Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Aliyekuwa Rais Afrika Kusini Jacob Zuma anakabiliwa na 'kosa la kuidharau mahakama '
Jaji mmoja nchini Afrika Kusini amesema anataka aliyekuwa rais wa nchi hiyo Jacob Zuma kuhukumiwa kifungo gerezani kwa kushindwa kufika mahakamani kujibu madai ya ufisadi.
Bwana Zuma, 79, alidharau ombi la kufika mbele ya tume ya uchunguzi ambayo mwenyekiti wake ni hakimu Ray Zondo.
Jaji amesema ukaidi wa Bwana Zuma kunaweza kusababisha kutotekelezwa kwa sheria na kwamba ataomba mahakama ya juu ya Afrika Kusini kumhukumu aliyekuwa rais kwa kosa la kuidharau mahakama kwa kitendo chake cha kukaidi wito wa kufika mahakamani.
Bwana Zuma amesema anaamini kwamba jaji Zondo alikuwa na upendeleo katika uamuzi alioutoa dhidi yake.
Awali, alikuwa ametaka jaji huyo kujiuzulu kama mwenyekiti wa jopo la uchunguzi wa kesi dhidi yake.
Jaji Zondo alitupilia mbali ombi hilo na kusema anafanya kazi yake bila upendeleo.
Takribani mashahidi 40 wamemuhusisha Bwana Zuma na madai ya ufisadi.
Miongoni mwa madai dhidi yake ni kuwa wakati wake madarakani, aliruhusu familia tajiri ya Gupta kupora mali ya serikali na kushawishi sera na uteuzi wa mawaziri.
Hata hivyo, Bwana Zuma na familia ya Gupta imekanusha madai hayo.
Mahakama ya kikatiba mwezi uliopita, ilitoa uamuzi wake na kusema kuwa Bwana Zuma analazimika kufika mbele ya tume hiyo.
Kufuatia hatua yake ya kutotii agizo la kufika mahakamani Jumatatu, hakimu Zondo amesema kila mmoja ana haki sawa mbele ya sheria na ikiwa Bwana Zuma ataruhusiwa kukiuka agizo la mahakama kutakuwa na athari kidemokrasia.
Bwana Zuma hajasema lolote kuhusiana na tukio hilo tangu jaji alipotoa uamuzi huo lakini awali aliwahi kusema kuwa haogopi kwenda gerezani.
Hata hivyo baadhi ya wanaomuunga mkono waliokuwa wamevaa mavazi ya kijeshi wamekuwa wakiandamana katika eneo la kijijini anakotokea na kuahidi kumlinda.
Bwana Zuma alilazimishwa kujiuzulu kama rais mwaka 2018 baada ya kukabiliwa na madai ya ufisadi katika kipindi chote cha miaka 9 ambayo alikuwa madarakani.
Mrithi wake, Cyril Ramaphosa, aliingia madarakani kwa kuahidi kutatua tatizo hilo.