Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Kufanya kazi kwa muda mrefu kunaua watu 745,000 kwa mwaka, utafiti umebaini
Kufanya kazi kwa saa nyingi kunasababisha vifo vya mamia ya maelfu ya watu kwa mwaka, kulingana na Shirika la Afya Duniani (WHO).
Utafiti wa kwanza kufanywa duniani unaonesha kuwa watu 745,000 walifariki dunia mwaka 2016 kwa sababu ya ugonjwa wa kiharusi na ugonjwa wa moyo kutokana na kufanya kazi kwa muda mrefu.
Ripoti hiyo ilibaini kuwa watu wanaoishi Kusini Mashariki mwa Asia na Magharibi mwa eneo la Pasifiki ndio walioathirika zaidi.
Shirika la WHO limesema kwamba huenda hali hiyo ikazorota zaidi kutokana na janga la virusi vya corona.
Utafiti huo umebaini kuwa kufanya kazi kwa saa 55 au zaidi kwa wiki kulihusishwa na hatari ya kupata ugonjwa wa kiharusi kwa asilimia 35 na hatari ya kupata ugonjwa wa moyo kwa asilimia 17 ikilinganishwa na kufanyakazi saa 35 hadi 40 kwa wiki.
Utafiti huo umeonesha kuwa Shirika la Wafanyakazi duniani (ILO) pia limeonesha kuwa karibu robo tatu ya waliofariki dunia kutokana na kufanya kazi kwa muda mrefu walikuwa katika umri wa makamo au wazee.
Mara nyingi, vifo hutokea baadaye, hata miongo kadhaa baadaye.
Wakati utafiti huo haukujumuisha kipindi cha janga la corona, maafisa wa WHO, Wamesema, mabadiliko ya hivi karibuni watu kufanya kazi nyumbani na kupungua kwa kasi ya uchumi huenda kumeongeza hatari zinazohusishwa na kufanyakazi kwa kipindi kirefu.
"Kuna ushahidi unaonesha kuwa nchi zinapofunga shughuli za kiuchumi, saa za kufanya kazi zinaongezeka kwa karibu asilimia 10," Afisa wa WHO Frank Pega amesema.
Ripoti hiyo inasema kufanya kazi kwa muda mrefu kulikadiriwa kuchangia karibu theluhi moja ya magonjwa yote yenye kuhusishwa na jambo hilo.
WHO imependekeza kuwa sasa wakati umewadia kwa waajiri kuchukua hatua wakati wanafuatilia hatari za kiafya kazini kwa wahudumu wao.