hizo mbili na ndio uliokuwa mwisho wa jitihada halisi za kuwapatanishaWaisraeli na Wapalestina

Mauaji ya Rabin

Mnamo tarehe 4 Novemba mwaka wa 1994 , Waziri mkuu wa Israel Yitzhak Rabin aliuawa kwa kupigwa risasi na Yigal Amir ambaye alitaka kuvuruga makubalino ya amani kati ya Waisraeli na Wapalestina . Rabin ndiye aliyekuwa kiongozi wa Israel aliyekuwa na uwezo wa kufanikisha kupatikana kwa Amani kati ya pande hizo mbili

Amir alitaka kuzuia Israeli kusalimisha ardhi katika Ukingo wa Magharibi ili idhibitiwe na Wapalestina; aliamini ardhi hiyo ni zawadi kutoka kwa Mungu kwa watu wa Kiyahudi ambayo haiwezi kuuzwa. Alifanikisha malengo yake.

Maafisa wa Israeli wakati huo walisema kuwa warithi wa Rabin walikuwa tayari kuzungumza. Ili kuendelea na mchakato wa amani .Hawakuweza kufanya makubaliano, walisema, kwani sio Yasser Arafat wala mrithi wake Mahmoud Abbas waliokuwa na uwezo wa kuleta maelewano muhimu kufanikisha kupatikana kwa amani.

Muuaji wa Rabin, Myahudi wa itikadi kali za kidini na mwanafunzi wa sheria aliyekuwa na miaka 20 hivi alikuwa na hakika kwamba alikuwa amepata ushindi wa kihistoria. Aliposhtakiwa kwa mauaji hayo, Amir alikiri kwa furaha kwamba alikuwa ameyatekeleza. Aliuliza glasi ya mvinyo ili aweze kufurahia mafanikio yake.

Miongoni mwa Wapalestina, wanamgambo huko Hamas tayari walikuwa wameanza kampeni ya kujitoa mhanga. Hawakutaka uhusiano wowote na Oslo, wakisema ni kujisalimisha na kwamba hakuwezi kuwa na maelewano ya eneo na serikali ya Israeli ambayo waliamini haifai kuwapo. Wasomi wengine wakuu pia walikataa mkataba huo

Kinachokubaliwa na wengi hata hivyo ni kwamba Iwapo kulikuwa na fursa ya kupatikana kwa Amani kati ya Israeli na Palestina basi fursa hiyo ilikuwa mwanzoni mwa mwaka wa 1995 .

Watu wenye misimamo mikali katika pande zote hata hivyo walikuwa na pingamizi na kwa upande wa Wayahudi ,Rabin alikuwa mtu ambaye alitishia uwezo wao kuendelea kukalia kimabavu maeneo waliyodai ni yao .

Rabin alikuwa kamanda anayeongoza katika vita vya uhuru vya Israeli mnamo 1948-49. Mnamo 1967, akiwa mkuu wa jeshi na jenerali mwandamizi wa Israeli, aliongoza vikosi vyao kwenye ushindi wao muhimu dhidi ya maadui wao waarabu

Katika siku sita, Israeli iliharibu vikosi vya jeshi za nchi za Jordan, Misri na Syria. Baada ya hapo, kama majenerali wengi wa Israeli, alikuwa ameingia kwenye siasa.

Mara tu mchakato wa amani wa Oslo ulipoanza, aliunga mkono mazungumzo hayo katika Bunge la Israeli, na kimataifa. Alipouawa ,yamkini alikufa na juhudi za uwezekano wa kupatikana kwa amani .

Yasser Arafat

Kwa miongo kadhaa Yasser Arafat alikuwa nguzo muhimu ya harakati za ya Wapalestina kujitawala.

Kwa wafuasi wake alikuwa mtu pekee aliye na uwezo wa kuweka matumaini ya Wapalestina hai na kuwa mstari wa mbele kuyatangaza maslahi yao kwa ulimwengu.

Kwa wakosoaji alikuwa gaidi aliyekuwa na nia mbaya ambaye aliwafelisha watu wake.

Alikuwa na umuhimu mkubwa kitaifa na wakati mwingine alionekana kama mzigo mkubwa kwa Wapalestina.

Wakati akiinua matumaini yao ya uhuru pia alionekana na wengine kama moja ya vizuizi kwa demokrasia ya Wapalestina na asasi za kiraia.

Juhudi zake kadhaa hata hivyo za kuhakikisha kwamba watu wake wanapata Amani nan chi yao hazikufua dafu na kifo chake kilizima kabisa matumaini hayo .

Ripoti moja ya Uswizi ilidai kwamba Arafat huenda aliuawa kwa sumu ya Polonium mwaka wa wa 2004 .Hata hivyo taarifa rasmi kuhusu kifo chake inasema aliaga dunia kwa ajili ya kiharusi kilichoababishwa na maradhi ya damu .

Mwili wake ulifukuliwa mwaka wa 2012 na matokeo ya vipimo na uchunguzi yalizidi kuonesha kwamba mwili wake ulikuwa na kiasi kikubwa cha sumu aina ya Polonium .Baadaye Israel ilinyooshewa kidole kuhusu mauaji yake lakini Tel Aviv ilikana vikali kuhusika na mauaji ya Arafat .

Wanasayansi - kutoka Kituo cha Hospitali ya Chuo Kikuu cha Vaudois (CHUV) huko Lausanne, Uswizi - walifanya uchunguzi wa kina wa rekodi za matibabu za Arafat, sampuli zilizochukuliwa kutoka kwenye mabaki yake na vitu alivyochukua kwenda hospitalini huko Paris alikokufia mnamo 2004.

Sampuli za kibaolojia zilijumuisha vipande vya mifupa ya Bw Arafat na sampuli za udongo kutoka karibu na maiti yake.

Wanasayansi walihitimisha kuwa matokeo yao "yanaunga mkono kwa wastani maoni kwamba kifo chake kilikuwa matokeo ya sumu na poloniamu-210".

Vifo vya viongozi hao wawili vilizima kabisa uwezekano wa uwezekano wa kupatikana kwa suluhisho la kudumu katika mzozo ambao hadi leo hii unaazidi kusababisha umwagikaji wa damu ya Wapalestina na Waisraeli .