Matokeo ya Uchaguzi Tanzania 2020: Huu ndio mwisho wa Maalim Seif kisiasa?

- Author, Rashid Abdallah
- Nafasi, Mchambuzi
Seif Sharif Hamad awali alikuwa mfuasi wa Chama cha Mapinduzi (CCM), kabla ya kuhama na kuwa mmoja ya waasisi wa Chama cha Wananchi (CUF), ambacho kilikuwa na nguvukwa upande wa Zanzibar kwa wakati wote kikiwa chini yake. Sasa yuko katika chama cha ACT Wazalendo.
Mkongwe huyo wa siasa bara na visiwani ameangukia tena pua katika uchaguzi wa mwaka huu. Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) imetangaza Maalim kapata 19% ya kura dhidi ya 76% ya mgombea wa CCM, Dkt. Hussein Ali Mwinyi.
Seif Sharif almaarufu Maalim Seif akiwa na umri wa miaka 76 sasa, amegombea kiti cha Urais kwa mara ya sita. Isivyo bahati, uchaguzi kaambulia kura kidogo zaidi kulinganisha na hizo chaguzi zilizopita.
Kukwama kwa hesabu zake za kisiasa
Mbinu za kisiasa za Maalim Seif zimeendelea kwenda kapa. Mwaka 2015 alisusia uchaguzi wa marudio visiwani Zanzibar kwa hesabu kuwa atapambania haki yake aliyoamini kaporwa akiwa nje ya serikali ya Umoja wa Kitaifa.
Juhudi zake zilikuwa ni pamoja na kuishinikiza ZEC imtangaze yeye kuwa mshindi wa uchaguzi ambao tume hiyo iliyafuta matokeo kwa njia za utata. Shinikizo hilo halikufanikiwa hasa baada ya tume kutangaza tarehe mpya ya uchaguzi wa marudio.
Vikao vingi vilifanyika kati ya Maalim Seif na viongozi wa CCM, wakijaribu kutatua mkwamo. Ila ajenda zilizokuwa zikijadiliwa kwa siri hazikuleta matokeo chanya wala muafaka kati ya upinzani na utawala.
Maalim aliitaka pia Jumuiya ya Kimataifa kuingilia kati jambo hilo. Juhudi zake zilikwenda mbali zaidi kwa kumuandikia barua kiongozi mkuu wa Kanisa Katoliki duniani, Papa Francis, Novemba 25, 2015 akimuomba kuingilia kati kwa kutumia ushawishi wake kutatua mgogoro wa Zanzibar kwa amani.
Sakata hilo lilikosa muafaka. Baada ya uchaguzi wa marudio CCM ikaendelea kuiongoza Zanzibar chini ya Dkt. Ali Mohammed Shein. Upande mwingine wa siasa Maalim akazidi kujiimarisha na chama chake cha CUF kwa ajili ya kukitoa madarakani chama hicho katika uchaguzi wa Oktoba 2020.
Kabla Oktoba haijafika, akiwa Katibu Mkuu wa CUF. Mgogoro wa kiuongozi ukazuka ndani ya chama chake. Mgogoro uliomlazimisha kukiacha chama hicho na kuhamia chama kichanga cha upinzani cha ACT Wazalendo, kilichopata usajili rasmi Mei 2014.
Ulipokaribia uchaguzi mkuu, jahazi la ushindi lilianza kwenda mrama baada ya majina ya wagombea wao wa ngazi Uwakilishi na Ubunge kuenguliwa na tume za uchaguzi (ZEC na NEC). Wagombea wa vyama vya upinzani waliwekewa pingamizi juu ya kasoro katika ujazaji wao wa fomu.
Ulipofika uchaguzi, mwenendo wa uchaguzi na kasoro zilizojitokeza, zilitoa kila dalili kwamba vyama vya upinzani havitokuwa na mavuno mazuri katika. Hatimae matokea ya tume yalionesha kushindwa vibaya kwa Maalim Seif na vyama vyote vya upinzani.
Juhudi za dakika ya mwisho za bwana Hamad, ilikuwa ni kuitisha maandamano katika kisiwa cha Unguja masaa machache kabla matokeo ya Urais kutangazwa. Lakini maandamano hayo yalizimwa kabla ya kuanza, huku baadhi ya viongozi wa chama chake wakijeruhiwa na wengine wakiendelea kutafutwa baada ya taarifa za kupotea kwao.
Chadema na ACT Wazalendo wametoa tamko la pamoja kupinga matokeo ya uchaguzi huu, wamelaani uvunjifu wa haki za binaadamu ambao umetendeka. Fauka ya yote wameweka azma ya kufanya maandamano yasiyo na ukomo kushinikiza uchaguzi mpya. Maalim ni sehemu ya tamko hilo. Kipi kinafuata? Muda utanena.
Maslahi ya kisiasa au wafuasi wake?
Kitendawili kikubwa kilichopo mbele yake, ni ikiwa atakubali kuingia katika serikali ya Umoja wa Kitaifa au atasusia na kuendelea kuwa nje ya mfumo huo wa serikali ambao yeye ni sehemu ya waasisi.
Kwanza tuweke kumbukumbu sawa. Kwa mujibu wa ripoti ya Human Rights Watch (HRW) inakisia watu 35 waliuwawakisiwani Pemba katika maandamano ya kisiasa ya mwaka 2001. Wapatao mia sita walijeruhiwa na takribani 2000 walikimbilia nchi jirani.
Katika juhudi za kupunguza maafa ya namna hiyo. Kamati ya maridhiano iliwafiki uwepo wa serikali ya umoja wa kitaifa. Tarehe 31/07/2010, Wazanzibari kupitia kura ya maoni walichagua kwa zaidi ya asilimia 60 kuongozwa kwa mfumo wa serikali hiyo.
Tukirudi katika kitendawili cha sasa. Maamuzi yoyote Maalim Seif atakayo yafanya yatakuwa na faida na hasara. Kuingia katika serikali hiyo kutamsaidia yeye na chama chake kujipanga upya kwa uchaguzi wa 2025 wakiwa katika uongozi ambao hupanga na kupangua kila kitu juu ya Zanzibar.
Pia, uamuzi wa kushirikiana na CCM utasaidia kurudisha maridhiano na kupunguza uhasama wa kisiasa ambao upo tangu mwaka 2015. Uhasama huo umetiwa petroli na namna uchaguzi ulivyoendeshwa hadi kupatikana matokeo yaliyowaacha wengi vinywa wazi.
Lakini upande mwingine wa shilingi, kususia serikali ya umoja wa Kitaifa kutamuongezea heshima kutoka kwa wafuasi wake hasa wale walioathirika kwa vipigo na kupoteza wapendwa wao katika uchaguzi huu.
ACT Wazalendo imetoa kauli juu ya mauwaji katika kisiwa cha Pemba na Nungwi, Unguja. Chama hicho kimevituhumu vikosi vya usalama kwa kuhusika na mauwaji hayo yaliyotokea kuanzia usiku wa kuamkia tarehe 27 Oktoba.
Kwa wafuasi wa chama hicho ambao wamepoteza wapendwa wao au kushambuliwa na kujeruhiwa, kushirikiana na serikali iliopo madarakani ni kama kudharau yale machungu waliyoyapata.
Hivyo Maalim ana mtihani mkubwa wa kimaamuzi mbele yake. Ni mtihani kati ya mipango ya kisiasa kuelekea 2025 au kubaki na wafuasi wake na kuiwacha CCM pekee iongoze nchi, huku akijua kuwa uchaguzi utakao kuja mambo yatazidi kuwa magumu.
Nimemuuliza mwandishi habari mkongwe ambaye ameripoti mara kadhaa chaguzi za Zanzibar, Mohammed Abdulrahman kuhusu mustakbali wa Maalim kisiasa.
Anasema; "kwa hakika mustakbali wake ni kitandawili na itategemea afya yake ukizingatia umri alionao. Hapa nafikiri wakati umewadia kuanza kujenga safu ya watakaoweza kujazanafasi yake".
Mwanzo wake
Seif Sharif Hamad alizaliwa Mtambwe, kisiwani Pemba, Zanzibar, Oktoba 1943. Alisoma elimu yake ya msingi na upili katika visiwa hivyo kabla ya kujiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kusomea shahada ya kwanza ya Sayansi ya Siasa.
Kabla ya kuwa mwanasiasa alikuwa Mwalimu aliyesomesha shule kadhaa Unguja na Pemba. Na hapo ndipo penye asili ya jina lake la Maalim kwa lafudhi ya Kizanzibari.
Hadi sasa bado ana ushawishi mkubwa katika siasa za visiwa hivyo vya wakaazi takribani milioni moja laki tatu na ushei.
Wakati anatangaza nia ya kugombea Urais kupitia ACT, alikiri uwepo wa sauti alizoziita chache zilizomtaka apumzike na kijiti hicho amwachie mtu mwingine. Swali ni, Je, sauti hizo zitapata nguvu sasa?
Hilo ni la kusubiri na kuona.












