Je maambukizi ya njia ya mkojo ni ugonjwa wa zinaa?

Maambukizi ya UTI yanawezwa baina ya wenzi au wanandoa, wanasema wataalamu

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Maambukizi ya UTI yanawezwa baina ya wenzi au wanandoa, wanasema wataalamu
    • Author, Dinah Gahamanyi
    • Nafasi, BBC Swahili

Maradhi ya njia ya mkojo (Urinary track Infections-UTIs), ni maambukizi ambayo baadhi ya watu wamekuwa wakiyafananisha na maradhi ya zinaa. Hii ni kutokana na kwamba maambukizi haya hushambulia na kuathiri sehemu zinazokaribiana na za siri au hata sehemu zenyewe za siri za mwanadamu. Lakini je, ukweli ni upi kuhusu maradhi haya na wataalamu wanasemaje?

BBC Idhaa ya Kiswahili imezungumza na muathiriwa wa UTI pamoja na daktari bingwa wa magonjwa ya uzaji pamoja na UTI.

Zainab Nkumbo Kayenga (sio jina lake halisi), ni mama wa watoto watatu mwenye umri wa miaka 32, ambaye alipitia changamoto kubwa wakati alipopata maambukizi ya UTI kwa mara ya kwanza.

''Nilipopata UTI kwa mara ya kwanza nilihisi maumivu makali upande wa chini wa tumbo, na nilipokuwa nikienda haja ndogo nihisi uchungu sana...nilidhani ni maumivu ya tumbo tu ya kawaida, nikahisi ni hali tu ya ujauzito, kwasababu ndio kwanza nilikuwa nimepata ujauzito. Lakini maumivu hayakuisha na baada ya siku chache nilianza kukojoa mkojo wenye damu, nikaanza kutoa harufu sehemu za siri, ikabidi niende hospitalini na kupewa dawa...ndipo nilipoambiwa nilikua ninaumwa UTI'''

Bi Zainab anasema katika kipindi hiki mumewe alimshuku kuwa alimletea ugonjwa wa zinaa:

''Kilikuwa ni kipindi kigumu sana kwani mume wangu alidhani nina ugonjwa wa zinaa na kuamua kunitenga na kunikasirikia na hata kutishia kuwa angeniacha. Hata hivyo daktari alimueleza kuwa alichokua akikidhania sicho'' Zainab aliiambia BBC kwa njia ya simu.

Wataalamu wanasemaje?

Dkt. Iganatius Kibe, daktari bingwa wa magonjwa ya uzazi nchini Kenya, anasema UTI ni ugonjwa ambao huwapata wanawake wengi na mara nyingi wanawake wajawazito wamekuwa wakiupata kutokana na mabadiliko ya homoni za mwili wakati mama anapopata ujauzito.

Hata hivyo anasema maambukizi haya ya njia ya mkojo yameongezeka zaidi nyakati hizi kwasababu wanawake wengi wamekuwa wakitumia mbinu mbalimbali za kusafisha sehemu zao za siri:

''Mara nyingi wanawake wanafikiria wanaume ndio wanawaletea ugonjwa huu wa UTI, kwasababu wanatumia vitu mbalimbali kusafisha sehemu zao za siri kama vile kemikali, avokado, maziwa ya mgando, yote haya yanaharibu tindikali asilia ambayo inasafisha sehemu ile ya siri ya mwanamke...matokeo yake tindikali hii tunaiita PH kwa lugha ya kitaalamu ikiisha pale unapata mwanamke anaanza anapata maambukizi ya kudumu ya UTI, kujikuna na kutoa maji maji ya harufu mbaya'' anasema Dkt. Iganatius Kibe.

Dkt Ignacius Kibe

Chanzo cha picha, Dkt Ignacius Kibe

Maelezo ya picha, Dkt Ignacius Kibe anawashauri wanawake kuacha kutumia vipotozi, kemikali na vitu vingine kusafisha sehemu za siri, ili kupepuka UTI

Dkt Kibe anasema maambukizi ya njia ya mkojo- UTIs, yamekuwa yakiibua mgogoro baina ya wenza au wanandoa huku wakilaumiana kila mmoja kumletea mwenzake ugonjwa wa zinaa.

''Tatizo hili nalishuhudia kila mara, hasa maambukizi haya ya UTI yanapogeuka na kuwa ugonjwa wa zinaa. Unapata UTI ilianza kama maambukizi ya kawaida yanayosababisha kuungua kwa kibofu cha mkojo na mirija ya mikojo, lakini baadaye hali hii inahamia katika sehemu za siri za mwanamke na kuziunguza hadi kwenye shingo ya uzazi na kusambaa hadi shemu nyingine na eneo zima la nyonga tunaita -Pelvic Inflammatory Disease . Inapofikia hapo mwanamke anaweza kumuambukiza mwanaume bakteria wale na hapo ndio unageuka kuwa ugonjwaa wa zinaa'' anasema Dkt Kibe.

Daktari anawashauri wanaume wenye wenzi waliopatwa na maambukizi ya UTI kuambatana na wake zao na kufanyiwa vipimo vya maabara kubaini iwapo wameambukizwa bakteria aina ya E.colli na aina nyingine za bacteria na hata virusi ili wawe na uhakika na afya zao.

UTI ni nini hasa?

Kulingana na madaktari bingwa wa magonjwa ya uzazi pamoja na, maambukizi ya njia ya mkojo husababishwa na vimelea au bakteria hatari ambao huzidi uwezo wa kinga ya mwili katika mfumo wa mkojo. Maambukizi haya yanaweza kuathiri mafigo, kibofu cha mkojo na mirija inayopita katikakati ya viungo hivyo.

Tafiti mbalimbali zinaonesha kuwa UTI ni mojawapo ya aina za maambikizi yanayowakumba watu wengi zaidi duniani na watu takriban milioni 8.1 hutembelea hospitali au kliniki kila mwaka kuwaona madaktari kutokana na maradhi haya.

Maambukizi ya mkojo yanaweza kugawanywa katika aina mbili ya njia ya juu ya mkojo na ya njia ya chini. Njia ya juu inajumuisha figo na mrija unaopeleka mkojo katika kibofu cha mkojo (ureter), na njia ya chini ya mkojo yenye kibofu cha mkojo na mrija unaoelekea sehemu ya nyonga.

Kwa wengi maambukizi ya njia ya mkojo husababishwa na bakteria aina E. coli , ambayo kwa kawaida hupatikana katika mfumo wa mmeng'enyo wa chakula.

Dalili za UTI

Mkojo mzito wenye harufu kali na damu ni moja ya dalili za maambukizi ya UTI
Maelezo ya picha, Mkojo mzito wenye harufu kali na damu ni moja ya dalili za maambukizi ya UTI

Dalili za maambulizi ya UTI zinategemea una umri gani, jinsia na ni sehemu gani imeathiriwa ya njia ya mkojo.

Dkt kibe anashauri ni vyema kwa mtu kufanyiwa vipimo vya maabara vya mkojo na damu kabla ya kupewa dawa za kutibu UTIs ili kubaini ni aina gani ya bakteria wanaosababisha maambukizi uliyonayo.

Dalili za kawaida za UTI ni pamoja na:

  • Haja ya kwenda haja ndogo kila mara
  • Kupanda kwa joto la mwili
  • Kuhisi baridi mwilini
  • Maumivu ya mgongo
  • Mkojo mzito wenye harufu kali na damu
  • Maumivu au muwasho unapokwenda haja ndogo
  • Kichefuchefu na kutapika
  • Maumivu ya misuli na tumbo

Hatari zake

Zaidi ya asilimia 50 ya wanawake wote hupata walau wakati mmoja maambukizi ya UTI maishani mwao

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Zaidi ya asilimia 50 ya wanawake wote hupata walau wakati mmoja maambukizi ya UTI maishani mwao

Zaidi ya asilimia 50 ya wanawake wote hupata walau wakati mmoja maambukizi ya UTI maishani mwao, huku asilimia 20 na 30 wakipata maambukizi ya mkojo yanayojirudia, zinasema tafiti mbalimbali.

Wanawake wajawazito wanakabiliwa na uwezekano mkubwa wa kupata maambukizi ya UTI kuliko wanawake wengine, lakini maambukizi hayo yanapotokea yana uwezekano mkubwa wa kusambaa hadi katika mafigo, Hii ni kwasababu ya mabadiliko mwilini wakati waujauzito yanayoathiri njia ya mkojo.

Maambukizi ya UTI miongoni mwa wanawake wajawazito yanaweza kusababisha hatari ya afya za wakinamama wajawazito na watoto na hivyo DKT anasharu kuwa wanawake wajawazito wanapaswa kufanyiwa vipimo kubaini uwepo wa bakteria katika mkojo wao, hata kama hawana dlili na kutibiwa kwa dawa za abitiotics kuzuia usambaaji wa bakteria hao.

Ni nani anayeweza kupata UTI?

Wanaume ambao hawajahiriwa wanakabiliwa na uwezekano mkubwa zaidi kuliko wanaume waliotahiriwa

Chanzo cha picha, iStock

Maelezo ya picha, Wanaume ambao hawajatahiriwa wanakabiliwa na uwezekano mkubwa zaidi kuliko wanaume waliotahiriwa

Watu wa rika zote na jinsia zote wanaweza kupata maambukizi haya ya njia ya mkojo. Hatahivyo, baadhi ya watu wana hatari ya kupata. Mambo yafuatayo yanaweza kuongeza uwezekano wa kusababisha UTI:

  • tendo la kujamiiana hususan linapofanyika mara kwa mara na linapojfanywa na wenza zaidi ya mmoja au wapya
  • kisukari
  • uchafu wa mwili
  • kutomaliza mkojo kabisa katika kibofu unapokojoa
  • utopata kinyesi
  • kuziba kwa mirija ya mikojo
  • mawe kwenye figo
  • matumizi ya baadhi ya tembe za kuzuia mimba
  • wanawake waliopitisha umri wa kujifungua
  • watu waliofanyiwa upasuaji wa njia ya mkojo
  • kinga dhaifu ya mwili
  • kutotembea kwa muda mrefu
  • Matumizi ya muda mrefu ya dawa za antibiotics, ambazo zinaweza kuvuruga bakteria asilia wazuri wa mfumo wa haja kubwa na njia ya mkojo.

Athari zake

Mambukizi mengi ya njia ya mkojo huwa sio makali, lakini baadhi yanaweza kusababisha matatizo makubwa, hususan yanaposhambulia sehemu ya juu ya njia ya mkojo.

Maambukizi ya UTI yanaweza kuathiri figo yasipotibiwa haraka

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Maambukizi ya UTI yanaweza kuathiri figo yasipotibiwa haraka

Ugonjwa wa muda mrefu wa figo au unaorejea rejea unaweza kusababisha uharibifu wa kudumu, na baadhi ya maambukizi ya ghafla ya figo yanaweza kutishia maisha, hususan ni kama bakteria wataingia kwenye mfumo wa damu hali inayofahamika kama epticaemia kwa lugha ya kitaalamu.

Pia huongeza hatari ya wanawake kujifungua vijusi au wenye uzito wa chini wanapozaliwa.

Je unaweza kuzuia?

Kuna hatua mbalimbali ambazo zikichukuliwa zinaweza kupunguza hatari ya kupata maambukizi ya UTI. Kulingana na Dkt Ignatius Kibe njia kuu ya kuzuia maambukizi ya njia ya mkojo ni pamoja na kuacha kutumia vipodozi, mafuta, losheni, manukato, kemikali na vitu vingine kusafisha sehemu za siri.

''Sisi madaktari hatutaki mwanamke aweke tindikali sehemu zake za siri, tindikali ya mwili asilia iliyopo kwenye njia za mkojo na uke inatosha...wanawake waache kabisa'', alisisitiza Dkt Kibe na kuongeza kuwa: ''Hiyo sehemu iachwe tusije tukaiharibu kwa kuoshwa na makemikali hatutaki kamwe!. Dawa zinazonunuliwa na kuweka sehemu za siri ziachwe!'', alisema.

Hatua mbali mbali ambazo zikichukuliwa zinaweza kupunguza hatari ya kupata maambukizi ya UTI:

  • Kunywa maji mengi na uende haja ndogo mara kwa mara ili kusafisha njia ya mkojo
  • Epuka vinywaji kama vile pombe na kahawa ambavyo vinaweza kudhuru kibofu.
  • Nenda haja ndogo mara baada ya kufanya tendo la ngono.
  • Jipanguse kuanzia mbele kwenda nyuma baada ya kwenda haja ndogo na kubwa.
  • Hakikisha sehemu zako za siri ni safi kila wakati.
  • Kuoga kwa maji yanayotiririka( showers) ni bora zaidi na epuka kutumia mafuta.
  • Pedi (sodo) zinazotumiwa nje ni bora zaidi kuliko zile zinazoingizwa ndani
  • Epuka kutumia bidhaa za manukato katika sehemu ya siri.
  • Vaa nguo ya ndani(chupi) iliyotengenezwa kwa pamba na nguo ambazo hazikubani ili kuhakikisha sehemu zako za siri zinakua karibu.
  • Watu wanashauriwa kuwasiliana na madaktari iwapo watahisi kuwa na dalili za UTI, hususan kama wana uwezekano wa kupata maambukizi ya figo.

Maambukizi ya UTI kwa wanaume.

Wakati wanaume wanapopata UTI, huathiri viungo sawa na maeneo sawa na ya wanawake

Chanzo cha picha, iStock

Maelezo ya picha, Wakati wanaume wanapopata UTI, huathiri viungo sawa na maeneo sawa na ya wanawake

UTI ni maambukizi ya nadra kwa wanaume. Wanaume wenye chini ya umri wa miaka 50 wanaopata maambukizi haya ni kati ya 5 na 8 katika kila wanaume 10,000 zinasema tafiti. Hatari ya maambukizi haya huongezeka kutokana na umri.

Wanaume wanapopata maambukizi ya njia ya mkojo huathirika maeneo sawa na ya wanawake.

Kwa wanaume, hatahivyo, saratani ya korodani pia husababisha hatari ya maambukizi ya UTI.

Mwanaume aliyetahiriwa ana uwezekano mdogo zaidi wa kupata maambukizi ya njia ya mkojo kuliko mwanaume ambaye hajatahiriwa.

Mchakato wa matibabu utakuwa sawa na ule unaopitiwa wanawake wenye maambukizi ya mkojo.