Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Idriss Deby: Mgawanyiko katika familia ya Deby yaitia Chad katika hali tete wakati huu wa mpito
Uhamisho uliotekelezwa wa mamlaka kwa haraka nchini Chad kwa Jenerali Mahamat Idriss Deby baada ya kifo cha baba yake unaonekana kutishiwa na mgawanyiko ndani ya ukoo wa rais na mivutano katika jeshi ambayo inaweza kuwa na matokeo mabaya kwa mustabali wa taifa hilo.
Marehemu Idriss Deby Itno alikuwa ameimarisha nguvu kimkakati wakati wa urais wake wa miaka 30 kwa kujizunguka na washirika kutoka kwa kabila lake la Zaghawa.
Jambo muhimu zaidi, alipeana majukumu ya serikali kwa wanafamilia na mkakati huo umesababisha mapambano ya nguvu ambayo vyombo vya habari nchini Chadi vinafuatilia kwa karibu.
Uhasama ndani ya familia
Mahamat Deby alitajwa katika hali tata kuwa kiongozi wa Baraza la Mpito la Jeshi (CMT) katika tangazo hilo hilo la kifo cha baba yake mnamo Aprili 20.
Sasa anaongoza timu ya washiriki 15 ambayo imetangaza itasimamia kipindi cha mpito cha nchi hiyo kwa miezi 18 ijayo.
Lakini kuonekana kwa ufanisi kunatishiwa na ripoti za vyombo vya habari za kuwepo hila za ikulu, ambazo zinatishia hali thabiti siku zijazo nchini Chad.
Mnamo tarehe 21 Aprili, vyombo vya habari vya Chad viliripoti kwamba kulikuwa na ugomvi kati ya Mahamat Deby na kaka yake, Zakaria Idriss Deby katika ikulu ya rais.
Ripoti zilisema ugomvi huo ulikuwa juu ya urithi wa baba yao na uvumi kwamba lilikuwa tikipo la 'ufyatulianaji wa risasi lilikataliwa na mwanachama mwandamizi wa CMT ambaye alikosoa ripoti hizo kama majaribio ya "kuyumbisha mfumo".
Mtu wa wake wengi
Marehemu Idriss Deby alikuwa na wake kadhaa na angalau watano kati yao wamejitokeza katika ripoti mbali mbali za vyombo vya habari nchini Chad. Wao ni Anda Ali Bouye; Zina Wazouna Ahmed Idriss; Amani Musa Hilal, Hadja Halime na Hinda Deby Itno. Maarufu zaidi kati yao ni Hinda Deby.
Hinda Deby
Binti wa mwanadiplomasia wa ngazi ya juu wa Chad, Hinda Deby Itno, 41, aliwahi kuwa katibu wa kibinafsi wa Idriss Deby kabla ya kuacha kazi hiyo ili kuzingatia wakfu wake, Grand Coeur.
Pamoja na ndugu zake walioajiriwa katika Ofisi ya rais, aliweza kushawishi uteuzi na kufutwa kazi kwa watu serikalini.
Ndugu yake, Khoudar Mahamat Acyl, aliwahi kuwa msaidizi wa marehemu rais Deby.
Inasemekana alikuwepo wakati Deby alipojeruhiwa vibaya katika vita na waasi huko Kanem, kaskazini mwa mji mkuu N'Djamena.
Ndugu zake wengine, Hissein Massar Hissein, Mahamat Issa Halikimi na Ahmat Khazali Acyl hapo awali walishikilia nafasi za baraza la mawaziri, wakifanya kazi kama mawaziri wa afya, haki na elimu mtawaliwa.
Hinda Deby ana uraia wa nchi mbili -Ufaransa na Chad. Watoto wake watano, ambao wote walizaliwa huko Neuilly-sur-Seine, karibu na Paris pia wana uraia wa nchi hizo mbili.
Alisemekana kuwa mdau muhimu katika sekta muhimu ya mafuta ya Chad.
Tangu Chad iwe taifa linalozalisha mafuta mnamo 2003, sekta hiyo imekuwa ikidhibitiwa na jamaa zake na watu wa ndani walio karibu naye katika nyakati tofauti tofauti.
Hinda pia ni Balozi Maalum wa UNAIDS.
Wakati wa kampeni za uchaguzi wa urais wa Aprili 11, Hinda aliwahimiza vijana na wanawake kumpigia kura Deby kupitia wakfu wake.
Zakaria Idriss Deby
Sawa na ndugu yake mdogo Mahmat, Zakaria Idriss Deby anasemekana alikuwa karibu na baba yake. Mama yake ni Anda Ali Bouye na anasadikiwa kuwa miongoni mwa wale waliopigiwa upatu kumrithi.
Zakaria alisomea shria ya biashara nchini Tunisia na baadae kupata mafunzo katika wizara ya mambo ya kigeni ya Chad kabla ya kuteuliwa naibu mkurugenzi wa mkuu wa baraza la mawaziri. Nafasi hiyo awali ilishikiliwa nan a watoto wengine wawili wa Deby - Amira Idriss Deby na Abdelkerim Idriss Deby.
Mwaka 2017, aliteuliwa kuwa Balozi wa Chad katika Muungano wa Milki za Kiarabu,UAE.
Pia alihudumu kama rais wa vijana wa vuguvugu la chama tawala Patriotic Salvation Movement (MPS).
Abdelkerim Idriss Deby
Abdelkerim alizaliwa mwaka 1992, na alifuzu katika chuo cha Marekani cha mafunzo ya kijeshi (USMA) katika eneo la West Point mwaka 2015.
Aliteuliwa kwa naibu mkuu wa utumishi wa umma katika ofisi ya rais Julai mwaka 2019.
Mwezi SeptembA mwaka 2020, Abdelkerim aliongoza ujumbe wa Chad uliokutana na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu kujadili "uwezekano wa kufungua" ubalozi wa Chad mjini Jerusalem.
Netanyahu alikuwa ametangaza kufufuliwa upya kwa uhusiano wa kidiplomasia wa Israel na Chad mwezi Januari 2019 - baada ya kutengana kwa miaka 46- wakati wa ziara yake mjini N'Djamena, ambapo alikutana Idriss Deby.
Mivutano ya urithi
Ushindani kati ya Mahamat na Zakaria uliongezeka mnamo Januari 2020 wakati marehemu rais Deby aliripotiwa kuugua na kumwacha Hinda kwa muda katika uongozi wa nchi hiyo ya Afrika ya kati.
Kulingana na vyombo vya habari vya Chad, Hinda Deby aliongoza mikutano ya ngazi ya juu ya serikali na kuwakaribisha wageni kutoka nje. Tovuti ya Zoom Tchad ilisema Rais Deby alimwachia mkewe madaraka wakati huo ili kuzuia mzozo kati ya ndugu hao wawili.
"Mpango wa Idriss Deby kumweka mkewe ili kudumisha madaraka yake ni muhimu kwa sababu hakuchagua mmoja wa wanawe.
Hii pia ingefungua mlango wa uhasama na vita vya kurithiana, "tovuti hiyo ilisema.
Athari za malumbano ya kifamilia
Inawezekana kwamba ugomvi juu ya urithi wa Deby unahusisha zaidi ya wanafamilia na haitashangaza kugunduliwa kwamba majenerali wakongwe katika jeshi pia wanahusika na mzozo huo.
Jumbe za twitter za tovuti ya Tchadinfos zinazokanusha kuwa "hakukuwa na shambulio la risasi huko Palais Rose na hakuna ugomvi" kati ya Mahamat na Zakaria zilimtaja mwanafamilia, labda aliyetaka kuwasilisha umoja wa familia hiyo wakati inapokabiliwa na kutojua kinachofuata.
Lakini mivutano ya familia imekuwa siri iliyofuchuka.
Kuna pia ishara za kugawanyika ndani ya jeshi, ambazo zilifunuliwa wakati Jenerali Idriss Abderamane Dicko alipokataa kuundwa kwa baraza la jeshi. Dicko, kiongozi wa zamani wa waasi, anasemekana kuwakilisha wanajeshi ambao wanapinga uongozi wa Mahamat Deby.
Dicko "anasema kuwa baraza hili la kijeshi ni kikundi cha marafiki wachache". Anataka mashauriano ya kina yafanyike haraka "kabla ya nchi kuingia kwenye machafuko", tovuti ya Tchadanthropus iliripoti.
Ikiwa kweli familia ya Deby na maafisa waandamizi zaidi wa jeshi wanapinga uongozi wa Mahamat, mivutano inaweza kuhatarisha juhudi za baraza hilo la mpito kutuliza Chad wakati wa kuna hofu kuhusu kipindi cha mpiito cenye mengi yasiyojulikana.