Mzozo wa Msumbiji: Kwanini wanajeshi wa Marekani wamo nchini humo?.

Kuongezeka kwa mashambulio ya wanamgambo katika mkoa wa kaskazini mwa Msumbiji wa Cabo Delgado kumelazimisha serikali kutathmini mkakati wake dhidi ya waasi wa Kiisilamu.

Imewaalika washauri wa jeshi la Marekani kusaidia vikosi vyake katika vita hivyo

Jukumu la vikosi vya Marekani ni nini?

Makubaliano kati ya serikali ya Msumbiji na Marekani ni kwa wanajeshi wa Marekani kutoa mafunzo kwa vikosi vya wenyeji wanaopambana na wanamgambo wa Al-Shabaab - wanaominika kuwa na uhusiano na kundi la Islamic State (IS).

"Vikosi vya operesheni maalum vya Marekani ... vitaunga mkono juhudi za Msumbiji za kuzuia kuenea kwa ugaidi na misimamo mikali," ubalozi wa Marekani nchini Msumbiji ulisema mnamo Machi 15.

"Ni wazi, Marekani inajaribu kupanua ushawishi wake," anasema Jasmine Opperman, mchambuzi wa Mradi wa Takwimu za Maeneo ya Migogoro na Matukio (Acled), ambayo inafuatilia vurugu za kisiasa ulimwenguni.

Lakini anaongeza kuwa ni mzozo mgumu wa huko, na kwamba "Marekani inarahisisha jambo hilo kuonekana jepesi kwa kuwataja [wanamgambo] hao kama sehemu ya Islamic State ".

Mnamo Machi 10, serikali ya Marekani iliitaja al-Shabaab nchini Msumbiji kama "shirika la kigaidi la kigeni", ikilielezea kama mshirika wa IS.

Ureno, iliyokuwa mtawala wa kikoloni wa Msumbiji, pia imejitolea kuwapa mafunzo wanajeshi.

"Tutatuma wafanyikazi wa kutoa mafunzo takriban 60 nchini Msumbiji kufundisha wanajeshi wa majini na makomando," afisa wa Ureno alisema.

Ijapokuwa serikali ya Msumbiji iko kimya kuhusu kukubali uwepo wao, makandarasi wa jeshi la kibinafsi wamekuwa wakifanya kazi katika mkoa huo pamoja na vikosi vyake vya usalama.

Hapo awali mnamo 2019, mamluki wa Urusi kutoka kikundi cha Wagner walikuwa wakiendesha shughuli katika eneo hilo

Hivi majuzi, Kikundi cha Ushauri cha Dyck chenye makao yake Afrika Kusini DAG) kiliaminika kualikwa na serikali ya Msumbiji kuisaidia kupambana na waasi.

Ripoti ya hivi karibuni ya Amnesty International juu ya ukiukwaji wa haki za binadamu uliofanywa huko Cabo Delgado ilihusisha kundi hili pamoja na vikosi vya serikali, na wanamgambo katika mauaji ya kiholela ya raia.

DAG inasema inachunguza madai yaliyotolewa dhidi yake.

"Unaposikia tuhuma hizi za majeruhi ya raia zinazohusisha wakandarasi wa jeshi la kibinafsi, inaiweka serikali katika picha mbaya," anasema Emilia Columbo, mshirika mwandamizi katika Kituo cha Mafunzo ya Kimkakati na Kimataifa cha Washington.

Kuna wasiwasi pia juu ya ufanisi wa wakandarasi hawa wa kibinafsi.

Kaimu mratibu wa kukabiliana na ugaidi wa Marekani John Godfrey amesema kuhusika kwa mamluki "hakujasaidia" serikali ya Msumbiji katika kukabiliana na tishio linalowakabili kutoka kwa wanamgambo.

Ni kipi kinachoskuma mzozo huu ?

Cabo Delgado kwa muda mrefu ni jimbo ambalo kwa muda mrefu limekuwa bila utulivu, lakini kuongezeka kwa vurugu zinazohusiana na wanamgambo wa Kiislamu zilianza mnamo 2017.

Ni mkoa ulio na umaskini mkubwa na kuna malalamiko juu ya upatikanaji wa ardhi na ajira.

Lakini umuhimu wa Cabo Delgado kwa serikali, na sababu zaidi ya malalamiko ya ndani, iko katika akiba tajiri ya gesi asilia inayochimbwa hivi sasa pwani mwa eneo hilo kwa kushirikiana na kampuni za nishati za kimataifa.

Inaonekana kwamba wanamgambo hao wamepata mafanikio makubwa katika kupata makurutu kutoka kwa mkoa huo na zaidi.

"Ningesema kulingana na jinsi walivyoenea haraka, inazungumzia ongezeko kubwa la usajili ", anasema Emilia Columbo.

"Tunapata ripoti za boti zilizojaa vijana kukamatwa wakati wanapoelekea Cabo Delgado."

Acled imerekodi zaidi ya visa 570 vya vurugu kutoka Januari hadi Disemba mwaka wa 2020 katika jimbo hilo.

Hizi ni pamoja na mauaji, kukatwa vichwa na utekaji nyara, na vifo kutoka kwa mashambulio yaliyofanywa na vikundi vyote vilivyohusika katika mzozo kuongezeka sana mwaka jana.

Tukio la kutisha zaidi lilikuwa la watu 50 kukatwa vichwa katika uwanja wa michezo katika kipindi cha wikendi.

Makundi ya haki za binadamu yameripoti uharibifu mkubwa wa majengo kote kaskazini mwa Msumbiji na wanamgambo. Ukosefu wa utulivu umesababisha idadi kubwa ya watu kutoroka makazi yao katika maeneo ambayo mzozo umezuka.

Karibu watu 670,000 walikuwa wakimbizi wa ndani katika majimbo ya Cabo Delgado, Niassa na Nampula mwishoni mwa mwaka 2020, kulingana na Ofisi ya UN ya Uratibu wa Masuala ya Kibinadamu.