Shambulio la shule Nigeria: Mamia ya wavulana waliotekwa 'waachiwa huru'

Mamia ya wavulana waliotekwa wiki iliyopita kutoka shule ya bweni kaskazini -magharibi mwa Nigeria wameachiliwa huru, mamlaka katika eneo hilo zimeambia BBC.

Msemaji wa gavana wa jimbo la Katsina amesema wavulana 344 wameachiliwa huru na kwamba wako katika hali nzuri.

Hata hivyo, ripoti zingine zinaashiria kuwa baadhi yao wamesalia mikononi mwa watekaji wao.

Shambulio hilo linadaiwa kutekelezwa na na wanamgambo la Boko Haram, ambalo awali lilitoa video ikiwaonyesha baadhi ya wavulana hao.

Katika taarifa yake, msemaji, Abdul Labaran, amesema wavulana hao walikuwa wakipelekwa katika mji mkuu wa mkoa wa Katsina, na hivi karibuni wataungana na familia zao.

Amesema video iliyotolewa na na Boko Haram ilikuwa ya kweli, lakini ujumbe unaonekana kutoka kwa kiongozi wa kikundi hicho Abubakar Shekau, ulikuwa wa kuiga.

Hapo awali mamlaka zilitoa idadi ndogo kuliko ile yiliyotolewa na wenyeji kama jumla ya vijana waliotekwa nyara na hadi sasa haijulikani ikiwa wote wako salama.

Gavana wa jimbo hilo Aminu Bello Masari alinukuliwa na shirika la habari la Reuters akisema, "tumepata wavulana wengi. Sio wote," huku chanzo cha usalama kililiambia shirika la habari la AFP wengine walibaki na watekaji wao.

Bwana Labaran alisema hakuna hata mmoja wa wavulana waliotekwa nyara aliuawa, huku maoni yake yakikinzana nay ale ya mvulana aliyeonyeshwa kwenye video hiyo ambaye alisema kuwa wengine waliuawa na ndege za kivita za Nigeria

Haijulikani jinsi kuachiliwa huru kwa wavulana hao kulitokea lakini habari hiyo imethibitishwa kwa BBC Hausa na afisa mwingine wa serikali ya jimbo hilo.

Ni nini kilitokea wakati wa shambulio?

Mashuhuda wanasema watu wenye silaha walikuja shuleni katika mji wa Kankara Ijumaa jioni wiki iliyopita, na wanafunzi wengi waliruka uzio wa shule na kukimbia waliposikia milio ya risasi.

Wengine walifuatiliwa na watu waliokuwa na silaha, ambao waliwadanganya na kuwafanya kuamini kwamba walikuwa wafanyikazi wa usalama, wanafunzi waliotoroka walisema. Mara tu wanafunzi walipokusanywa, waliamrishwa na kupelkewa msituni na watu hao waliokuiwa na silaha.

Siku ya Alhamisi, video ilitolewa ikiwa na nembo ya Boko Haram, ikionyesha baadhi ya wavulana, ambao wengine wanaonekana kuwa wadogo sana.

Mmoja wa wavulana alisema walitekwa nyara na genge la kiongozi wa Boko Haram Abubakar Shekau na kwamba wanajeshi wote wa serikali ambao walikuwa wametumwa kuwasaidia warudishwe.

Hali ni mbaya kiasi gani?

Boko Haram imekuwa maarufu kwa miaka kumi iliyopita kwa utekaji nyara wa watoto wa shule, ikiwemo ni pamoja na huko Chibok mnamo 2014, wakati wasichana wa shule karibu 300 walikamatwa. Jina la kikundi hicho hutafsiri kama "elimu ya Magharibi ni marufuku".

Hata hivyo, utekaji nyara huu umefanyika kaskazini mashariki mwa Nigeria, ambako ndio ngome ya Boko Haram.

Licha ya madai ya Boko Haram, serikali ya Nigeria imesema utekaji nyara wa Katsina ulifanywa na magenge ya eneo hilo ambayo yana uhusiano na kundi hilo.

Mashambulio na utekaji nyara umeenea kaskazini magharibi mwa Nigeria na mara nyingi hulaumiwa kwa majambazi, neno ambalo linatumika kuwatambulisha magenge yanayofanya kazi katika eneo hilo.

Shirika la Amnesty International linasema zaidi ya watu 1,100 waliuawa na majambazi katika miezi sita ya kwanza ya mwaka huu, huku serikali ikishindwa kuwafikisha mahakamani washambuliaji wao.