Mike Sonko: Kupanda na kushuka kwa gavana wa zamani wa jiji kuu la Kenya Nairobi

Muda wa kusoma: Dakika 6

Katika kuporomoka kutoka madaraka ya juu hadi kuwa raia wa kawaida , gavana wa zamani wa mji mkuu wa Kenya Nairobi sasa anakabiliwa na mashitaka mengi ya jinai yakiwemo utakatishaji fedha na ugaidi. Je ,Mike Sonko ni nani na aliibukaje kuwa mmoja wa wanasiasa mashuhuri wa Kenya?

Anajulikana kwa maisha yake ya mtindo wa kisasa, nguo za kupendeza na vito vya bei ghali, Gidion Mbuvi Kioko alipata jina la utani la Sonko - msimbo wa Kiswahili kumaanisha tajiri - baada ya mazoea ya kuwapa hadharani pesa wafuasi wake katika makazi ya mabanda ya Nairobi.Jina lilikwama.

Muda mrefu kabla ya kuingia kwenye siasa na kupewa jina hilo la utani, alifungwa jela miaka ya 1990 kwa kesi ya udanganyifu wa ardhi. Alifanikiwa kutoroka kutoka gerezani kwa kuwahonga walinzi wake, kabla kukamatwa na kurudishwa gerezani.

Baada ya kuachiliwa, alianzisha biashara zilizofanikiwa ikiwa ni pamoja na matatu (magari ya usafiri wa umma ), kampuni ya ujenzi na uuzaji wa nyumba na eneo la burudani huko Nairobi, na sasa alikuwa na pesa na ujasiri wa kujitosa kwenye siasa.

Akiwa na umri wa miaka 35 alikua mbunge mnamo 2010, kisha akawa seneta miaka mitatu baadaye kabla ya Bw Sonko kupigiwa kura kama gavana wa Nairobi mnamo 2017.

Kupanda kwake kuliwashangaza wengi na palikuwa na matumaini makubwa kwamba angeongoza mabadiliko ya mji mkuu kama alivyoahidi, licha ya elimu ya kiwango cha wastani kwani alisoma tu hadi kiwango cha sekondari.

Alikuwa na ustadi wake kuelewa siasa za jiji na kuepuka changamoto nyingi huku akionekana kuelewa shida nyingi za jiji.

Na kwa wale ambao walitilia shaka uwezo wake, alikuwa na afisa mkuu mtendaji wa zamani wa kampuni ya mafuta kama naibu gavana kumsaidia kutekeleza mipango yake mikubwa ya jiji.

Sare za Jeshi

Lakini kama vile kupanda kwake kulikuwa kwa njiaya kipekee basipia kuanguka kwake kulikuwa na kishindo .. Alishtakiwa mnamo Desemba kwa utovu wa nidhamu na kutumia vibaya mamlaka ya ofisi yake.

Bwana Sonko pia anakabiliwa na mashtaka mengi kortini, pamoja na kesi kadhaa za ufisadi, kumshambulia mtu na makosa yanayohusiana na ugaidi. Anayakana yote.

Anadaiwa kuiba zaidi ya shilingi milioni 300 ($ 2.7m; £ 1.9m) kupitia utoaji mbovu wa kandarasi kwa kampuni za marafiki zake ambao inasemekana walirejesha sehemu ya fedha hizo katika akaunti zake za benki bada ya kupokea malipo yao.

Taarifa zaidi kumuhusu Mike Sonko:

Hivi majuzi pia alishtakiwa kwa kuajiri na kuwapa silaha wanamgambo, kupata mavazi ya kijeshi yanayohusiana na makundi ya kigaidi na kufadhili shughuli za ugaidi.

Picha yake na walinzi wake wa kibinafsi akiwa amevalia mavazi ya kijeshi kwenye jukwaa la umma, ambayo inasemekana alichapisha kwenye kurasa zake za mitandao ya kijamii, ni sehemu ushahidi katika kesi inayomkabili.

Haijajulikana Bwana Sonko atashtakiwa lini - anakabiliwa na mashtaka mengi, ambayo mengine ni ya tangia mwaka wa 2019.

Yeye na wafuasi wake wanasema mashtaka hayo yanachochewa kisiasa na yana dhamira ya kumtisha.

Uhusiano wake na Rais

Mnamo mwaka wa 2014, wakati maafisa wa kitaifa walipotuma tingatinga kubomoa nyumba za makazi zinazodaiwa kujengwa kwenye ardhi ya umma jijini Nairobi, Bw Sonko, wakati huo alikuwa seneta wa jiji hilo, alikimbilia eneo la tukio.

Sehemu ya umati wa watu ilikuwa ikitazama kwa kukata tamaa, ikiona uwekezaji wao ukiangushwa ardhini.

Seneta huyo alimpigia simu Rais Uhuru Kenyatta, na kumweka kwenye spika: "Mheshimiwa, bwana," seneta huyo alisema, "hapa mtaani Balozi ,nyumba zenye thamani ya mabilioni ya pesa zinaharibiwa."

"Nani anazibomoa?" rais aliuliza.

"Ni waziri wa kilimo ... nilikuwa nimemwandika barua na alinihakikishia kwamba hatafanya hivyo.

Yuko hapa na sasa nyumba zinaangushwa' Bwana Sonko alijibu.

Rais alisema atasimamisha ubomoaji. Umati ulipiga kelele kwa furaha.

Muda mfupi baadaye waziri huyo alithibitisha kwamba alikuwa ameamrishwa asimamishe ubomoaji huo, hadi mzozo wa ardhi utatuliwe.

"Rais ni rafiki yangu. Nilimuweka kwenye simu ya spika kwa sababu nina imani naye - ndiye rais anayeweza kupatikana kwa urahisi zaidi ulimwenguni," Bw Sonko alisema wakati huo.

Kwa ushawishi wake wote huo na kuwa karibu na mamlaka Bwana Sonko alikuwa amefanya siasa kwa chini ya miaka mitano .

' Nilikuwa mhalifu na niliwahi kuwa mfungwa'

Bwana Sonko alianza safari yake ya kisiasa mnamo 2010, wakati alipogombea uchaguzi mdogo wa ubunge.

Alikuwa mtu asiyejulikana katika siasa, lakini alikuwa tajiri na mkali - alitumia pesa zake na kujipendekeza kwa watu wengi. Alishinda kwa urahisi.

Tabia isiyo ya kawaida ya Bwana Sonko imekosolewa mara nyingi.

Mnamo mwaka wa 2011, kama mbunge mpya, aliondolewa bungeni kwa kuvaa vipuli na miwani za rangi. "Ninawakilisha vijana ambao walinichagua bungeni," aliiambia BBC. Alisema atapambana kubadili sheria za mavazi, ingawa hakufanikiwa.

Kama mbunge, alishiriki katika maandamano mbali mbali, ambayo mara moja alishuhudiwa akibingiria barabarani akiwa amejilaza na kupiga ukuta ngumi . Alitumia shirika lake la kibinafsi kutoa huduma za bure wakati alipokuwa seneta hatua iliyomfanya kukosolewa kwa kutaka kumhujumu gavana wa wakati huo

Wakati mwingine alirekodi mazungumzo ya faragha na kuyachapisha kwenye mitandao ya kijamii, akijipatia jina "msanii wa kurekodi".

Hata kama gavana, vituko vyake viliendelea. Wakati janga la corona lilipofika Kenya, alikosolewa kwa kuingiza chupa ndogo pombe ya Hennessy katika vifurushi vya chakula vilivyopewa wakazi waliohitaji misaada Nairobi.

"Imeaminika kuwa pombe ina jukumu kubwa katika kuua coronavirus," alisema. Shirika la Afya Ulimwenguni hata hivyo linaonya kuwa kunywa pombe kunaweza kudhoofisha kinga ya mwili.

Pamoja na tabia zake hizo, rekodi yake ya zamani ya uhalifu imeibuka katika majadiliano ya umma juu ya uadilifu wake, haswa kwa kuzingatia umaarufu wake na kupanda kake katika madaraka ya kisiasa

Mnamo mwaka wa 2012, Kamati ya Haki ya Utawala nchini Kenya - ofisi ambayo inachunguza malalamiko dhidi ya mashirika ya umma na maafisa wa serikali - ilimuorodhesha Bw Sonko kati ya wanasiasa waliodhamiriwa kuwa "hawafai kuidhinishwa kugombea uchaguzi kwa ajili ya dosarikuhusu hadhi zao na uadilifu.

Bw, Sonko amekuwa akipuuza ukosoaji kama huo.

"Wakosoaji wangu wananiita mhalifu… ndio mimi nilikuwa mfungwa, nilikuwa mhalifu hapo zamani, lakini leo mimi ndiye gavana wa jiji hili kubwa," alisema mnamo 2019.

'Alifeli kuliendesha jiji'

Wakati Bwana Sonko alipoapishwa mnamo 21 Agosti 2017, aliahidi kuwa jiji halitawahi kuwa sawa tena.

"Nitafanya kazi usiku kucha kuhakikisha huduma bora zinatolewa kwa wakati kwa wakazi wote' alisema.

Lakini njia yake ya uongozi isiyo ya kawaida na usimamizi wake tata zilisababisha kujiuzulu, kufutwa kazi na kukosana mara kwa mara kwa maafisa wa jiji.

Ahadi kwamba gavana angebadilisha kaunti haikutumizwa.

"Sonko hakujua jinsi ya kusimamia mifumo rasmi ya serikali na anaondoka kwa njia ile ile alioingia pamoja na sarakasi zake' alisema baadaye Seneta Isaac Mwaura .

Baadaye Sonko alisaini hati za kusalimisha baadhiya majukumu ya serikali ya kaunti kwa Mamlaka ya jiji la Nairobi inayosimamiwa na jenerali wa kijeshi .

Wakati wa kuzisaini hati hizo agizo la mahakama ilikuwa limetolewa asiingi ofisini make.Pia alikabiliwa na tishio la kura ya kutokuwa na Imani naye

Ingawa Bwana Sonko hapo awali alitangaza alikuwa amekabidhi madaraka yake kwa hiari, alipigana mara kwa mara ili arejeshewe tena, wakati mmoja akidai kwamba alikuwa amedanganywa.

Rais Kenyatta alisema gavana huyo alishindwa kutawala mji huo, na alikuwa ametoa NMS kumsaidia.

"Nilimwambia rafiki yangu Sonko, ikiwa unahitaji msaada nitajaribu kupata mtu, lakini alijikita katika kuvalia miwani na kujisifu juu ya kazi aliyosema alikuwa akifanya," rais alisema hivi karibuni.

Rais anasema alianzisha mchakato wa kuondolewa kwa Bwana Sonko juu ya mtindo wake wa usimamizi na kutofanya kazi

Ulikuwa mwisho wa kutamausha kwa wale ambao walitamani mabadiliko ya kweli na waliamini kwamba utawala wa Bw Sonko ungeyaleta.

Alikuwa ameahidi huduma bora - na wakati akitaja mafanikio kadhaa, pamoja na kurudisha ardhi ya umma na kujenga barabara, kwa wengi ilionekana kuwa mbwembwe .

Asili yake ya kutoa suluhu za haraka na takrima ambazo mwanzoni ziliwapendeza baadhi ya watu zilimaanisha uwajibikaji mdogo kwa ahadi ambazo alikuwa amewaambia waliomchagua.

Sasa ameachishwa majukumu ya ofisi ya umm na ana muda mwingi wa kujiandaa kwa changamoto nyingi za kisheria ambazo ziko mbele.