Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Boko Haram wathibitisha kuwateka wanafunzi
Kundi la wanamgambo wa Kiisilamu lenye makao yake nchiniNigeria, Boko Haram limesema limetekeleza vitendo vya utekaji nyara wiki iliyopita wa mamia ya wavulana wa shule katika jimbo la Katsina Kaskazini Magharibi mwa Nigeria.
Zaidi ya wanafunzi 300 hawajulikani waliko, lakini wengine waliweza kutoroka.
Mamlaka hapo awali zililaumu "majambazi" kwa shambulio hilo.
Boko Haram limekuwa maarufu kwa miaka kumi iliyopita kwa utekaji nyara kwenye shule, pamoja na huko Chibok mnamo 2014, lakini tukio hilo lilifanyika Kaskazini Mashariki.
Katika ujumbe wa sauti kuhusu utekaji nyara, kiongozi wake Abubakar Shekau alisema "kilichotokea Katsina sisi tunahusika" na kwamba kundi lake linapinga elimu ya Magharibi.
Mwaka huu mamia ya watu katika eneo la Kaskazini Magharibi mwa Nigeria wameuawa katika mashambulio ya kile mamlaka imeyaita magenge ya wahalifu, lakini hadi sasa haijulikani ikiwa walikuwa na uhusiano na Boko Haram.
Kundi hilo la wanamgambo limefanya uasi tangu 2009, hasa Kaskazini Mashariki mwa Nigeria. Maelfu ya watu wamekufa na mamilioni wamelazimishwa kuyaacha makazi yao.
Wanaharakati wamemkosoa Rais Muhammadu Buhari, ambaye jimbo lake ni Katsina, kwa kushindwa kusimamia operesheni ya usalama dhidi ya wanamgambo hao.
Wengine wamemshutumu kwa kutowaonesha huruma waathiriwa na familia huko baada ya video iliyowekwa mtandaoni Jumanne kumuonesha akitembelea shamba lake.
"Ni uzembe kabisa na tabaka tawala lisilojali, halielewi maana ya kutawala," Waziri wa zamani wa Elimu wa Nigeria Oby Ezekwesili alikiambia kipindi cha Newsday cha BBC.
"Hapa sisi ni kama nchi tu tunajionesha kabisa kama wasio na busara kabisa linapokuja suala la maisha ya wanadamu hasa ya watoto wetu," alisema, akiishutumu serikali kwa kuuita "ugaidi kuwa ujambazi".
Wakazi wanaoishi karibu na Shule ya Sekondari ya Sayansi ya Serikali huko Kankara waliambia BBC walisikia milio ya risasi saa tano saa za Nigeria wiki iliyopita Ijumaa, na kwamba shambulio hilo lilidumu kwa zaidi ya saa moja.
Wafanyakazi wa usalama katika shule hiyo waliweza kuwafukuza baadhi ya washambuliaji kabla ya polisi kufika, maafisa walisema.
Polisi walisema kwamba wakati wa majibizano ya risasi, watu wengine wenye bunduki walilazimika kurudi nyuma. Wanafunzi waliweza kuruka uzio wa shule hiyo na kukimbilia mahali penye usalama, walisema.
Karibu wanafunzi 800 walikuwa shuleni wakati shambulio hilo lilipotokea na zaidi ya 300 bado hawajapatikana - lakini haijulikani ikiwa wote wanashikiliwa na watekaji nyara.
Mvulana wa miaka 17 ambaye alifanikiwa kuwatoroka watekaji nyara aliiambia BBC idhaa ya Hausa jinsi alivyotambaa kwa maili kadhaa katika msitu.
Rais Buhari ambaye kwa sasa yuko Katsina kwa ziara binafsi alikuwa akiarifiwa kila saa kuhusu juhudi za kuwaokoa watoto hao, msemaji wake Garba Shehu alisema.
Watoto hao wanaamini kwamba wenzao 10 walichukuliwa na majambazi, lakini hili bado lilihitaji kuthibitishwa, Bwana Shehu aliiambia BBC.
Aliandika kwenye mtandao wa Twitter Jumanne akisema kwamba Gavana wa Katsina Aminu Bello Masari amekutana na kumjulisha Rais Buhari kuhusu operesheni ya kuwaachilia wanafunzi waliotekwa nyara.
Wazazi wengi wamesema wamewaondoa watoto wao kutoka shule hiyo, Gavana Massari pia aliamuru kufungwa kwa shule zote za bweni katika jimbo hilo.