Mwanamfalme Harry na mkewe Meghan hawatarejelea tena shughuli za Kifalme

Mwanamfalme Harry na mkewe Meghan hawatarejelea shughuli za kifalme, kulingana na Makao ya Kifalme ya Buckingham.

Malkia amethibitisha kwamba Mwanamfalme Harry na mkewe Meghan "hawataendelea na majukumu yao ya kuhudumia umma".

Taarifa kutoka makao ya Kifalme imeongeza kuwa Mwanamfalme Harry na mkewe Meghan "bado wanasalia kuwa wanafamilia wanaopendwa".

Wawili hao wamesema "utoaji huduma ni kokote" na wamejitolea kuendelea kusaidia mashirika wanayowakilisha.

Mwanamfalme Harry na mkewe Meghan Januari iliyopita walisema kwamba watajiondoa kama "waandamizi" katika familia ya Kifalme na kuanza kufanya kazi ili waweze kujitegemea.

Mwanamfalme Harry na mkewe Meghan ambao sasa hivi wanaishi California, walijondoa rasmi katika majukumu hayo mnamo mwezi Machi kukiwa na mpango wa kupitia tena mipangilio hiyo baada ya miezi 12.

Uthibitisho huo kuna maanisha kwamba mwanamfalme Harry na mkewe Meghan watarejesha nafasi za kazi walizokuwa wameteuliwa za wanajeshi wa heshima na wadhamini wa Kifalme kazi ambazo zitagawanywa tena wanafamilia wengine wa Kifalme wanaofanyakazi .

Chini ya makubaliano ya mwaka jana, wanandoa hao waliacha kutumia majina ya hadhi ya Kifalme lakini Harry alisalia na nafasi yake kama mwanamfalme kwasababu nafasi hiyo ni ya kuzaliwa.

Kujiondoa kwao kulifuatiwa na majadiliano kati ya Harry na watu wa familia ya Kifalme.

Taarifa kutoka makao ya Kifalme ya Buckingham imesema: "Malkia ameandika kuthibitisha kwamba kujiondoa katika kufanyakazi kwenye Familia ya Kifalme haiwezekani kuendelea na majukumu na wajibu ambao unaandamana na maisha ya kuhudumia umma.

"Sote tumehuzunishwa na uamuzi wao, Mwanamfalme Harry na mkewe Meghan wanasalia kuwa wanafamilia wanaopendwa sana."

Tangazo hilo linawadia siku chache baada ya wanandoa hao kusema hadharani kwamba wanatarajia mtoto wao wa pili.

Pia watazungumzia uamuzi wao wa kujiondoa katika kazi za Kifalme kwenye runinga kupitia mahojiano na Oprah Winfrey mwezi ujao.

Tangu walipojiondoa katika utekelezaji wa majukumu yao ya Kifalme, wote wametia saini makubaliano ya kibiashara na kampuni kubwa za Netflix na Spotify.

Pia hivi karibuni mke wake alishinda kesi mahakamani iliyohusisha suala la faragha dhidi ya gazeti la Mail kwa uchapishaji wa kipande cha barua kwa baba yake.

Mapema mwezi huu, Harry pia alifanikiwa kumshtaki mwandishi wa gazeti la Mail kwa kumchafulia jina juu ya madai ya uongo "ya kupuuza" jeshi la Kifalme baada ya kujiuzulu majukumu yake katika Familia ya Kifalme.