Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Kesi ya genge kubwa la uhalifu yaanza kusikilizwa Italia
Mamia ya raia wa Italia ambao ni wanachama wa genge la uhalifu lenye nguvu zaidi nchini humo watafikishwa mahakamani kwenye kesi ya uhalifu ambayo haijawahi kufanyika katika kipindi cha miongo kadhaa.
Wanachama wa genge hilo pamoja na maafisa wafisadi 355 walishtakiwa baada ya genge la uhalifu la 'Ndrangheta' kufuatiliwa kwa muda mrefu.
Zaidi ya mashuhuda 900 wanatarajiwa kutoa ushahidi wao na baadhi ya makosa yanayowakabili ni pamoja na mauaji, ulanguzi wa dawa za kulevya, unyang'anyi na utakatishaji wa fedha.
Kesi hiyo imeanza kusikilizwa Jumatano na inatarajiwa kuchukua kipindi cha miaka miwili.
Kesi hiyo inasikilizwa katika moja ya majengo maalum yaliyoboreshwa kusini mwa eneo la Calabria, lililopo eneo ambalo ni ngome ya genge la uhalifu la 'Ndrangheta.
Jengo hilo ambalo lilikuwa kituo cha mawasiliano ya njia ya simu katika mji huo wa Lamezia Terme, limebadilishwa na kuwa mahakama ili kutoa fursa kwa mamia ya watu ambao wangependa kusikiliza kesi hiyo.
Hakuna kesi yoyote ile inayohusisha genge la uhalifu ambayo imewahi kusikilizwa nchini Italia yenye washtakiwa wengi namna hiyo tangu miaka ya 1980.
Washitakiwa ni kina nani?
Tofauti na kesi zingine za awali zilizosikilizwa kutoka mwaka 1986 hadi 1992 na kulenga makundi makubwa ya uhalifu huko Sicily, kesi ya Jumatano inalenga genge moja pekee la familia ya Mancuso, ambalo linachangia pakubwa uwepo wa genge la uhalifu la 'Ndrangheta.
Genge la 'Ndrangheta sasa hivi ndio lenye nguvu zaidi nchini humo na familia ya Mancuso inasemekana kwamba mara nyingi hutekeleza shughuli zake katika mkoa wa Calabrian la Vibo Valentia.
Wakati wa kikao cha awali ilichukua zaidi ya saa tatu kusoma majina ya washitakiwa, shirika la habari la AFP limesema.
Majina hayo ni pamoja na wanasiasa, maafisa wa polisi na wafanyakazi wa umma pamoja na wanachama halali wa genge hilo.
Mshtakiwa wa ngazi ya juu ni mkuu wa familia hiyo kwa jina Luigi Mancuso, 66, maarufu kama "Mjomba".
Washitakiwa wengine inasemekana wanajulikana kwa majina ya utani ya "Mbwa mwitu", "mwili mkubwa" na "Blondie".
Idadi ya walioshitakiwa imeongezeka hadi zaidi ya 400 pale washukiwa 92 walioanza kushtakiwa walipojumuishwa.
Washukiwa hao ni pamoja na Giancarlo Pittelli, wakili na aliyekuwa seneta wa waziri mkuu Silvio Berlusconi wa chama cha Forza huko Italia.
Bwana Pittelli amekanusha kuhusisha genge la uhalifu la 'Ndrangheta na siasa ya dunia na taasisi nyingine zenye nguvu kama vile mahakama.
Washitakiwa wengi walikamatwa na polisi katika msako wa alfajiri nchini Italia, Ujerumani, Uswizi na Bulgaria Desemba 2019.
Ni mashtaka gani yanayowakabili?
Genge la uhalifu la 'Ndrangheta linaaminika kudhibiti usambazaji wa kiwango kikubwa cha dawa za kulevya aina ya kokeini kuingia Ulaya kutoka Amerika Kusini na kwingineko.
Lakini hati ndefu ya mashitaka dhidi ya mamia ya walioshtakiwa ina makosa mengine kando na ulanguzi wa dawa za kulevya.
Inajumuisha genge la uhalifu, mauaji, majaribio ya mauaji, unyang'anyi, utoaji mikopo yenye riba ya juu, utoaji wa siri za serikali na utumiaji mbaya wa madaraka.
"Kesi hiyo inathibitisha jinsi genge hilo la uhalifula la 'Ndrangheta' lilivyokita mizizi katika jamii," amesema Federico Varese, profesa wa masuala ya uhalifu kutoka chuo kikuu cha Oxford alipozungumza na shirika la habari la AFP.
"Inashutusha kuona kuna kundi kubwa la uhalifu namna hii kiasi kwamba linahusisha mamia ya wanachama wake katika kesi."
Mhusika mkuu katika kesi hiyo ni mwendesha mashtaka, 62, Nicola Gratteri, ambaye amekuwa akiishi chini ya ulinzi wa polisi kwa zaidi ya miongo mitatu.
Ameapa kuliangamiza "genge hili la 'Ndrangheta, ambalo linachukua maisha ya watu wengine".
Hata hivyo profesa Varese ameonya kuwa kesi hiyo haiwezi kuwa mwisho wa genge hilo.
"Mnaweza kuwafunga gerezani lakini ikiwa mtashindwa kutatua sababu ya chimbuko la genge hilo, litaanza genge jingine," amesema.