Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Wanawake waliouliza maswali kuhusu sababu za wanaume kubaka
Kuhojiana na wabakaji kumeathiri sana ustawi wa Tara Kaushal.
Tangu alipoanza utafiti wake mnamo 2017, ameshuhudia msongo wa mawazo .Siku kadhaa, kulikuwa na machozi tu.
Jioni moja, si muda mrefu uliopita, alijikuta amejifungia peke yake katika chumba chake cha kulala huko Noida, kitongoji cha mji mkuu wa India, Delhi.
"Mwenzangu, Sahil, alikuwa nje, na alikuwa akijaribu kurekebisha," anasema.
"Alikuwa akigonga mlango ili kufahamu kama nilikuwa sawa, na nilikuwa ndani nikilia kwa sauti.
''Nilitambua kuwa nilihitaji tiba.''
Hata kabla ya kuanza utafiti wake, Tara alipata athari za unyanyasaji wa kingono. Alianza kuzungumzia hilo alipokuwa na miaka 16.
''Nilibakwa nikiwa na miaka minne,'' aliwaambia wazazi wake. '' Na mtunza bustani.''
Kufunguka huko kuliwaacha wazazi wake midomo wazi. Lakini kwake ilikuwa kama kufungua milango ya kupitisha maji.
Tangu wakati huo, Tara aliweza kuzungumza kwa uwazi kuhusu unyanyasaji wa kingono alioupitia, akizungumza kwenye mijadala ya wazi, akiwaambia marafiki zake na hata baadaye kuandika kitabu
''Ninafahamu jina lake. Ninajua anavyofanana. Ninakumbuka nywele zake za kujiviringa na damu kwenye gauni yangu ya buluu.''
Alipokuwa akikua, alifikiri kuhusu matukio mengine ya udhalilishaji wa kingono yanayofanyika kila siku. Alitaka kufahamu kwanini ilitokea
''Kitabu changu 'Kwa nini wanaume hubaka' ni safari ndefu ya binafsi na kitaalamu,'' ameiambia BBC.
Kuwasaka wabakaji
Ubakaji na unyanyasaji wa kijinsia umekuwa ukiangaziwa nchini India tangu 2012, wakati mwanafunzi anayesomea utaalamu wa mazoezi ya viungo mwenye umri wa miaka 23 alipobakwa na genge la wanaume kwenye basi lililokuwa kwenye mwendo huko Delhi.
Alifariki siku chache baadaye kutokana na majeraha aliyoyapata wakati wa shambulio hilo. Washtakiwa wanne walinyongwa mnamo Machi 2020.
Licha ya uchunguzi kuongezeka na adhabu dhidi ya watu wanaojihusisha nauhalifu huo, idadi ya matukio ya ubakaji yamekuwa yakiongezeka.
Kulingana na Ofisi ya Kitaifa ya Rekodi za Uhalifu, polisi walirekodi matukio 33,977 va ubakaji nchini India mnamo mwaka 2018. Lakini wanaharakati wanasema idadi ni kubwa zaidi, kwani matukio mengi hayaripotiwi.
Tara alitaka kujua zaidi kuhusu wale wabakaji ambao hawaripotiwi kamwe au kuhukumiwa. Alikutana na wanaume tisa kote nchini, ambao wote walikuwa wanatuhumiwa kwa ubakaji, ingawa hawajawahi kuchunguzwa rasmi na mamlaka.
"Nilitumia wakati katika mazingira yao ya nyumbani; kuwahoji na kuwafuatilia, na familia zao na marafiki," anaandika katika kitabu chake. "Nilikuwa nimejificha - nikiwa na jina tofauti na barua pepe zinazofanana na vitambulisho vya Facebook."
Alificha tatoo zake na alihakikisha amevaa kwa heshima kurta (kanzu ya jadi).
Tara alihakikisha anafuatana na mtafsiri, ambaye pia anamuelezea kama mlinzi. Alijifanya kuwa raia wa India kutoka Australia akitafiti sinema juu ya maisha ya wanaume wa kawaida.
"Maswali 250 niliyouliza na vitu nilivyoona vilikuwa sawa kwa wanaume wote, lakini sikuwaambia kamwe kuwa nilikuwa nikiwafanyia utafiti kwa sababu walitambuliwa kama wabakaji," anaandika.
Mwisho wa hayo, Tara aliondoka akitambua wazi: ''Wanaume hawa wanauelewa hafifu wa maana ya ridhaa au kufahamu ubakaji ni nini.''
Kuwatazama wabakaji kama 'watu wengine'
Tara alipoanza utafiti wake, alizungumza na wanawake kwenye mtandao wa kijamii kuhusu unyanyasaji wa kijinsia.
''Wanaume wawili miongoni mwa niliowafanyia utafiti hatimaye walijitokeza kwenye mazungumzo niliyokuwa nayo na wanawake hao.'' alisema.
Ilikuwa vigumu kuwapata wanaume wengine saba. Hivyo nilifika polisi, kwenye vyombo vya habari na mashirika yasiyo ya kujipatia faida na yale ya uchunguzi.''
Wanaume wengi walikwenda kuthibitisha au kutekeleza ubakaji wakati nilipofanya nao mahojiano.
Lakini ulikuwa uamuzi wa makusudi kutozungumza na wabakaji waliohukumiwa.
"Watu hawaishi kama visiwa - kumsoma mwanaume bila kusoma mazingira yake inaweza kuwa na kikwazo kidogo."
'Yeyote anaweza kuwa mbakaji'
Wote walikuwa na hadithi ya kusimulia ; mbakaji huyo ambaye alishiriki katika genge la ubakaji alisema alikimbia mara tu baada ya tukio hilo, Mfanya usafi katika sinagogi anasema ''alishawishika'' kumbaka mtoto wa kike mwenye miaka mitano na kijana mwingine anasema alikuwa na uhusiano na msichana mmoja lakini baadae alishutumiwa kubaka baada ya familia ya msichana kubaini kuwa wako pamoja.
Kwanini wanaume hubaka?
"Hakuna anayeweza kujibu swali hili kwa kuwa ni jinai kubwa amesema Dkt Madhumita Pandey. Mtaalamu wa elimu ya jinai anaeleza
"Baadhi walihusika kwenye genge la ubakaji, baadhi waliwajua wanaowabaka, wengine waliwabaka watu wasiowafahamu kabisa. Na pia kuna aina mbalimbali za wabakaji- walio na hasira, wakatili, na wale wanaotenda kama njia ya kuadhibu.
Lakini amesisitiza kuwa wanaume hawa wanaweza kuwa; waume, wafanyakazi wenza, marafiki wa karibu, wenza wa darasani na hata maprofesa.
Ametoa wito kwa jamii kushughulikia suala la unyanyasaji wa kijinsia, wakati anatumia wazo la profesa wa Uingereza Liz Kelly kwamba unyanyasaji wa kijinsia uko kwenye mwendelezo ambapo aina tofauti za unyanyasaji wa kijinsia zinaingiliana.
"Inatukasirisha kujua mbakaji ametoa maoni juu ya chaguo la mwathiriwa la nguo na kutumia kama kisingizio cha kumbaka. Lakini kwanini tumeshtuka sana?" Anauliza.
"Kwa nini inashangaza kwamba tabia ya kila siku ambayo sisi hurekebisha hutiwa chumvi na kisha hudhihirika kwa hali mbaya zaidi?"
"Ninapoishia kuzungumza na yule mbakaji, naona kwamba msamiati wao wa kijamii na visingizio vya vitendo vyao kwa kweli vinatoka kwenye tafsiri ya kijamii ambayo wamekulia''. Alisema Dkt Madhumita.