Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Zifahamu hatua sita zinazotumika kupandikiza mimba
Wizara ya Afya nchini Tanzania imetangaza kuwa hospitali kuu ya rufaa nchini humo ya Muhimbili inatarajiwa kuanza kutoa huduma za upandikizaji mimba kwa wanawake hivi karibuni.
Huduma hiyo ya kitabibu imekuwa ikitumika sehemu mbalimbali duniani kwa miongo minne sasa na katika miaka ya hivi karibuni imezidi kusogezwa katika hospitali za umma katika maeneo ambayo wananchi wake hawana uwezo wa kuipata huduma hiyo katika hospitali binafsi.
Mtoto wa kwanza kuzaliwa kwa kutumia njia ya upandikizaji wa mimba alikuwa ni Bi Louise Brown aliyezaliwa Julai 25 nchini Uingereza. Wazazi wake walihangaika kupata mtoto kwa miaka tisa bila mafanikio kabla ya kukutana na madaktari ambao waliwatumia katika majaribio ya njia hiyo na hatimaye kufanikiwa kupata mtoto.
Je, kupandikiza mimba ni nini?
Katika hali ya kawaida, mimba hutunga kupitia tendo la ndoa pale mbegu za kiume ama manii zinapoungana na yai la mwanamke.
Kupandikiza mimba, ama kwa kimombo In Vitro Fertilization (IVF) ni mchakato wa kuunganisha yai la mwanamke na mbegu za mwanaume nje ya mwili wa binadamu katika maabara na kisha kurudishwa kwenye mwili wa mwanamke ili mimba ikue.
Utaalamu huo uligunduliwa miongo minne iliyopita na wanasayansi watatu wabobezi wa magonjwa ya uzazi kutoka nchini Uingereza amabao walikuwa wanatafuta njia mbadala kwa wanawake wanaoshindwa kushika mimba kwa hali ya kawaida. Wanasayansi hao ni Profesa Robert Edwards, Dkt. Patrick Steptoe na Dkt. Jean Purdy.
Prof Edwards alifanikiwa kufanya urutubishaji wa yai na manii katika maabara mwaka 1968 lakini aliendelea kuboresha utafiti wake na Dkt. Steptoe na Dkt. Purdy mpaka mwaka 1977 walipokutana na Bw. John na mkewe Lesley Brown ambao walishindwa kupata mtoto kwa miaka tisa.
Kwa mujibu wa jarida la Science Daily, kufikia Julai 2018 takriban watoto milioni nane walikuwa wamezaliwa kwa kutumia utaalamu huo duniani kote.
Hatua sita zinazofuatwa kupandikiza mimba
Idara ya Huduma za Afya ya Uingereza (NHS) imeorodhesha hatua sita ambazo hufuatwa na madaktari wa masuala ya uzazi katika upandikizwaji wa mimba. Hatua zote sita hizo ni kwa upande wa wanawake. Kwa wanaume kuna hatua moja tu.
Hatua ya kwanza ni kusimamsha mzunguko wa kawaida wa hedhi. Katika hatua hii mwanamke hupewa dawa kwa njia ya kunusa ama sindano kwa muda wa wiki mbili. Hatua hii ni muhimu ili kuboresha ufanisi wa dawa za hatua inayofuata.
Hatua ya pili ni kuboresha uzalishaji wa mayai. Baada ya kusimamisha mzunguko wa kawaida wa hedhi, mwanamke hupatiwa homoni ya FSH ambayo inanchochea uzalishaji mkubwa wa mayai. Homoni hiyo hutolewa kwa njia ya sindano kwa siku 10 mpaka 12 mfululizo.
"FSH inaongeza idadi ya mayai ambayo ovari (mfuko ambao mayai huzalishwa kwenye mwili wa mwanamke) zako huzalisha . Hii inamaanisha mayai mengi zaidi yanaweza kuchukuliwa kwa ajili ya urutubishwaji. Uwepo wa mayai mengi yaliyorutubishwa, kliniki inakuwa na mawanda makubwa ya kuchagua kiini tete (embryo) cha kutumika katika matibabu yako," unaeleza mtandao wa Idara ya Huduma za Afya ya Uingereza (NHS).
Hatua ya tatu ni kukagua maendeleo ya hatua mbili za awali. Hospitalai hufanya vipimo mbalimbali ikiwemo kupiga picha (ultrasound) ya ovari zako na wakati mwengine hata vipimo vya damu. Saa 34 mpaka 38 kabla ya mayai ya mayai kuvunwa, mwanamke anayepitia matibabu haya huchomwa sindano ya mwisho ya homoni ambayo inasaidia mayai kukomaa.
Hatua ya nne ni kuvuna mayai kutoka kwenye mwili wa mwanamke. "Utapigwa ganzi kisha mayai yako yatavunwa kotoka kwenye ovari zako kwa kutumia sindano maalumu inayopitishwa kwenye uke. Upitishwaji wa sindano hiyo kutoka ukeni mpaka kwenye ovari unaongozwa kwa kutimia picha za ultrasound," inaeleza NHS.
Hatua hii huchukua dakika 15 mpaka 20 kukamilika. Baadhi ya wanawake hupata maumivu kidogo ya tumbo ama kutokwa na damu ukeni baada ya hatua hii.
Wakati hatua hii ikiendelea, hatua moja anayopitia mwanaume nayo hufanyika, ambapo hutakiwa kutoa manii na kuiwasilisha hospitali haraka iwezekanavyo ambapo wataalamu watachukua mbegu bora zaidi kwa ajili ya kuzitumia kwenye hatua ya tano ya mwanamke.
Hatua ya tano ni kurutubisha yai. Hatua hii inafanyika kwenye maabara ambapo wataalamu wanaunganisha yai na mbegu za mwanaume na yai la mwanamke.
Baada ya saa 16 mpaka 20 madaktari huangalia kama yai limerutubishwa vyema. Kwa kawaida hurutubisha zaidi ya yai moja ili kupata lile ambalo lina hali nzuri zaidi kwa ajili ya kulipandikiza katika tumbo la uzazi la mwanamke.
Mayai yaliyorutubishwa (kiini tete) huendelea kukua ndani ya maabara kwa muda wa siku sita kabla ya kuhamishiwa kwenye tumbo la uzazi ama kwa jina lengine mji wa mimba wa mwanamke.
Hatua ya mwisho ni kuhamisha kiini tete kutoka maabara mpaka mji wa mimba. Baada ya mayai kuvunwa, mama mjamzito mtarajiwa hupewa homoni maalumu ya kuuandaa mji wa mimba kuweza kubeba kiini tete. Kuhamishiwa kiini tete katika mji wa mimba hufanyika kwa kupitia mrija maalumu unaopitishwa kwenye uke wa mjamzito mtarajiwa.
Hatua hii ni rahisi kuliko ya kuvuna mayai, na hivyo kwa kawaida ganzi haihitajiki.
Utajuaje kama mimba imetunga?
Baada ya kiini tete kuhamishiwa kwenye mji wa mimba, hushauriwa kusubiri kwa takribani wiki mbili kabla ya kufanya kipimo cha mimba ili kuona kama matibabu hayo yamefanikiwa.
Baadhi ya hospitali hushauri kutumika kwa kipimo cha mimba cha kawaida cha mkojo ukiwa nyumbani na ukishapata majibu uwapelekee. Hospitali nyengine hutaka urejee kwa ajili ya kipimo cha damu ambacho kinatoa majibu ya uhakika zaidi.
Endapo mimba itakuwa imetunga, basi kliniki za kawaida kwa mama mjamzito huendelea mpaka pale atakapojifungua.
Si mara zote IVF hufanikiwa, na inapotokea hali kama hiyo, madaktari hutoa ushauri wa kitabibu na kupewa fursa ya kuamua kujaribu tena matibabu hayo baada ya muda.