Je, hatua ya Bobi Wine kuondoa shauri la kupinga ushindi wa Museveni ina maana gani kwa Tume ya Uchaguzi, Mahakama na wafuasi wake?

Kiongozi wa chama cha NUP nchini Uganda Bobi Wine

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha, Kiongozi wa chama cha NUP nchini Uganda Bobi Wine ameondoa shuri la kupinga matokeo ya uchaguzi wa rais Museveni
    • Author, Markus Mpangala
    • Nafasi, Mchambuzi, Tanzania

Kwa mara ya nne Mahakama ya Rufani imefifisha matumaini ya vyama na wanasiasa wa upinzani kupata haki baada ya shauri la kupinga matokeo ya uchaguzi yaliyotangazwa na Tume ya nchi hiyo na kumpa ushindi aliyekuwa mgombea wa chama cha NRM, Yoweri Museveni kutangazwa kuondolewa Mahakamani hapo.

Aliyekuwa mgombea wa urais wa chama cha NUP, Robert Kyagulanyi mwenye lakabu maarufu Bobi Wine ametangaza kuondoa shauri hilo licha ya kuwa na hoja 26 kibindoni, huku akiendelea na taratibu za Kimahakama kusajili, kusikilizwa na kuondoa.

Akizungumza jijini Kampala, Bobi Wine, NUP na timu ya wanasheria wakiongozwa na Medard Lubega Sseggona tarehe 23 Februari mwaka huu waliviambia vyombo vya habari kuwa uamuzi wa kuondoa shauri hilo umetokana na kukosa imani na Majaji watatu na mfumo mzima wa Mahakama, huku Jaji Mkuu akitajwa kuwa na mgongano wa maslahi baada ya kuwa Wakili wa Museveni katika kesi mbili za kupinga matokeo ya uchaguzi zilizopita nchini humo.

Walalamikiwa katika shauri hilo ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Tume ya Uchaguzi na Yoweri Museveni ambapo Bobi Wine amedai uchaguzi mkuu wa Januari 14 mwaka huu wa 2021 ulikuwa wa udanganyifu, ukiukwaji na uvunjaji wa sheria.

Hoja za Bobi Wine zinaungwa mkono na rais wa Marekani, Joe Biden na Jumuiya ya Ulaya ambapo kwa nyakati tofauti wametoa matamko kupitia wawakilishi wao wakidai watachukua hatua kali dhidi ya wote waliohusika kuharibu uchaguzi huo.

Duru za kisiasa zinabainisha kuwa matamko hayo mawili yalipokelewa kwa mshtuko na mamlaka za Uganda, hatua ambayo ilimlazimu Rais Museveni kukutana na ujumbe wa Ulaya, kama ambavyo wiki mbili zilizopita ujumbe huo ulivyokutana na Bobi Wine.

Kwa mujibu wa matokeo ya uchaguzi huo yaliyotangazwa na Tume, Yoweri Museveni alipata kura 6,042,893 sawa na asilimia 58.38, wakati Bobi Wine alipata kura 3,631,437 sawa na asilimia 35.08.

Ni sababu zipi zimechangia kuondolewa shauri hilo?

Mosi, Bobi Wine analalamikia Mahakama ya Rufani kupendelea upande wa watawala na haipo huru hali ambayo itamnyima haki.

Pili, mwanasiasa huyo hana imani na Majaji watatu kati ya 9 waliopangwa kusikiliza shauri lake, wakiongozwa na Jaji Mkuu Owiny-Dollo. Wengine ni Mike Chibita na Ezekiel Muhanguzi.

Tatu, kufyekwa kwa vielelezo vya ushahidi kutoka 137 ambavyo viliwasilishwa Mahakamani hapo hadi kubakiwa na 53, jambo ambalo limetafsiriwa kuwa ni mkakati maalumu wa kudhoofisha kesi hiyo.

Nne, kukamatwa kwa baadhi ya mashahidi muhimu ambao walitarajiwa kusimama kizimbani katika shauri dhidi ya Tume, Mwanasheria Mkuu wa serikali na Museveni.

Wafuasi wa rais Museveni wanasema kwamba amewahakikishia udhabiti katika taifa hilo la afrika Mashariki

Chanzo cha picha, EPA

Maelezo ya picha, Wafuasi wa rais Museveni wanasema kwamba amewahakikishia udhabiti katika taifa hilo la afrika Mashariki

Tano, Jaji Mkuu Alfonse Owiny-Dollo anatuhumiwa kuwa na uhusiano wa karibu na rais, hivyo kuwa na mgongano wa kimaslahi kwani amewahi kuwa wakili wa Museveni Mahakamani katika kesi za chaguzi mbili kupinga ushindi wake.

Licha ya juhudi za Wakili Hassan Male Mabirizi kuwasilisha hati ya pingamizi Mahakamani hapo kutaka Jaji Owiny-Dollo ajiondoe , Jaji huyo amekataa kujitoa kwenye shauri hilo.

Je, sheria inaagiza nini ili kuondoa shauri?

Sheria ya Uchaguzi wa urais nchini humo Kifungu cha 61 inaeleza shauri lolote litaondolewa katika Mahakama ya Rufani endapo kutakuwa na likizo ya mahakama na baada ya hapo itatolewa notisi kadiri inavyoagizwa na mahakama. Aidha, inafafanua kuwa shauri hilo likikubaliwa kuondolewa mlalamikaji atalazimika kulipa gharama za kesi.

Wakili wa upande wa utetezi, Oscar Kihika amemtaka Bobi Wine kuthibitisha madai yake na hata akiondoa shauri hilo atalazimika kulipa gharama zote za kesi. Bobi Wine atangaza kuwa atalipa gharama zozote atakazoagizwa na Mahakama hiyo.

Nini maana shauri hili kwa Tume ya Uchaguzi na Mahakama?

Kama zilivyo nchi zingine linapofika suala la uchaguzi mkuu, Uganda nayo imekuwa ikishuhudia malumbano makali juu ya uaminifu wa Tume yao (EC) na uhuru wa Mahakama ya Rufani kutoa hukumu za haki kwa vyama vya upinzani, ambavyo vinaituhumu kuwapendelea watawala.

Tafiti mbalimbali zinaonesha kumekuwa na uhaba wa uhuru katika Tume na viongozi wake. Taswira waliyonayo baadhi ya wapigakura na wanasiasa kwa ujumla ni mashaka juu ya mwenendo wa tume kusimamia uchaguzi huru na haki, na kuwa kiini cha udanganyifu wakati wa uchaguzi.

Kumekuwa na hofu inayoelezewa kuwa ushahidi ambao ungewasilishwa ungesababisha matatizo kwa uongozi wa Tume pamoja na kushusha heshima. Kuondolewa kwa shauri hilo kunanusuru mwenendo wa Tume unaotilia shaka kuwekwa hadharani.

Ikumbukwe wakati wa uchaguzi wa mwaka 2016 asilimia 89 ya kura za maoni zilitaka mabadiliko katika Tume na michakato yote ya uchaguzi mkuu. Aidha, tume hiyo imekuwa ikikabiliwa na utata kutokana na bajeti hafifu, udanganyifu wa majina ya wapigakura na vituo vya kupigia kura na uhesabuji wake.

Mwaka 2001, Kizza Besigye alishindwa kufurukuta Mahakama ya Rufani baada ya kushindwa jaribio la kupinga ushindi wa Yoweri Museveni. Mahakama ya Rufani ilitupilia mbali madai yaliyowasilishwa mezani.

Mwaka 2006 Jaji George Kanyeinamba aliongoza jopo la Majaji kusikiliza kesi ya kupinga ushindi wa Museveni. Mwaka 2011 kesi ya kupinga ushindi wa Museveni ilifunguliwa, licha ya Mahakama kukiri dosari kwenye baadhi ya taratibu za uchaguzi, lakini haikufuta matokeo ya uchaguzi.

Bobi Wine

Msuguano wa mwaka 2016 ndani ya Mahakama unatajwa kuwa huenda ukawa chachu ya kufanya uamuzi wa kupingwa matokeo ya uchaguzi mwaka huu ikiwa utatokea. Mwaka huo huo pia aliyekuwa mgombea wa urais Amama Mbabazi alishindwa baada ya madai yake ya kupinga ushindi wa Museveni kutupiliwa mbali Mahakamani na Jaji Mkuu Bart Katureebe.

Hatua hiyo ilisababisha wapinzani na wafuasi wa demokrasia kujenga dhana kuwa kumekuwa na upendeleo katika utoaji hukumu katika kesi mbalimbali pamoja na kulinda udhaifu mkubwa wa Tume na Mahakama.

Hoja hiyo inaungwa mkono na aliyekuwa mgombea urais kupitia chama cha FDC, Patrick Amuriat ambaye anadai mfumo mzima wa Mahakama Uganda haupaswi kuaminiwa.

Bobi Wine na mchezo wa kisiasa

Baada ya kumtikisa Yoweri Museveni kwenye kampeni za uchaguzi mkuu, kisiasa ilitarajiwa kuwa angekimbilia katika Mahakama ya Rufani baada ya matokeo kutangazwa kuwa ameshindwa kumwangusha kiongozi huyo.

Vilevile katika kipindi hicho cha kampeni Bobi Wine alikuwa kwenye malumbano makali na taasisi kama vile Tume ya Uchaguzi, Jeshi la Polisi na vyombo vya dola kwa ujumla akivituhumu kuwa vinakipendelea chama tawala.

Ushahidi ni matukio ya kukwamishwa katika mikutano ya kampeni na jeshi la polisi kwenye miji mbalimbali, kukamatwa kwa wafuasi wake, wanasiasa na mgombea urais mwenyewe Bobi Wine kisha kuwekwa rumande ni miongoni mwa mambo yaliyotikisa mfumo wa utawala nchini humo.

Kwa mantiki hiyo sehemu pekee ambayo ilikuwa haijaonja joto la kisiasa la Bobi Wine lilikuwa mhimili wa Mahakama. Ushahidi wa Bobi Wine kuionjesha joto lake Mahakama upo katika hotuba aliyotoa Februari 23 mwaka huu wakati akitangaza kuondoa shauri hilo. Alieleza nia ya kufungua ilikuwa ni kupata haki au kufichua mwenendo mbovu wa Mahakama.

Hatua ya kuondoa shauri hilo inawachanganya wapinzani wake kisiasa kwa kuwa walimtarajia mahakamani lakini yeye amebadili mbinu hivyo haijulikani nini atakifanya baadaye.

Kwa upande mwingine, msingi wa madai yake umejengwa kisiasa kiasi fulani kutatuliwa jambo hilo pasipo ushahidi usiotia shaka inakuwa vigumu. Kwamba madai ya kisiasa huwa hayapati utatuzi kisheria.

Vilevile kisiasa chama tawala kilikuwa kinatamba na kumfanya Bobi Wine kuwa nyuma yao, lakini sasa upepo umebadilika badala yake watawala sasa wanafuata nyuma ya NUP ili kujitetea na kujaribu kupambana naye.

Shauri hilo limedumu kwa siku 22 Mahakamani kati ya 45 zilizopangwa kusikilizwa na kutolewa hukumu. Hata mashauri mengine matatu, Kizza Besigye (mawili) na Amama Mbabazi (Moja) yote yalisikilizwa hadi mwishoni, lakini Bobi Wine ameleta aina mpya ya kushughulika na mhimili wa Mahakama. Kwa kiasi kikubwa miongozo ya kisiasa inayotumiwa na NUP ndiyo inaleta mshangao kwa wengi, na kutotilia shaka kuwa huu ni mchezo maridadi wa kisiasa.

Nini kitatokea baada ya shauri kuondolewa? Kimsingi hili ndilo swali kubwa kuliko yote wakati huu. Bobi Wine anaonekana amezichanga vema karata zake, hivyo wafuasi na wapinzani wake watajiuliza, ni mwelekeo upi au jambo gani litakuwa kipaumbele chake baada ya kuitikisa Mahakama.

Kwenye mkutano na vyombo vya habari amekaririwa akisema kushindikana kupata haki mahakamani watapeleka shauri hilo katika mahakama ya umma kutolea maoni na nini cha kufanya. Hii ni mbinu ya kisiasa ambayo inaendelea kumfanya awike na kutawala mijadala ya kitaifa kuliko chama tawala na mtawala wa sasa. Ni hesabu za kisiasa tu.