Jamal Khashoggi: Marekani kuchapisha ripoti ya mauaji ya mwanahabari huyo

Ikulu ya White House imesema kuwa Rais wa Marekani Joe Biden anapanga kuzungumza ''hivi karibuni'' na Mfalme Salman wa Saudi Arabia.

Hatua hiyo imekuja wakati mamlaka za Marekani ikijiandaa na kuchapisha ripoti kuhusu mauaji ya mwanahabari wa Saudi Arabia Jamal Khashoggi.

Bw. Khashoggi aliuawa mwaka 2018 katika ubalozi wa Saudia jijini Instanbul, Uturuki.

Bw. Biden amesema alitaka ''kutathimini upya'' mahusiano ya nchi yake na Saudi Arabia, akisema kuwa Marekani angependa zaidi kuwa na mazungumzo moja kwa moja na Mfalme Salman.

Lakini mwandishi wa habari wa BBC anasema kuwa mwanamfalme Mohammed ni maarufu sana miongoni mwa Wasaudia vijana na ni dhahiri kuwa ana udhibiti wa ufalme.

Rais aliyeondoka madarakani Donald Trump awali alikuwa akituhumiwa kuzibia masikio madai ya ukiukaji wa haki za binadamu unaohusishwa na mrithi wa Saudi Arabia, Mohammed bin Salman, lakini maswali yanabaki juu ya msimamo wa rais wa Marekani Joe Biden

Suala hilo limezua utata juu ya hatua za Mohammed bin Salman na jinsi suala hilo litashughulikiwa na serikali mpya inayoongozwa na Joe Biden, Mwanademocrat ambaye ni tofauti sana na Donald Trump.

Ombi la kinga, kulingana na Washington Post, lilikuwa limejikita katika kesi dhidi ya bin Salman iliyofunguliwa na Marekani dhidi ya Saad al-Jabri, afisa wa zamani wa ujasusi wa Saudia ambaye kwa sasa amekimbilia Canada.

Gazeti hilo liliongeza kuwa vyanzo visivyojulikana vilisema kwamba Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani iliwataka mawakili wa Sa'ad kuwasilisha nyaraka za kisheria kuthibitisha kesi yao, ili kuamua ikiwa watakubali ombi la kinga ya Bin Salman. Wakati ambapo Idara ya Sheria ya Marekani inafikiria kufungua kesi hiyo.

Wizara ya Mambo ya nje ya Marekani inatarajiwa kutuma ombi kwa maafisa wa Idara ya Sheria, ambao uamuzi wao uko katika ngazi ya juu.

Ikiwa kinga ya Bin Salman hatimaye itatekelezwa, itamaanisha kwamba jina lake litaondolewa kwenye kesi yoyote inayoihusisha Marekani.