Hopewell Chin'ono: Mwandishi wa Zimbabwe asimulia alivyofungwa mwezi mmoja kwa kufichua vitendo vya rushwa

Chanzo cha picha, Reuters
Katika mfululizo wa barua kutoka kwa waandishi wa habari mwanahabari wa Zimbabwe, Hopewill Chin'ono anaeleza namna gani alikabiliana uso kwa uso na athari za kusaidia kufichua kashfa ya rushwa mwanzoni mwa mwaka huu.
Nilikua nikitarajia kutokea kwa changamoto hiyo-hivyo wakati wanaume wanane, baadhi wakiwa na silaha za aina ya AK-47, waliwasili kwenye geti langu wakiwa na gari ambalo halikutambulika mara moja saa za asubuhi tarehe 20 mwezi Julai, sikushangazwa.
Tahadhari moja ilikuja takribani wiki saba zilizotangulia, pale msemaji wa chama tawala aliponiita mimi ''sio mwaminifu'' na kunishutumu kuwa nilikuwa nalichafua jina la familia ya rais.
Hayo ni baada ya kuchapisha taarifa kuhusu kashfa ya ugavi kuhusu mamilioni ya dola za kupambana na Covid-19 mikataba ya manunuzi ya vifaa kwa gharama kubwa- Waziri wa afya baadae alifukuzwa kazi na sasa anakabiliwa na kesi kuhusu shutuma hizo.
Wakati maafisa wa serikali waliponiita nitoke nje ya nyumba yangu niliomba kuona hati ya kunikamata lakini hawakunionesha.
Badala yake walivunja dirisha la kioo cha chumba cha kulia chakula kwa silaha, na kupita kuingia kwenye chumba change cha kulala ambako nilikuwa nikiwasubiri na simu yangu ambayo niliitumia, kulirusha mubashara tukio lao la kuvunja na kuingia nyumbani kwangu.
Niliburuzwa nje ya chumba changu nikiwa peku, na kunitaka nipite njia ile ile waliyoingilia yenye vioo vilivyovunjikavunjika.
Huo ulikuwa mwanzo wa ndoto yangu ya kutisha ya siku 45.
Nilikuwa peke yangu, nilikamatwa siku moja na Jacob Ngarivhume, mwanaharakati wa kisiasa ambaye aliitisha maandamano ya amani dhidi ya vitendo vya rushwa.
Sote kwa pamoja tulishtakiwa kuchochea vurugu kwa kuwa niliidhinisha maandamano hayo kama vile katiba ya Zimbabwe inavyoruhusu raia kuandamana kwa amani-jambo ambalo serikali ya Rais Emmerson Mnangagwa mara nyingi imelipinga vikali.
Wakati tukiwa katika rumande katika gereza kuu la Harare, tulitembelewa na kiongozi mkuu wa upinzani wa Zimbabwe, Nelson Chamisa, ambaye tuliambiwa aliikasirisha ofisi ya rais.
Ugonjwa wa ngozi na kuhara
Hivyo, siku iliyofuata, tulibebwa kwenye gari na kupelekwa kwenye gereza lenye ulinzi mkali la Chikurubi, ambapo wahalifu hufungwa pingu mikononi na vyuma miguu wanapokwenda eneo jingine la gereza.
Jela ina uwezo wa kumudu wafungwa 1,360,lakini lilikuwa na wafungwa zaidi ya 2,600.

Chanzo cha picha, AFP
Kwenye chumba cha gereza, kilichopaswa kuwa na watu 16,lakini kulikuwa na wengine 44.
Hakukuwa na nafasi ya kugeuka wakati wa kulala, na wakati huo ni wakati wa maambukizi ya janga la Covid-19.
Wafungwa hawakuwa na barakoa kabisa, hakukuwa na maji tiririka wala sabuni kwenye vyumba vya gereza, walifungiwa kwa saa 17 kwa siku.
Kukiwa na taa moja, ilikuwa vigumu kusoma.
Wakati wa mchana tulikuwa kwenye uwanja, ambapo wafungwa 500 walitumia matundu mawili tu ya vyoo.
Kadhalika hukuwa na maji tiririka .
Wafungwa wengi walikuwa wakiugua kutokana na lishe duni- wakiugua maradhi ya ngozi na kuhara.
Kulikuwa na uji wa mahindi kwa ajili ya staftahi, chakula cha mahindi na maharage ya kuchemsha kwa ajili ya chakula cha mchana kilichokuwa kinapakuliwa saa nne asubuhi na jioni mahindi yaliyopikwa vibaya na kabichi ya kuchesha.
'Nilitokwa na machozi'
Nilianza kuugua juma la mwisho la mwezi Agosti nikiwa na homa kali- hospitali ya gereza haikuwa hata na dawa ya kuondoa maumivu .
Daktari wangu alipofika gerezani, hospitali haikuwa na kifaa cha kupima kiwango cha presha.
Wafungwa wengi wamegeukia imani ya kidini-na ilikuwa vigumu kupata usingizi kwa sababu ya watu kusali kwa sauti kubwa, ni chanzo pekee kwao kupata tumaini.
Baadhi yao wako huko kutokana na uhalifu walioufanya, kuna wengine wapo kwasababu ya uanaharakati wa kisiasa, baadhi walihukumiwa bila kuwepo kwa ushahidi.
Nilipaza sauti kwa wasimamizi wa magereza kuhusu hali ilivyo-tukapata taa nyingine tatu na baadhi ya barakoa- baadhi ya wafungwa walipimwa virusi vya corona.
Wafungwa wenzangu walishukuru. Baada ya kupatiwa dhamana tarehe 2 mwezi Septemba, nilitokwa na machozi wakati baadhi yao waliponitazama kabla sijaondoka na kusema: ''Tafadhali usitusahau.''
Nilihisi mapambano yangu dhidi ya rushwa yalikuwa yametambulika kuwa kweli.
Nilikuwa nikiandika kuhusu wizi wa fedha za Umma na nilipokuwa katika gereza la Chikurubi niliona jinsi taasisi hiyo ilivyokuwa na shida katika uwekezaji wake.
Taabu yangu pia ni kudhihirisha ugumu wanaokabiliwa nao waandishi wa habari wa uchunguzi nchini Zimbabwe.
Miaka mitatu tangu Robert Mugabe kuondolewa madarakani, vitendo vya kutekwa kwa watu waliokuwa wakionekana kuwa wakosoaji wa serikali vimekuwa kawaida.
Si kwamba hakukuwa na vitisho chini ya utawala wa Mugabe, lakini nilikuwa nina uwezo wa kuripoti taarifa bila kukamatwa, ikiwemo makala yangu iliyopata tuzo iliyozungumzia vurugu za baada ya uchaguzi mwaka 2008.
Wakati nilipokamatwa msemaji wa serikali alisema hakuna kazi iliyo juu ya sheria, Ninafikiri kuwa nia ya kukamatwa kwangu ni kuwatisha waandishi wa habari-na mpango huo unaonekana kufanikiwa.
Hivi karibuni nilikutana na wanahabari wachanga ambao walisema kuwa wana taarifa muhimu . Sababu yao ya kushindwa kuiripoti ni nini? ''Tunaogopa sana,'' walisema












