Sani Abacha – mabilioni yalioibwa na aliyekuwa rais wa Nigeria yatafutwa

Chanzo cha picha, Getty Images
Wakati aliyekuwa rais wa Nigeria Sani Abacha alipoiba mabilioni ya madola na kufariki dunia ghafla kabla ya kutumia pesa hizo, kulipelekea kuanzishwa kwa msako wa kimataifa uliofanyika kwa miongo kadhaa.
Mwanamume aliyepewa kazi ya kutafuta pesa zilizoibwa amezungumza na mwanahabari wa BBC akimuelezea jinsi ambavyo shughuli hiyo imekuwa ikifanyika katika kipindi cha maisha yake.
Septemba 1999, wakili wa Uswizi Enrico Monfrini alijibu simu ambayo ilibadilisha maisha yake katika kipindi cha miaka 20 ijayo.
"Alinipigia simu usiku wa manane, kama inawezekana nikutane naye katika hoteli aliyokuwa kwasababu ya jambo muhimu sana alilotaka kuniarifu: Nikamwambia, 'Ni usiku lakini sawa tu nitakuja.'"
Sauti ya mtu aliyekuwa akizungumza naye ilisikika kuwa ya afisa wa juu katika serikali ya Nigeria.
'Unaweza kutafuta pesa zilizoibwa'?
Bwana Monfrini anasema afisa huyo alipelekwa Geneva na Rais wa Nigeria wakati huo, Olusegun Obasanjo, na alitumwa kwenda kutafuta pesa zilizoibwa na Abacha, rais aliyetawala nchi hiyo kuanzia mwaka 1993 hadi kifo chake 1998 kilichotokea ghafla.
Kama wakili, Bwana Monfrini alikuwa ameunda mtandao wa raia wa Nigeria aliokuwa na uhusiano mzuri nao tangu miaka ya 1980, waliofanyakazi katika makampuni ya utengenezaji wa kahawa, kakao na bidhaa zingine.
Alishuku wateja waliokuwa wanapendekezwa na aliyekuwa rais.
"Aliniuliza: 'Unaweza kutafuta pesa hizo na je unaweza kuzizuia? Unaweza kufanya maandalizi pesa hizi zikarejeshwa nchini Nigeria?'
"Nilisema: 'Ndio.' Lakini ukweli ni kwamba wakati huo sikujua kazi hiyo inahitaji muda gani kutekelezeka. Na nikalazimika kujifunza kwa haraka sana, kuifanya."

Chanzo cha picha, AP
Na ili kuanza kazi hiyo ya uchunguzi, polisi ya Nigeria ilimpatia maelezo kidogo juu ya akaunti za benki za Uswizi za aliyekuwa rais, ambazo zilishukiwa kuwa pesa zilizoibwa na Abacha na washirika wake ziliwekwa kwenye akaunti hizo, Bwana Monfrini aliandika katika kitabu alichokipa kichwa ''Kutafuta pesa zilizoibwa''.
Alisema kwamba uchunguzi wa awali uliochapishwa na polisi Novemba 1998, ulibaini kuwa zaidi ya dola milioni 1.5 ziliibwa na Abacha na washirika wake.
'Madola aliyoiba zilisafirishwa na malori'
Moja ya njia iliyotumika kubeba kiwango kikubwa cha pesa namna hiyo kulihitaji ujasiri.
Abacha angemuambia mshauri wake, amuombee pesa kwa ajili ya suala la usalama na hakuweka wazi pesa hizo zitatumika kwa njia gani.
Baada ya hapo angesaini ombi hilo na mshauri wake kulipeleka Benki Kuu moja kwa moja ambako alitoa pesa hizo, mara nyingi zikiwa ni pesa taslim.
Mshauri wake angechukua kiasi kikubwa cha pesa hizo na kuzipeleka nyumbani kwa Abacha.
Baadhi ya pesa zilikuwa zikipakiwa kwenye malori zikiwa noti za dola", ameandika Bwana Monfrini.
Hii ilikuwa moja ya njia ambayo Abacha na washiriki wake waliitumia kuiba kiasi kikubwa cha pesa.
Njia zingine zilizotumika zilikuwa ni pamoja na kutoa kandarasi kwa rafiki zake kwa thamani ya juu na kutaka makampuni ya kigeni kulipa kiasi kikubwa cha rushwa ili ziweke kuendesha shughuli zao nchini Nigeria.

Chanzo cha picha, Getty Images

Hili liliendelea kwa karibu miaka mitatu hadi kila kitu kilipobadilika pale Abacha alipofariki dunia ghafla akiwa na umri wa miaka 54, mnamo Juni 8, 1998.
Haijafahamika kama alikuwa na ugonjwa wa moyo au alipewa sumu kwasababu mwili wale haukufanyiwa uchunguzi baada ya kufariki dunia, kulingana na aliyekuwa daktari wake wa kibinafsi aliyezungumza na BBC.
Abacha alifariki dunia kabla ya kutumia mabilioni ya pesa aliyokuwa ameiba lakini maelezo kidogo tu ya benki yalitumika kama vidokezo kuchunguza pesa hizo zilifichwa wapi.
"Nyaraka zinazoonesha historia ya akaunti zake zilitoa maelekezo kidogo tu ya akaunti zake," amesema Bwana Monfrini.
Akiwa na taarifa hizo alipeleka suala hilo kwa mkuu wa sheria nchini Uswizi.
Na hapo ndipo alipopata mwanya.
Bwana Monfrini alifanikiwa kushawishi familia ya Abacha na washirika wake wa karibu kuanzisha uchunguzi wa kihalifu.
Hii ilikuwa ni hatua ya msingi kwasababu ilionesha machaguo mengine ya jinsi mamlaka zinaweza kukabiliana na akaunti zake za benki.

Sani Abacha ni nani?

Chanzo cha picha, AFP
- Alikuwa miongoni mwa jeshi wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe
- Alikuwa na jukumu muhimu katika mapinduzi yaliyotokea mara mbili kabla ya kuwa waziri wa ulinzi Agosti mwaka 1993
- Alikuwa rais kupitia mapinduzi ya kijeshi ya Novemba 1993
- Serikali yake ilishutumu unyanyasaji mkubwa wa haki za binadamu
- Nigeria ilijiondoa kutoka Jumuiya ya madola baada ya miaka tisa ya wanaharakati wa haki za binadamu mwaka 1995
- Alifariki dunia Juni 8, 1998 akiwa na miaka 54
- Alikuwa baba wa watoto 10

Kilichofuata mwanasheria mkuu alitoa tahadhari kwa benki zote Uswizi akizitaka zitoe maelezo ya akaunti yoyote ile iliyofunguliwa kwa jina la Abacha na washirika wake.
"Na ndani ya saa 48, asilimi 95 ya benki zote na taasisi zingine za kifedha zilitangaza walichonacho kile kilichoonekana kwa ajili ya familia."
Na hatua hiyo ikaweka wazi akaunti zote alizokuwa nazo duniani.
"Benki zikatoa maelezo kwa mwendesha mashataka huko Geneva na ningefanya kazi hiyo ya mwendesha mashtaka kwasababu hakuwa na muda wa kuifanya," Bwana Monfrini ameielezea BBC.
'Taarifa zilizopatikana kupitia akaunti za benki'
"Tuliona katika kila akaunti pesa hizo zimetoka wapi au pesa hizo zimeenda wapi.
"Maelekezo ya kina juu ya taarifa za malipo ya akaunti hizo pamoja na malipo mengine zilinipa maelezo zaidi ya malipo yaliyofanyika ama kupokelewa au kutolewa kwa nchi zingine.
"Tulikuwa na ushahidi wa aina mbalimbali vile pesa hizo zilivyokuwa zimetumwa maeneo mbalimbali, Bahamas, Nassau, na visiwa vya Cayman - na kwingineko."
Kutafuta mtandao wote aliokuwa nao Abacha ilikuwa kazi kubwa kwa Bwana Monfrini.
"Hakuna aliyeonekana kuelewa kazi hiyo yote ilihitaji juhudi kiasi gani. Nililazimika kulipa watu wengi, mahasibu na mawakili wengi tu kutoka nchi tofauti tofauti."

Chanzo cha picha, AFP
"Familia ya Abacha nayo walikuwa wanagombana na kunapigana vita kweli. Walikuwa wanapinga karibu kila kitu. Hatua hii ilichelewesha mchakato mzima."
Baadhi ya pesa hizo zilirejeshwa kutoka Uswizi baada ya miaka mitano.
Mwaka 2008, Bwana Monfrini aliandika kuwa, kiasi cha pesa dola milioni 508 zilipatikana katika familia ya Abacha kwenye akaunti za benki nchini Uswizi na kurejeshwa kutoka Uswizi hadi Nigeria kati ya mwaka 2005 na 2007.
Kufikia mwaka 2018, kiwango cha pesa ambacho kilikuwa kimerejeshwa Nigeria ni zaidi ya dola bilioni 1.












