Brexit: Makubaliano mapya ya kibiashara kuanza kutekelezwa baada ya bunge kupiga kura

Makubaliano ya baada ya Uingereza kujitoa Umoja wa Ulaya kati ya pande hizo mbili kuanza kutekelezwa Alhamisi 23:00 baada ya kutiwa saini kuwa sheria.

Bunge liliunga mkono makubaliano hayo kwa haraka mno Jumatano, baada ya pande hizo mbili kufikia makubaliano mkesha wa Krismasi.

Uingereza inajiondoa katika soko la pamoja la Umoja wa Ulaya na umoja wa forodha lakini makubaliano hayo yanatamatisha uwezekano wa kodi kwa bidhaa.

Waziri Mkuu wa Uingereza Boris Johnson amewashukuru wabunge na kusema: "Hatima ya nchi hii muhimu sasa ipo mikononi mwetu."

Lakini wapinzani wanasema nchi hiyo itakuwa vibaya zaidi hata kuliko ilivyokuwa ikiwa kwenye Umoja wa Ulaya.

Kujiondoa kwa Uingereza kunatokea Januari 31, lakini hadi kufikia sasa Uingereza imeendelea kufuata sheria za biashara za Brussels.

Makubaliano hayo yamefikiwa muda mfupi tu kabla ya siku ya mwisho iliyowekwa kufanya hivyo na kutoa mwongozo mpya wa kibiashara na uhusiano wa kiusalama baada ya pande hizo mbili kutengana.

Hatua hii inawadia miaka minne na nusu tangu Uingereza ilipopiga kura ya kujiondoa Umoja wa Ulaya katika kura ya maamuzi.

Mambo ya msingi

  • Makubaliano ya Brexit yamefikiwa siku kidogo tu kabla ya siku ya mwisho iliyokuwa imewekwa. Hii inamaanisha Uingereza na Umoja wa Ulaya zinaweza kuendelea kufanya biashara bila kodi za ziada kuongezwa kwenye bidhaa.
  • Kipi kilichokuwa muda mrefu? Uingereza ilipiga kura ya kujiondoa Umoja wa Ulaya mnamo mwaka 2016 lakini ikajiondoa kwenye Umoja huo Januari 31, 2020, lakini viongozi walikuwa na hadi mwisho wa 2020 kufikia makubaliano ya kibiashara.
  • Bado kuna mabadiliko makubwa mbele. Ingawa yaliyofikiwa ni makubaliano mazuri ya kibiashara, pia kutakuwa na mabadiliko ya vile watu watakavyosafiri kati ya Umoja wa Ulaya na Uingereza na namna wanavyoishi na kufanyakazi.

Mswada wa siku za usoni wa EU wenye kuangazia makubaliano ya kibiashara Uingereza, uliungwa mkono katika hatua ya kwanza bungeni kwa kura 521 dhidi ya 73 Jumatano baada ya bunge kuitishwa tena kutoka mapumziko ya krismasi.

Baadaye, bunge la Seneti lilipitisha mswada huo baada ya kusomwa kwa mara ya tatu.

Katika mahojiano na mwandishi wa BBC Laura Kuenssberg, Waziri mkuu alisema kuwa makubaliano hayo yataruhusu Uingereza kufanya mambo kivyao lakini pia kuwa na biashara huru na Umoja wa Ulaya.

Wabunge wengi wa chama cha Labour walipiga kura kuunga mkono mswada huo baada ya kiongozi wao Sir Keir Starmer kusema "makubaliano hata kama ni kidogo ni bora kuliko kutokuwa na makubaliano kabisa".

Rais wa Tume ya Ulaya Ursula von der Leyen na rais wa baraza la Umoja wa Ulaya Charles Michel walitia saini makubalino hayo Jumatano huko Brussels.