Mzozo wa Israel na Wapalestina:Jumapili ndefu kwa Wapalestina baada ya mashambulizi kuwaua zaidi ya watu 40

Maafisa wa Palestina huko Gaza wanasema Jumapili ilikuwa siku mbaya zaidi tangu mapigano ya sasa na Israeli yaanze.

Zaidi ya watu 40 waliuawa katika mashambulio ya hivi karibuni ya anga ya Israeli huko Gaza, maafisa huko wanasema.

Jeshi la Israel limesema wanamgambo wa Kipalestina wamefyatua makombora zaidi ya 3,000 nchini Israel katika wiki iliyopita.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres ameonya kuwa mapigano zaidi yanaweza kutumbukiza eneo hilo katika "mgogoro ambao hauwezi kuhimiliwa".

Aliomba kukomeshwa mara moja kwa vurugu "mbaya kabisa".

Mapema Jumatatu, ndege za kivita za Israeli zilizindua mashambulio 80 ya anga katika maeneo kadhaa ya Jiji la Gaza, muda mfupi baada ya wanamgambo wa Hamas kufyatua roketi nyingi kusini mwa Israeli.

UN pia imeonya juu ya uhaba wa mafuta huko Gaza ambao uinaweza kusababisha hospitali na vituo vingine kupoteza nguvu za umeme .

Lynn Hastings, naibu mratibu maalum wa Umoja wa Mataifa katika Mchakato wa Amani Mashariki ya Kati, aliiambia BBC kwamba ametoa wito kwa mamlaka ya Israeli kuruhusu UN kuleta mafuta na vifaa lakini aliambiwa haikuwa salama.

Maafisa wa Gaza walisema watu 42, wakiwemo wanawake 16 na watoto 10, walifariki katika mashambulizi ya Israel siku ya Jumapili.

Watu kumi, wakiwemo watoto wawili, wameuawa katika mashambulio ya roketi dhidi ya Israeli tangu mapigano yalipoanza Jumatatu iliyopita, Israeli ilisema.

Idadi ya jumla ya vifo huko Gaza sasa imefikia watu 188, wakiwemo watoto 55 na wanawake 33, na 1,230 wamejeruhiwa, kulingana na wizara ya afya inayosimamiwa na Hamas. Israel inasema makumi ya wanamgambo ni miongoni mwa waliokufa.

Nini kilifanyika siku ya jumapili?

Mashambulio ya angani ya Israeli yaligonga barabara yenye shughuli nyingi huko Gaza baada tu ya usiku wa manane siku ya Jumapili, na kusababisha angalau majengo matatu kuanguka na vifo kadhaa kutokea .

Hamas ilizindua makombora mengi kuelekea kusini mwa Israeli usiku na mchana.

Mamilioni ya Waisraeli walikimbia maeneo salama wakati ving'ora vilipokuwa vikilia . Wapalestina pia walijaribu kuchukua tahadhari, lakini katika eneo lenye watu wengi na lenye vifaa duni, wengi hawakuwa na pa kwenda.

Riyad Eshkuntana aliliambia shirika la habari la Reuters kuwa aliwalaza watoto wake wa kike katika chumba cha nyumba ambacho alidhani kilikuwa mbali zaidi na milipuko hiyo. Binti yake mmoja tu, Suzy, mwenye umri wa miaka sita ndiye aliyenusurika usiku huo. Mkewe na watoto wengine watatu walifariki.

"Nilikimbia kuwaangalia wasichana," akasema Bw Eshkuntana. "Mke wangu aliruka aliwakumbatia wasichana ili awatoe nje ya chumba, kisha shambulio la pili la angani lilipiga chumba ... Dari ziliharibiwa na nilikuwa chini ya kifusi."

Jeshi la Israeli baadaye lilisema lilikuwa limefanya shambulio kwenye mfumo wa handaki ya wanamgambo katika eneo hilo. Kuanguka kwa mahandaki kulisababisha nyumba zilizo juu kuanguka pia, na kusababisha majeruhi yasiyotarajiwa ya raia, ilisema.

Jeshi la Israeli linasema limekuwa likilenga viongozi na miundombinu inayohusishwa na Hamas.

Ilisema pia ilishambulia nyumba za kiongozi wa Hamas Yahya Sinwar na kaka yake Muhammad Sinwar, ambaye alitajwa kama mkuu wa vifaa na nguvu kazi ya harakati hiyo.

Haiwezekani walikuwa nyumbani wakati wa shambulio hilo kulingana na shirika la habari la Associated Press.

Wafanyikazi wa uokoaji wa Gaza walitumia siku nzima kujaribu kuwaokoa watu kutoka kwa vifusi baada ya mashambulizi

Wizara ya afya ya Palestina ilisema daktari alikuwa miongoni mwa waliokufa: Dk Ayman Abu Al-Ouf, mkuu wa tiba ya ndani katika hospitali ya Shifa na sehemu ya timu ya kupambaa na virusi vya corona .

Nchini Israeli, makombora ya Hamas yaligonga Ashkelon, Ashdod, Netivot na maeneo mengine ya katikati na kusini mwa Israeli. Hakukuwa na ripoti za majeruhi.

Jeshi la Israeli limesema limeshuhudia idadi kubwa zaidi ya mashambulio ya roketi katika eneo lake katika wiki iliyopita.

Mfumo wa ulinzi wa Iron Dome nchini umefaulu kuzuia roketi nyingi. Lakini zingine zilisababisha uharibifu wa magari na majengo, pamoja na sinagogi la Yad Michael huko Ashkelon, ambapo mlipuko ulisababisha shimo kubwa ukutani kabla ya ibada ya jioni kwa likizo ya Kiyahudi ya Shavuot. Hakuna mtu aliyeripotiwa kuumizwa na wenyeji walianza haraka kuondoa vitu vilivyoharibiwa ili huduma hiyo iendelee, kulingana na Times of Israel.

Je,Kuna uwezekano wa mapigano kusitishwa?

Akiwalaumu wanamgambo kwa mzozo huo. Bw Netanyahu alisema mashambulizi yataendelea kwa "muda mrefu kadri itakavyohitajika" na kila linalowezekana lilikuwa likifanywa ili kupunguza vifo vya raia.

Jumamosi, jeshi la Israeli lililipua Jengo la ghorofa katika Jiji la Gaza linalotumiwa na vyombo vya habari vya kimataifa baada ya kutoa ilani kwa waliokuwemo kuondoka .

Rais Biden alimwambia Bw Netanyahu aliendelea kuunga mkono haki ya Israeli ya kujilinda. Alielezea wasiwasi wake juu ya vifo kwa pande zote mbili na akataka waandishi wa habari walindwe.

Akizungumza na Rais Abbas, kiongozi huyo wa Marekani alisema amejitolea "kuimarisha ushirikiano wa Marekani na Palestina". Alisema pia mashambulizi ya roketi kutoka kwa Hamas ndani ya Israeli yanafaa kukomeshwa mara moja .

Rais Abbas, ambaye yuko katika Ukingo wa Magharibi, ana nguvu kidogo huko Gaza lakini Marekani imekataa kuzungumza na Hamas, ambayo inaiona kama kundi la kigaidi.

Nini kilifanyika katika mkutano wa Umoja wa Mataifa?

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lenye wanachama 15 halijaweza kukubaliana juu ya taarifa ya umma katika siku za hivi karibuni na hakuna iliyotolewa baada ya mkutano.

Marekani - mshirika mkubwa wa Israeli - ndio inayosita , ikiamini haingesaidia katika mchakato wa kidiplomasia.

Katika mkutano wa Jumapili, Balozi wa Marekani Linda Thomas-Greenfield alisema Marekani ilikuwa tayari kutoa msaada "ikiwa pande husika zitataka kusitisha vita" na imekuwa ikifanya kazi bila kuchoka kujaribu kumaliza mzozo huo.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Palestina, Riyad al-Maliki, alizungumza juu ya shambulio la Jumamosi kwenye kambi ya wakimbizi, ambalo liliwaua watu 10 wa familia moja, na mtoto mmoja wa miezi mitano kunusurika baada ya kutolewa kutoka kwa vifusi. "Israeli mara nyingi hutuuliza tujiweke katika viatu vyao," alisema, "lakini hawajavaa viatu. Wanavaa buti za kijeshi."

Kwa kujibu, Mwakilishi wa Kudumu wa Israeli, Gilad Erdan, alitoa mfano wa kifo cha msichana wa Kiarabu - Israeli wa miaka 10, aliyeuawa na roketi ya Hamas. Alisisitiza Israeli inaongeza kile alichokiita "juhudi za kishujaa" ili "kuvunja miundombinu ya kigaidi na kuepusha majeruhi ya raia".

Bwana Erdan alimaliza kwa kulitaka Baraza la Usalama kulaani Hamas bila shaka lakini alionya kuwa Israeli itachukua hatua zote muhimu kujilinda.